Habari

Manispaa Dar zanawa mikono

Halmashauri za Manispaa ya Kinondoni na Ilala, zimewatupia mpira wananchi kuwa, ni jukumu lao la kuzinusuru shule za sekondari za kata ambazo zinakabiliwa na matatizo lukuki ya ukosefu wa walimu, madarasa, vitabu na maabara.

Na Godfrey Monyo na Aneth Kagenda

 
Halmashauri za Manispaa ya Kinondoni na Ilala, zimewatupia mpira wananchi kuwa, ni jukumu lao la kuzinusuru shule za sekondari za kata ambazo zinakabiliwa na matatizo lukuki ya ukosefu wa walimu, madarasa, vitabu na maabara.

 

Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni, Bw. Noel Mahyenga alisema ni jukumu la wananchi kuzinusuru shule za kata katika hali ngumu zinazokabiliana nazo.

 

Alidai kuwa manispaa pekee haziwezi kuzinusuru shule hizo.
Kwa upande wake Ofisa Uhusiano wa Manispaa ya Ilala, Bi. Tabu Shaibu alisema wananchi wanahamasishwa kushirikiana kuhakikisha kwamba, shule hizo zinapata vifaa vinavyohitajika.

 

Akizungumzia hatua juhudi za manispaa yake kuzinusuru shule hizo, Bw. Mahyenga aliyasema bila kushirikiana na wananchi, Manispaa peke yake haitafanikiwa kuzitoa shule hizo katika hali ngumu ilizonazo.

 

Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili katika shule kadhaa za jijini hivi karibuni ulibaini kuwepo kwa matatizo mengi hali ambayo inachangia kushusha kiwango cha elimu kwa wanafunzi.

 

Alisema Manispaa yake ilitegemea kukusanya zaidi ya Sh. bilioni mbili kwa ajili ya kuboresha na kuanzisha shule hizo lakini ilishindwa kufanikiwa na badala yake ilifanikiwa kukusanya kiasi kisijozidi Shilingi bilioni moja.

 

Aidha alisema kutokana na pengo hilo na mambo mengi kutofikia katika kiwango walichokusudia wamelazimika kusitisha baadhi ya miradi ya manispaa.

 

“Fedha nyingine tulizokuwa tunalazimika kufanyia mambo mengine ya maendeleo tumelazimika kuzitumia kwa ajili ya shule hizo za kata,“ alisema Bw. Mahyenga.

 

Hata hivyo jitihada za kumpata Mkurugenzi wa Manispaa ya Temeke hazikuzaa matunda baada ya kuambiwa yupo safarini mkoani Arusha.

 

Kwa upande wake, Ofisa Uhusiano wa Manispaa ya Ilala, Bi. Tabu alisema wanaendelea kupeleka madawati na walimu katika shule zote za sekondari za kata zilizopo katika manispaa yake.

 

Alisema hayo kufuatia habari zilizochapishwa na gazeti hili jana kuelezea matatizo yanayozikabili shule za sekondari za kata.

 

“Ni kweli vitu hivyo muhimu vinahitajika lakini shule za kata yangu zinaendelea kusambaziwa madawati na nina imani kuwa itafikia mahali tutakuwa hatuna shida ya madawati na walimu wanaongezeka,“ alisema Bi. Shaibu.

 

Alisema walikuwa wametengeneza madawati kutosheleza wanafunzi na meza kwa mwaka jana lakini mwaka huu walilazimika kuongeza kwa kuwa idadi ya wanafunzi walioanza masomo yao iliongezeka.

 

Alisema mwaka jana walitengeneza madawati 7,160 kwa wanafunzi wote waliokuwepo kwenye mashule na sasa yaliyotengenezwa ni 9,000 lakini bado yanahitajika mengine.

 

Aliongeza kuwa, idadi inayohitajika ya madawati ni 3,515 yaliyopo ni 2,896 na kwamba wanao upungufu wa madawati 616.

 

Alisema walimu waliopo kwenye mashule hayo ni 589, wanapungua 128 na wanahitajika 717 na kwamba wanaendelea kuleta wengine.

 

Aidha Bi. Shaibu alisema kuwa wazazi wanaamasishwa kuchangia wakishirikiana na Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Msingi (MMEM) ili kufanikisha zoezi hilo.

 

Alisema pamoja na wazazi na MMEM, lakini pia wanaendelea kuwahamasisha wananchi katika upatikanaji wa madawati.

 

Naye mwandishi wa PST Kisarawe, Ally Hengo anaripoti kuwa, Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe, mkoani Pwani, imenunua madawati 1,000 kwa ajili ya shule 11 za sekondari zilizomo wilayani humo ili kukabili tatizo la upungufu mkubwa wa samani hizo.

 

Kaimu Afisa Elimu wa Wilaya ya Kisarawe, Bw. Hassan Danga, alisema madawati hayo yaliyogharimu jumla ya Sh. milioni 60, yataanza kugawanywa kwenye shule zilizopangiwa mgao huo kuanzia wiki hii.

 

Aidha, Bw. Danga amezitaja shule hizo za sekondari zitakazo nufaika na mgawo huo kuwa ni Chanzige, Maneromango, Gongoni, Kibuta, Masaki, Mfuru, Msimbu, Mzenga, Makurunge, Chole na Janguo.

 

Aliongeza kuwa kufuatia kununuliwa kwa madawati hayo kwa kiasi kikubwa kutapunguza uhaba wa madawati kwa wanafunzi, na kuwaagiza walimu wakuu kuhakikisha hayaharibiwi kwa njia yoyote wakati halmashauri hiyo ikijitahidi kuondoa kabisa uhaba huo.

 

Afisa Elimu huyo aliwataka walimu hao iwapo watawabaini wanafunzi watakao yaharibu madawati hayo kwa makusudi kuwachukulia hatua kupitia kwenye bodi za shule zao ili kuhakikisha mali za shule zinalindwa kikamilifu.

 

Wakati huo huo, jumla ya majina 49 ya wanafunzi yatima na ambao wazazi wao hawana uwezo wa kuwalipia ada, yamewasilishwa ofisi ya elimu toka serikali za vijiji 76 wilayani hapa, kwa ajili ya zoezi la kulipiwa ada hiyo na serikali kuu.

 

Bw. Danga alisema kati ya wanafunzi hao wa kidato cha kwanza mwaka huu, tayari idara yake imeshayafanyia uhakiki na kuyawasilisha ofisi ya Ofisa Elimu Mkoa wa Pwani kwa hatua zaidi.

 

 

 

Source: Nipashe

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents