Maoni: Kimbiji (Bob Junior): Video bora kwa wimbo wa kawaida?

Naomba nikiri kuwa sikuwa nimeitazama video ya Bob Junior ya wimbo wake mpya, Kimbiji hadi jana jioni kwenye show ya 20 za Town ya Clouds TV. Nikiri pia video hiyo ilinivutia sana na moja kwa moja nikaiweka kwenye orodha ya video nzuri zilizotoka mwaka huu.

http://www.youtube.com/watch?v=oyJI9VMW8k4

Nimependa mambo kadhaa kwenye wimbo huu. Kwanza ni story nzuri inayooneshwa kwenye video hii. Ni story za kila siku zinazowakuta vijana wanaokuja mjini kutafuta maisha na mwisho wa siku wanakuta yale waliyokuwa wakitegemea yakiwa tofauti kabisa. Maisha magumu ya mjini huwafanya vijana wengi kutamani kurudi kijijini walikotokea ama wengine kuamua kuwa vibaka ama kutumbukia kwenye matumizi ya madawa ya kulevya.

Pili nimependa jinsi Bob Junior alivyouvaa uhusika. Kwa alichokifanya, Sharobaro huyu anapita moja kwa moja kwenye mchujo wa kuwa muigizaji mzuri, career anayoweza kuanza kuifikiria kwakuwa anaiweza.

Tatu nimependa location ya video hii. Toka wakati yupo kijijini, anapanda basi na kuja mjini, sehemu ya sokoni anayouza nyanya na kisha kukamatwa na mgambo, sehemu ya milima anapookena akiimba na kucheza, barabarani anapokutana na msichana anayempenda na kumchukua kumpeleka kwake na sehemu zingine.

Nne nimependa rangi ya video hii. Video ina rangi nzuri inayoyapendezesha sana mandhari ya ukijani yaliyotawala. Hakuna effects zisizo za maana kama nizionazo kwenye video nyingi za Kibongo nk.

Changamoto niinayo mimi kwenye wimbo huu (naweza nisiwe sahihi) ni wimbo wenyewe. Nahisi huu ni wimbo wa kawaida wenye video kali sana. Wimbo umetayarishwa na Man Walter wa Combination Sounds (Mtayarishaji bora wa muziki wa Bongo Flava wa tuzo za KTMA 2013).

Hii si mara ya kwanza Man Walter kufanya wimbo wenye asili ya dance. Amewahi kutengeneza hit single ya Ali Kiba, Dushelele. Kwa haraka haraka Dushelele na Kimbiji zina vitu vinavyofanana. Na zote Dushelele na Kimbiji ni dance chotara (nyimbo za dance ambazo hazijakidhi viwango vya kuwa dance kamili). Ni nyimbo zinazojaribu kusikika kama za dance lakini hazikidhi viwango vingi vya kuwa nyimbo za dance kwakuwa kwanza zimepigwa kwa vyombo vichache na hivyo zinasikika zikipwaya masikioni.

Naamini unafahamu jinsi nyimbo za bendi kama FM Academia, Twanga Pepeta na zingine zinavyosikika kwa ubora wa dance.
Bila shaka alichokifanya Man Walter ni kuita mtu mmoja ama wawili waliomsaidia kupiga solo bass guitar na kinanda kupiga yeye mwenyewe.

Ninahisi pia hata drums alizozitumia kwenye wimbo huu ni za kinanda na MIDI kilichounganishwa na software za kutengeneza beat kama Cubase, Reason ama FL Studio.

Kwa mkusanyiko kama huo, ni ngumu kutengeneza wimbo utakaosound vizuri masikioni kama nyimbo za dance tulizozizoea. Nikupe mfano mmoja. Chukua wimbo maarufu wa Twanga Pepeta (African Stars)- Mtu Pesa uliotoka zaidi ya miaka 6 iliyopita na kisha uulinganishe na Kimbiji, naamini utapata jibu la point tangu.

Mtu Pesa inasound vizuri kwasababu imepigwa live na vyombo vingi akiwemo mtu wa drums na sio drums za kwenye keyboard kama kwenye Dushelele na Kimbiji.

Ushauri kwa Bob Junior, kama anataka kutengeneza wimbo wenye mahadhi ya dance, basi akubali kuingia gharama kwa kuikodi bendi iliyokamilika ambayo itampigia vyombo na yeye ama producer mwingine akihusika na engineering tu. Bila kufanya hivyo, nyimbo zitakazokuwa zinatoka, zitakuwa zile zenye mahadhi ya muziki wa dance nusu.

Related Articles

Back to top button
Close
Bongo5

FREE
VIEW