Siasa

Makali ya maisha yaongezeka

MAKALI ya maisha kwa wananchi yanazidi kuongezeka kutokana na bei ya bidhaa mbalimbali kuzidi kuongezeka, hali inayoelezwa kuwa inamwongezea ugumu wa maisha mwananchi wa kawaida.

Mwandishi Wa Habari Leo


MAKALI ya maisha kwa wananchi yanazidi kuongezeka kutokana na bei ya bidhaa mbalimbali kuzidi kuongezeka, hali inayoelezwa kuwa inamwongezea ugumu wa maisha mwananchi wa kawaida.


Gazeti hili limebaini kuwa kuanzia mwezi uliopita bei za vitu mbalimbali ambavyo ni vya msingi katika matumizi ya kila siku ndani ya familia bei zake zimeongezeka, hali inayowafanya wananchi kuishi kwa kujifunga mkanda.


Wakati bei hizo zinaongezeka, mfumuko wa bei kwa mujibu wa takwimu za Benki Kuu ya Tanzania (BoT) umeshuka kutoka asilimia nane ya mwezi Oktoba hadi kufikia asilimia 7.8 mwezi Novemba.


Katika jiji la Dar es Salaam, bei za vitu ambazo zimepanda ni unga wa sembe ambao gunia la kilo 50 linanunuliwa kwa Sh 23,000 badala ya Sh 18,000. Bei ya rejareja ni Sh 600 kwa kilo.


Mafuta ya kula lita 20 imepanda kutoka Sh 34,500 hadi kufikia Sh 40,000 na kipimo maarufu kama kibaba kimepanda kutoka Sh 100 hadi Sh 170.


Mkate unauzwa Sh 700 badala ya Sh 450 huku mkaa kipimo kimepanda kutoka Sh 500 hadi Sh 800.


Kipande cha sabuni ya kufulia kimepanda kutoka Sh 100 hadi Sh 200, wakati boksi la sabuni 10 linalokaa miche 10 linauzwa Sh 6,600 badala ya Sh 4,800.


Kibiriti nacho kimepanda bei kutoka Sh 20 hadi Sh 30 wakati chumvi kubwa inauzwa Sh 250 badala ya Sh 100. Chumvi ndogo kwa sasa inauzwa kwa Sh 120 badala ya Sh 50.


“Hali ya maisha inazidi kuwa ngumu, mshahara ni mdogo na vitu vinazidi kuongezeka bei,” alisema Mwalimu Rose Ngaiza.


Vitu hivyo katika familia ndivyo vinatumika kila siku. Lakini bei hizo zimepanda wakati kuna na vuguvugu la kupandisha bei ya umeme ambayo pia wachumi wanabashiri kuwa itachangia kupanda kwa bei za baadhi ya bidhaa.


Naibu Gavana wa Benki Kuu, Juma Reli, aliliambia gazeti hili jana kuwa vitu vinapanda bei kutokana na bei za mafuta ambazo hazishuki badala yake zinaendelea kupaa kila kukicha.


“Lakini cha ajabu vitu vimepanda bei, lakini sisi takwimu zinaonyesha kwamba mfumuko wa bei umeshuka kutoka asilimia 8 mwezi Oktoba hadi kufikia asilimia 7.8 mwezi jana,” alisema naibu gavana huyo.


Alisema pia thamani ya shilingi ya Tanzania imeimarika zaidi na sasa dola moja ya Marekani ni Sh 1,150 badala ya Sh 1,300 za awali.


Alisema kuimarika kwa thamani hiyo kunatafasiriwa kiuchumi kuwa bei za bidhaa zinazoagizwa kutoka nje ya nchi zinafaa zipungue bei na sio kuendelea kupanda.


Naibu gavana huyo alisema bidhaa ya petroli pia inatakiwa kushuka bei kutokana na kuimarika kwa thamani ya shilingi. “Lakini cha ajabu hapa kwetu bei zinaendelea kupaa, sisi hilo hatuhusiki na eneo hilo.”


Hata hivyo, uchunguzi uliowahi kufanywa na Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura) umebaini kuwa malipo na ada mbalimbali zinazotozwa kwenye mafuta yanayoagizwa kwa ajili ya huduma zinazotolewa na taasisi mbalimbali nchini yanaongeza mzigo wa bei kwa mnunuzi.


Ada hizo hutozwa kwa misingi ya ama thamani ya shehena ya mafuta, viwango thabiti (fixed rates), au kwa kuzingatia ujazo wa shehena. Aidha, baadhi ya taasisi hutoza ada hizo kwa kutumia viwango vya fedha za kigeni na wengine fedha ya Tanzania. Ada hizi huchangia katika mabadiliko ya mara kwa mara ya bei za bidhaa za mafuta ya petroli.


Reli alionya kuwa iwapo umeme utapanda bei, wazalishaji wengi pia wataongeza bei kwa bidhaa mbalimbali ili kufidia gharama hizo za nishati.


Kwa upande wake Waziri wa Fedha Zakia Meghji alipotakiwa kuzungumzia kasi ya kupanda kwa bei, yeye alijibu, “Hayo mambo tunaulizwa kila siku lakini cha msingi hapo angalia uchumi unavyoimarika.”


Waziri huyo alisema mfumuko wa bei umeshuka, lakini pia akazungumzia tatizo la kupanda kwa bei za mafuta katika soko la dunia kuwa pia kunaathiri kupanda kwa bidhaa mbalimbali nchini.


“Unajua kuna watu wenyewe wanapandisha tu bei, hao ni walanguzi,” alisema Meghji ambaye hakutaka kuzungumzia suala hilo kwani alisema lengo la serikali ni kuleta ahueni ya maisha kwa wananchi wake.


Wakati Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha wa 2007/08 ikitangazwa, kima cha chini cha mshahara wa mfanyakazi kiliongezwa kutoka Sh 75,000 hadi Sh 84,000 kwa mwezi.


Kiasi hicho kililalamikiwa na Shirikisho la Vyama Huru ambalo lilitaka kima hicho kifikie Sh 312,000 kwa mwezi kutokana na kupanda mno kwa gharama za maisha.


Hivi karibuni Askofu Mkuu Mstaafu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKKT), Dk Samson Mushemba alimwomba Rais Jakaya Kikwete kufanya mikakati ya kupunguza bei za vitu.


Askofu huyo alizungumza mbele ya Rais wakati wa kumsimika Askofu mpya Alex Malasusa, kuwa watu wengi hasa maeneo ya vijijini wanazidi kuwa maskini kutokana na kupanda kwa gharama za vitu.


Source: Habari Leo

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents