Habari

Makontena yapita bila kukaguliwa Dar

TANZANIA iko hatarini kuingiza bidhaa zitakazoweza kuwadhuru raia wake, kufuatia Kampuni tanzu ya COTECNA, TISCAN inayojishughulisha na ukaguzi wa mizigo

Na Peter Edson

 

 

 

TANZANIA iko hatarini kuingiza bidhaa zitakazoweza kuwadhuru raia wake, kufuatia Kampuni tanzu ya COTECNA, TISCAN inayojishughulisha na ukaguzi wa mizigo bandarini jijini Dar es Salaam kuacha kutumia tekinolojia ya kisasa kuchunguza bidhaa zilizomo ndani ya makontena, imefahamika.

 

 

 

Akitembelea bandari hiyo juzi Kitengo cha huduma ya upakuaji wa mizigo Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk Diodorus Kamalla alihoji uongozi TISCAN kama wana utaratibu wa kuyachunguza kwanza makontena hayo kabla ya kuchukuliwa.

 

 

 

Waziri huyo, pia alitaka kujua kwa undani kuhusu utaratibu ambao TISCAN imekuwa ikitumia kubaini bidhaa hatarishi, ambazo hupitia katika bandari hiyo na zenye uwezo wa kuleta madhara kwa wananchi kwa njia moja au nyingine.

 

 

 

Akijibu hoja hiyo mmoja kati ya viongozi wa juu wa kampuni hiyo, alimueleza Waziri Kamalla kuwa, kwa sasa hakuna utaratibu wowote ambao unatumiwa kuchunguza makontena na bidhaa zingine na kuongeza kuwa, unaandaliwa ili huduma hiyo ya uchunguzi ianze kutumika.

 

 

 

Akizungumza na wafanyakazi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA), waziri huyo, alisema ili kupunguza msongamano katika bandari hiyo, ni vema viwango vya ushuru wa makontena vikapandishwa.

 

 

 

Awali makontena hayo yalikuwa yakilipia ushuru wa dola 20 hadi 40 kwa siku kulingana na ukubwa na kupelekwa kwenye ghala za nje ambako kiwango hicho hupanda zaidi ya mara tatu.

 

 

 

Kamalla, alisema ushuru uliopo ni mdogo na kwamba haumshawishi mmiliki kuchukua kontena lake mapema kwani wengi wao, wana uwezo wa kulipia yakiwa bandari tofauti na yakiwekwa kwenye ghala za nje.

 

 

 

Alisema viwango vya nje ambavyo viko juu vimekuwa vikiwafanya wamiliki hao kuchukua hatua haraka ya kuyakomboa makontena yao, ili kuepuka gharama nyingi ambazo wangetozwa wakati wa kuchukua .

 

 

 

“Wamiliki wengi makontena yao yanakuwa tayari yamekaguliwa na kulipiwa kodi, lakini hawayatoi…jambo hili linaongeza msongamano wa mizigo bandarini,ukiwatoza zaidi watashawishika kuyachukuwa mapema,”alisema Dk Kamalla.

 

 

 

Naye Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Ephraim Mgawe, alisema viwango vipya vitaanza kutumika hivi karibuni, baada ya kupitiwa na wataalamu na wadau wengine.

 

 

 

 

 

Mgawe, alisema ili kuambatana na kuanzishwa kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki, miundo mbinu ya bandari hiyo ni midogo kwani milango yake haiwezi kuhudumia meli kubwa, pia kina cha maji katika magati ni kifupi.

 

 

 

Alisema miundombinu kama barabara duni na mtandao wa reli usiokidhi haja ya nchi jirani zinazozizunguka bandari nchini, umekuwa kikwazo kufanikisha utekelezaji wa sera za bandari hiyo, kwani mara nyingi mizigo hutumia muda mwingi kusafirishwa.

 

 

 

Mbali na hapo, alisema kuwa kucheleweshwa kukaguliwa kwa bidhaa zinazosafirishwa kwenda nchi za jirani kwenye mipaka, nako kunachangia kuendelea kuwepo kwa msongamano wa mizigo mingi katika bandari hiyo.

 

 

 

Alisema ni vema ukawepo utaratibi wa mipakani ili kupitisha mizigo kwa haraka, ili kuwapa fursa madereva kutumia muda mfupi kuchukuwa mizigo na kuifikisha eneo husika na kisha kurudi kwa ajili ya kupakia mizigo mingine.

 

 

 

Source: Mwananchi

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents