Siasa

Mama aomba msaada wa Rais Kikwete

Mama aomba msaada wa Rais Kikwete
Mama mzazi wa kijana Ibrahim Said aliyempiga kibao Rais mstaafu Mwinyi,
alitinga Baraza la Waislamu Tanzania (Bakwata) kumsihi Mufti wa
Tanzania, Sheikh Issa Bin Shaaban Simba, akamuombe Mzee Mwinyi na Rais
Jakaya Kikwete kumnusuru kijana wake kwa vile afya yake hairidhishi
gerezani.


Mama huyo mkazi wa Mabibo jijini Dar es Salaam alifika katika ofisi za Bakwata, Kinondoni baada ya kutoka Gereza la Keko kumuona mtoto wake.
Akizungumza na waandishi huku akibubujikwa na machozi, Rehema alisema hali aliyomkuta nayo mwanaye ni mbaya na hairidhishi.Ibrahim Said (26) alihukumiwa kifungo cha mwaka mmoja jela kutokana na kosa la kumshambulia kwa kumnasa kibao Mzee Mwinyi, alipokuwa akihutubia Baraza la Maulid lililofanyika katika Ukumbi wa Diamond Jubilee, jijini Dar es Salaam Machi 9 mwaka huu.

Rehema alidai kijana huyo anaumwa na amevimba mwili kutokana na kipigo na adhabu nyingine anazopata katika gereza hilo."Nimekuja kumuomba Mufti akamuombe Rais, mwanangu apunguziwe adhabu au ikiwezekana amsamehe na kutoka gerezani, kwa kuwa yeye ni mkuu wa nchi na anayo mamlaka hayo,” alisema na kuongeza:
"Kosa alilofanya mwanangu ni kama ajali tu, na yeyote inaweza kumpata. Lakini naumia sana kutokana na hali aliyonayo gerezani hata kutembea hawezi anaburuzwa na kipigo kimeongezeka”.

Baada ya kufika kwa Mufti na kueleza matatizo yake, Sheikh Simba alimuamuru Afisa Habari wa Bakwata Issa Mkalinga kuita waandishi ili mama huyo aongee nao na kutoa malalamiko yake.
Kwa upande wake, Mufti Simba aliahidi kuyafikisha maombi ya mama huyo kwa Rais Kikwete na Mzee Mwinyi.
"Mimi niliomba radhi siku ile ile kwa Mzee Mwinyi na yeye alimsamehe, lakini Ibrahim ameshitakiwa na Jamhuri wala si mzee Mwinyi. "Malalamiko na maombi yake kuhusu mateso anayoyapata mwanaye, mimi nitayachukua na kuyafikisha kwa Rais Kikwete na Mzee Mwinyi ili aweze kutendewa haki huko aliko,” alisema Mufti Simba.

Wakati huo huo, Baraza Kuu la Jumuiya na Taasisi za Kiislamu (T), limemtaka Mzee Mwinyi kumtoa gerezani kijana huyo aliyefungwa mwaka mmoja kwa kosa la kumshambulia Mwinyi kwa madai kuwa ndiye alimpandisha hasira kwa kuwashawishi Waislamu kutumia kondomu.

Aidha, Baraza hilo limezindua rasmi mfuko maalum wa kumsaidia na familia yake katika kipindi chote cha mwaka mmoja wa kifungo hicho, na Sh600,000 zilikusanya papo hapo.
Tamko hilo lilitolewa katika Baraza la Maulid ya kuzaliwa kwa Mtume Muhammad (S.A.W) lililoandaliwa na baraza hilo na kufanyika juzi ndani ya Msikiti wa Kituo cha Kiislamu Tanzania (TIC) Magomeni jijini Dar es Salaam.
Akisoma maazimio ya baraza hilo yaliyosainiwa na Katibu Mkuu wa Kamati ya Kutetea Haki za Waislamu, Sheikh Ponda Issa Ponda, msemaji wa baraza hilo, Sheikh Salim Khator alisema Mwinyi ana wajibu wa kumtoa gerezani kijana huyo kwa kuwa yeye ndiye alisababisha kifungo chake.

Alisema suala la Waislamu kumsaidia mwenzao aliyepata matatizo ni la lazima na hivyo, wote wanapaswa kuwasilisha michango yao katika ofisi za baraza hilo kwa ajili ya kijana huyo.“Tunazindua rasmi mfuko maalumu utakaotumika kumuhudumia ustadhi Ibrahim na familia yake iliyobaki nyumbani,” alisema Khator.

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents