Habari

Manji aitema Coco Beach

Mfanyabiashara maarufu Yusuf Manji na Mkurugenzi wa Kampuni ya Quality Group amemuomba radhi Rais wa Jamhuri ya Tanzania, Dkt John Pombe Magufuli kutokana na kesi aliyoifungua akidai kupewa haki ya uwekezaji katika eneo la Coco Beach lililopo jijini Dar es Salaam.

Manji alishinda zabuni iliyotangazwa na Manispaa ya Kinondoni mwaka 2005, kwa ajili ya uwekezaji wa eneo la Coco Beach karibu na Bwalo la Maofisa wa Polisi lililopo Oysterbay.

Manji ameeleza hayo kupitia taarifa yake kwa vyombo vya habari ambapo alisema licha ya kampuni yake kupitia kampuni ya Q-Consult kuingia makubaliano na Manispaa ya Kinondoni Desemba 21, 2007 kulikuwa na ucheleweshaji wa mradi huo.

“Hali hiyo ilisababisha kampuni yetu kutafuta njia ya sheria katika Mahakama Kuu Kitengo cha Ardhi, Desemba 17, 2007 na kufungua kesi ya ardhi namba 334 ya 2009 ambapo baada ya miezi sita Mahakama Kuu iliagiza Manispaa ya Kinondoni kutekeleza ahadi yake,” alisema Manji.

“Kwa kutambua maelekezo ya Serikali ya Awamu ya Tano tunatii agizo na kuacha eneo hili liendelee kwa matumizi kama ambavyo linatumika sasa.Ninaomba radhi binafsi kwa Rais John Magufuli na Serikali yake kwa sintofahamu yoyote iliyojitokeza wakati wa ufuatiliaji wa jambo hili.”

Hata hivyo Manji alisema wamewaagiza mawakili wao kujitoa kama wapinzani katika rufaa iliyowekwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali na kutodai gharama zozote walizoingia au hasara ya mapato kwa kuwa masilahi yao sio halali ukilinganisha na manufaa ya jamii.

“Quality Group Limited inatambua na kuunga mkono juhudi zote za Rais Magufuli za kizalendo katika kusimamia rasilimali za nchi yetu,” alisema Manji.

Na Emmy Mwaipopo

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents