Habari

Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini (TMA) yatoa taarifa uwezekano wa kutokea Vimbunga pacha bahari ya Hindi

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa taarifa ya uwezekano wa kutokea kwa vimbunga pacha Magharibi mwa bahari ya Hindi upande wa kaskazini na kusini mwa Ikweta.

Mamlaka hiyo imetoa taarifa hiyo kupitia akaunti zake za kijamii ”Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) inatoa taarifa ya uwezekano wa kutokea kwa vimbunga pacha magharibi mwa Bahari ya Hindi upande wa kaskazini na kusini mwa Ikweta na hivyo kuwa na uwezekano wa kuathiri mifumo ya hali ya hewa nchini.” Imeandika TMA.

Mamlaka hiyo imeongeza kuwa ”Migandamizo hiyo midogo pacha inaelekea kuimarika na kuwa vimbunga katika Pwani ya Somalia (Upande wa Kaskazini mwa Ikweta ) na Kaskazini Mashariki mwa Kisiwa cha Madagascar (Kusini mwa Ikweta).”

”Aidha, mgandamizo mdogo wa hewa uliopo kusini magharibi mwa bahari ya Hindi (karibu na kisiwa cha Madagascar) unatarajiwa kuimarika na kuelekea kaskazini mwa kisiwa cha Madagascar, na hivyo unatarajiwa kusababisha ongezeko la mvua pamoja na vipindi vya mvua kubwa hususan katika baadhi ya maeneo ya Pwani ya Kaskazini ya nchi yetu kati ya terehe 5 na 6 Disemba 2019.”

”Mamlaka imeendelea kutoa tahadhari ya vipindi vifupi vya mvua kubwa kwa baadhi ya maeneo ya mikoa ya Dar es salaam na Pwani na angalizo la mvua kubwa kwa baadhi ya maeneo ya mikoa ya Kagera, Geita, Mwanza, Shinyanga, Simiyu, Mara, Tanga pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba, Rukwa, Mbeya, Songwe, Iringa, Njombe na Ruvuma.”

”Kwa upande mwingine, mgandamizo mdogo wa hewa katika pwani ya Somalia unatarajiwa kuendelea kuwa mbali na pwani ya Tanzania na hautarajiwi kuwa na madhara katika nchi yetu.”

”USHAURI: Wananchi wanashauriwa kuendelea kufuatilia taarifa za utabiri kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania na kuzingatia tahadhari zitakazotolewa na mirejeo yake pamoja na kupata na kuzingatia ushauri na miongozo ya wataalam katika sekta husika ili kupunguza athari zinazoweza kujitokeza.”

”Mamlaka ya hali ya hewa Tanzania inaendelea kufuatilia hali hiyo katika bahari ya Hindi pamoja na mwenendo wa mifumo ya hali ya hewa kwa ujumla na itatoa taarifa za mrejeo kila itakapobidi.”

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents