Bongo5 Makala

Makala: Usupastaa ni mzigo wa mwiba alisema Fid Q

Usupastaa una raha yake. Ile hali ya kupita mtaani na kila mmoja akigeuka kukuangalia kwa umakini akifurahi kukuona. Kama ni kwenye show, mashabiki hukufuata wakitaka kupiga picha na wewe ama kwa desturi za nchi kama Marekani watataka usaini autograph. Kama wewe ni mwanaume basi wasichana wengi wenye uzuri wa kila aina watataka wawe wapenzi wako.

SuperStar_2013_logo

Hizo ni dalili kwa msanii kuwa amefika kwenye kilele cha mafanikio. Pesa nyingi anazopata kutokana na shows na mauzo ya kazi zake humpa uwezo wa kununua vitu vingi vya thamani yakiwemo magari. Vipi pale usupastaa unaposhindwa kuendana na kipata chako? Hapo ndipo hugeuka kuwa mzigo mzito, tena wa miba kama alivyosema Fareed Kubanda.

“Aina ya maisha ya sanaa ya Tanzania Albert kafikisha ujumbe kwamba kumbe wasanii kuna vitu wanatakiwa wavipate ili waweze kuishi kama wasanii, “ anasema Afande Sele.

“Vinapokosena inakuwa ngumu sana kubeba jina ambalo huwezi kulitumikia. Kwa mtu wa kawaida sawa unaweza ukapanda bajaji ukapanda daladala watu wakachukulia poa. Lakini ukishakuwa supastaa mkubwa kwa mfano Albert Mangwea halafu ukipanda daladala, halafu haki zako unaona zinaibiwa inaweza kupelekea hata ukachanganyikiwa, ukichanganyikiwa inaweza ikapelekea kichaa au kifo ukasema zile bangi zile au maunga yale kumbe kuna vitu ambavyo vimekuwa mazingira ya yeye kuvipata,” anasisitiza Afande.

“Kwahiyo huo ni ujumbe kwa serikali inatakiwa icheck hati miliki inakuaje ili sisi wasanii tuweze kuishi kupitia majina yetu. Raia wa kawaida anaweza akachukulia poa tu kwasababu yeye anajua anaweza akapanda daladala tena mtu asishangae. Lakini leo mimi Afande Sele nikipanda daladala naonekana kafulia, inanifedhehesha. Kwahiyo najilazimisha kumiliki BMW au kumiliki Benz wakati uwezo hamna ilimradi uende tu sawa na jina lako.”

Pata picha upo kwenye stand ya daladala na ukashangaa unapigana vikumbo kupanda na kusukumana na mtu kama Ommy Dimpoz kwa mfano!! Ni wazi kuwa hutaamini macho yako na jibu utakalolipata haraka ni kuwa ‘mchizi amefulia.’ Ndio maana masupastaa hufanya kila wawezalo kumiliki usafiri wao ili kutunza hadhi zao.

Lakini utawezaje kutunza hadhi yako wakati huingizi pesa? Katika mazingira ya muziki wa Tanzania ambao hutegemea zaidi shows, ni wasanii wangapi wanapiga show za uhakika? Ukiangalia ni wachache na wengi ni wale wale. Mara yako ya mwisho umesikia Jay Moe amepiga show wapi na lini? Kama hana mishemishe mingine ya kumuingizia kipato ni lazima awe na stress.

“Kukosa fedha na kuweza kutimiza mahitaji ya maisha lazima uchanganyikiwe, unakimbilia vitu vitu suala za pombe au sijui madawa ya kulevya au nini inategemea na mtu moyo wako una nguvu kiasi gani cha kudhibiti hivi vitu,” alisema Majani kwenye mahojiano na TBC FM.

Suala analozingumzia Afande ndilo ambalo limepelekea wasanii wengi waliokuwa wakubwa kujiiingiza kwenye ulevi na hata matumizi ya madawa ya kulevya kwakuwa mifereji ya kipato kupitia muziki wao inakuwa imefungwa na hawana kazi zingine. Kama serikali na wadau wengine wa muziki nchini wangeweka mazingira mazuri ya kufanya matumizi ya muziki wa wasanii kwenye radio, TV na hata kwenye kumbi za starehe yawaingizie fedha, hali ingekuwa tofauti.

Mfano mzuri ni Kenya ambapo wasanii wengi wameendelea kunufaika na malipo ya mirahaba kutoka vyombo vya habari kutokana na kucheza kazi zao. Hiyo ndio maana hata Joh Makini alisema sanaa isiwe njia ya kutengeneza maskini wenye majina makubwa. Kutokana na mazingira haya mabovu ya kiwanda cha muziki nchini, wasanii wengi wakongwe wamelazimika kuvilalamikia baadhi ya vyombo vya habari kuwa vimechangia katika maanguko yao.

“Hivi vitu vingi vinaletwa kwasababu muziki wetu hauna mipango,industry yetu ipo very disorganized. Kwasababu hiyo inafanya watu wamekuwa wakubwa na wamekaa muda mrefu kwenye muziki na nguvu zinaanza kuwapungua wakati hawajafikia yale malengo na wanajiona hawana chochote,”alisema Mwana FA.

Producer wa Bongo Records, P-Funk Majani anadai kuwa marehemu Mangwea alijiingiza kwenye matumizi ya madawa ya kulevya kwakuwa licha ya kuwahi kutoa miongoni mwa albam bora kabisa za Bongo Flava, mpaka mauti yake muziki haujampa anachostahili na hivyo kumfanya asonononeke.

“I look in myself and I ask myself what is the reason for him to do this it was because psychologically he was unstable. Mangwea ni mtu ambaye amefanya vitendo vikubwa hapa nchini lakini ile faida na support a ukweli hajaipata,” alisema Majani.

“Ukiangalia wasanii wengine wa Bongo Records akina Juma Nature, Profesa Jay they got more leverage but Mangwea was a very big artist, he made one of the best ever albums in Tanzania till to date. I think that’s what drove him slowly in depression and people don’t use drugs unless they are depressed. Kwasababu mimi situation kama hiyo ilishawahi kunifikia.”

Ni kweli kuwa maisha sio rahisi kwa supastaa aliyefilisika. Supastaa wa aina hiyo aidha huonekana akilalamika kila siku ama akijikuta amekuwa mlevi na kupoteza kabisa mwelekeo wake. Kingine kinachowafedhesha ni kejeli za mashabiki kama alivyosema Afande Sele.

Kwakuwa si rahisi kubadilisha mazingira hayo magumu ya muziki wa Tanzania, wasanii wanatakiwa kufikiria nje ya box kwa kujielimisha kwenye fani mbalimbali ili muziki unapogoma waweze kuajiriwa ama kujiajiri wao wenyewe lasivyo ni ngumu sana kuwa supastaa maskini.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents