Burudani ya Michezo Live

Maoni: Watangazaji 10 bora wa radio wa vipindi vya burudani Tanzania 2013

Hivi karibuni nilifanya mazungumzo na watangazaji wakongwe watatu nchini, Godwin Gondwe aka Double G ambaye kwa sasa ni lecturer wa chuo kikuu cha Tumaini na pia msomaji wa habari wa ITV na shughuli zingine, Sosthenes Ambakisye aka SOS B ambaye kwa sasa hayupo tena kwenye utangazaji na Basil Mbakile ambaye kwa sasa ni mtangazaji/reporter wa idhaa ya Kiswahili ya BBC.

headphones

Wote hawa kwangu ni miongoni mwa watu walionivutia kwenye kazi ya utangazaji (role models) na niliwatafuta kwa lengo la kutaka kushare nao hofu nilionayo sasa kwenye vipindi vya burudani katika redio nyingi za Tanzania. Hofu hiyo ni kuwa kwa mwaka 2013, vipindi vya radio vya burudani vimeshuka kwa kiasi kikubwa ukilinganisha na miaka iliyopita.

Kushuka kwake kunatokana na watangazaji wengi kufanya kazi kwa mazoea, kutojiandaa, kukosa vitu exclusive vya kuweka kwenye vipindi vyao, udhaifu katika kufanya interview na wasanii, uchaguzi wa nyimbo unaogubikwa na upendeleo hasa kwa wasanii wa nyumbani na mambo mengine. Wote kwa pamoja walikiri kuwepo kwa tatizo hilo.

Katika maongezi hayo ambayo mwakani naweza kuja kuyaandikia makala maalum kuhusiana na hilo, Godwin Gondwe aliniambia kuwa watangazaji wengi wanatanguliza umaarufu badala ya bidii ya kazi. Alisema watangazaji wengi hasa wa redio kubwa wamelewa umaarufu walionao ambao unawafanya wasijitume tena kama walivyokuwa wakifanya zamani.

SOS B alinieleza kuwa watangazaji wa sasa hawajiandai kabisa na hivyo vipindi vyao kushindwa kuwa na vitu muhimu vya kuwalisha wasikilizaji. Alimaanisha kuwa, vipindi vingi hukamilika na kumwacha msikilizaji bila kitu kinachoweza kumuongezea maarifa au elimu mpya kuhusu burudani na wasanii licha ya kuburudika.

Basil Mbakile alinieleza kuwa watangazaji wengi wanashindwa kuwa wabunifu kwakuwa wanakosa mapenzi ama ‘passion’ ya utangazaji na hivyo kuuchukulia utangazaji kama ajira kumpatia tu ujira.

Pamoja na hofu hiyo wapo watangazaji wa radio wanaoendelea kujituma kuvifanya vpindi vyao viwe bora zaidi. Kwa mwaka 2013, hawa ni watangazaji bora zaidi upande wangu na ambao naamini wataongeza bidii zaidi mwaka 2014 ili wawe bora kupita walivyokuwa mwaka 2013.

1. Millard Ayo – Amplifaya na Clouds FM Top 20

IMG_2490

Kwangu na kwa wengine wengi, Millard Ayo ndio mtangazaji bora zaidi Tanzania kwa sasa. Kwa miaka miwili mfululizo, 2012 na 2013, Millard amekuwa akiongoza kura za maoni za Bongo5 kuhusu mtangazaji anayesikilizwa zaidi Tanzania.

Godwin Gondwe anamchukulia Millard kama mtangazaji anayejituma zaidi kuliko wote Tanzania na kwamba kama angekuwa anafanya kipindi muda sawa na yeye, basi angekuwa anampa hofu sana. Naye mtangazaji mkongwe, Masoud Masoud wa TBC Taifa, aliwahi kusema kwenye kipindi cha Mkasi mwaka huu kuwa, Millard ndiye mtangazaji anayemkubali kwa sasa na humkumbusha enzi zake za ujana wake.

Japo si kituo chake cha kwanza kuanza kazi, jina la Millard lilianza kufahamika nchini kupitia kipindi cha Milazo 101 cha Radio One. Sauti yake yenye mamlaka na ubunifu hewani, ulikifanya kipindi hicho kuwa maarufu kuliko vingine vya burudani katika radio hiyo inayomilikiwa na kampuni ya IPP.

Kuondoka kwake Radio One kulikuwa ni pigo kubwa lakini lenye neema kwa Clouds FM. Alihamia Clouds FM na kuanzisha kipindi kipya kiitwacho Amplifanya ambacho kilichukua nafasi ya kipindi cha nyimbo za kiafrika, Bambataa. Haikuchukua muda kipindi cha Amplifanya kikawa miongoni mwa vipindi bora kabisa Clouds FM. Kipindi hicho pia ni miongoni mwa vipindi vinavyoiingizia fedha nyingi redio hiyo na kumfanya Millard kuwa miongoni mwa watangazaji wa kituo hicho wanaolipwa mshahara mkubwa zaidi.

Leo hii Millard ni miongoni mwa watangazaji bora Tanzania na wanaosikilizwa zaidi. Si maarufu tu redioni bali pia ndiye mtangazaji wa Tanzania mwenye mashabiki wengi zaidi kwenye mitandao ya kijamii. Ana zaidi ya followers 75,000 kwenye Twitter huku Facebook akiwa na likes zaidi ya 153,000.

Umaarufu wake kwenye mitandao ya kijamii umemfanya ageuke brand na kuyavutia makampuni makubwa kama CRDB Bank, Fast Jet na mengine kudhamini kile anachotweet. Tweets zake tu zinamuingizia fedha huku akimiliki pia website yake binafsi yenye wasomaji lukuki na yenye matangazo mengi.

Kwa mshahara anaoupata, kazi ya uripota wa DSTV, ubalozi wa Fastjet, website yake, deal za voice-overs na mambo mengine, Millard anaingiza takriban ama zaidi ya shilingi milioni 10 kila mwezi.

Millard ni zaidi ya mtangazaji, bali ni mwandishi mwenye ‘pua ya habari’ (nose for news) huku akiongoza kwa kuja na angle za kipekee za habari zenye mvuto kwa watu (human interest stories) zinazokifanya kipindi chake cha Amplifaya kuteka matangazo ya jioni siku za wiki.

Pamoja na kupata mafanikio hayo, Millard ameendelea kuwa mchapakazi, simple, mtu anayejituma kutafuta habari hata sehemu za mbali kabisa, mcheshi na mtu wa watu. Hakuna shaka kuwa, Millard ana mustakabali wa nguvu kwenye fani hiyo. Ni mfano wa kuigwa kwa watangazaji wengine na hazina kubwa kwa wazazi wake, Clouds Media Group na hata taifa kwa ujumla.

2. Hamis Mandi aka B12 – XXL Clouds FM

B12

Kwa muda mrefu, XXL kimeendelea kuwa kipindi namba 1 cha burudani nchini. Kama wimbo wa msanii usipochezwa kwenye XXL, basi wimbo huo una kasoro. Yeye mwenyewe B-Dozen anajiita mfalme wa vipindi vya mchana na hakuna msanii yeyote mkubwa wa Bongo ambaye hajawahi kuhojiwa na mtangazaji huyu mahiri. Kwangu mimi, B-Dozen ndio roho ya XXL ambaye kama asipokuwepo, hakuna mtangazaji anayeweza kukipa kipindi hicho ladha iliyozoeleka. Ndicho kipindi ambacho nyimbo kali za wasanii zimezinduliwa exclusively mwaka 2013. Mwaka huu B12 alitajwa kwenye orodha ya Top Ten Most ya Channel O ya watangazaji bora wa Afrika huku yeye akikamata nafasi ya 9.

3. Raheem Da Prince – The Switch, Times FM

Raheem

Utangazaji wa Raheem na uelewa wake wa muziki, hunifanya nivutike sana kusikiliza kipindi chake cha The Switch kila Jumamosi. Japokuwa Madj wa show hiyo DJ D-Ommy na DJ KU ni sehemu ya kivutio cha show hiyo, ufuatiliaji wa Raheem kuhusiana na muziki wa Marekani na kwingine, hunifanya nitoke na elimu kubwa kila nisikilizapo show yake.

Amekuwa akijituma sana kuchambua matukio ya muziki yakiwemo kuchambua album za wasanii wa Marekani na mambo mengine. Mwaka huu nilifurahia zaidi uchambuzi alioufanya kwa kushirikiana na Reuben Ndege aka Nchakalih, Hermy B na Miss East Africa 2012, Jocelyne Maro wa album ya Jay Z, Magna Carta Holy Grail. Sijawahi kusikia uchambuzi mkali wa muziki kama huo kwenye redio yoyoye ya Tanzania kwa miaka mingi.

4. Vanessa Mdee – The Hitlist, Choice FM

308042_481355628565126_1797969664_n

Vanessa Mdee hutangaza kipindi cha The Hitlist cha Choice FM na ndio sehemu yangu iliyosalia ya kusikiliza nyimbo mpya za Marekani ambazo kwa sasa ni nadra kuzikisia kwingine. Awali show niliyokuwa nikiitegemea kwa kusikiliza selection nzuri ya nyimbo mpya za Marekani ilikuwa ni kwenye The Cruise ya Choice FM kipindi ambacho Steve Kabuye alikuwa anatangaza bado. Napenda uchangamfu wa Vee Money kwenye show yake na uelewa mzuri wa ngoma za nje.

5. Jabir Saleh – The Jump Off, Times FM

Jabir

Namchukulia Jabir Saleh aka Kuvikacha kama maktaba ya muziki wa vijana. Nadiriki kusema ni watangazaji wachache sana Tanzania wenye uelewa wa muziki wa Hip Hop kama alionao Jabir. Ukisikiliza kipindi cha The Jump Off, hakuna shaka kuwa elimu yako kuhusu Hip Hop itapanuka zaidi na kamwe huwezi kujuta kumsikiliza.

6. Sam Misago – Power Jams , EA Radio

944577_346691582123045_1523449421_n

Power Jams na XXL ndivyo vipindi vyenye ushindani zaidi kwa siku nyingi katika vipindi vya mchana. Akiwa amejipa jina ‘The Presenter’s President, Sam ni miongoni mwa watangazaji wenye mashabiki wengi mchana.

7. Bizzo – Show Time; New Chapter , RFA

1239763_570266786344526_1898720372_n

Umaarufu wa Bizzo ulianzia Ebony FM, Iringa ambako alikuwa akifanya show iitwayo The Splash. Kwa sasa Bizzo ambaye jina lake halisi ni Renatus Kiluvya, ni mtangazaji wa kipindi cha Show Time cha Radio Free Africa. Kwa kiasi kikubwa amejitahidi kuliziba pengo la Kidbwoy aliyekuwa amezoeleka sana kwenye kipindi hicho.

8. Perfect Crispin – Club 10, Clouds FM

perfect

Perfect ni mtangazaji wa kipindi cha vijana hususan wa sekondari cha Club 10. Ni kipindi maarufu zaidi kwa wanafunzi wa sekondari kuliko vyote nchini na kwa kiasi kikubwa ameendelea kukimudu na kukiendesha kwa ustadi mkubwa mwaka 2013.

9. Jimmy Jamal – Daladala Beat, Magic FM

1236110_708050345876973_748240325_n

Dala Dala Beat ni miongoni mwa show kongwe kabisa za burudani nchini. Jimmy ni mtangazaji mwenye sauti nzito na mwenye uelewa mkubwa wa muziki wa ndani na nje. Napenda namna anavyofanya interview zake na uchangamfu hewani.

10. King David

King Davidy

Kwa wengi, King David ni jina geni kabisa. Lakini kitu kimoja cha uhakika kuhusu jamaa huyu ni kwamba ukimsikiliza lazima utamkubali na kama angekuwa anatangaza redio kubwa, kwa sasa angekuwa akicheza ligi moja na watangazaji wengi hao juu. Ana sauti nzuri na yenye mamlaka, anajua muziki wa ndani na nje na ni mbunifu. Alikuwa mtangazaji wa Uplands FM ya Njombe ambako alikuwa akifanya vipindi kama Bonge la Drive na Uplands FM Top 20 na kwa sasa amehamia kwenye kituo cha redio kipya kiitwacho Kings FM cha Njombe kitakachoanza rasmi matangazo mwakani.

Related Articles

Back to top button
Close
Bongo5

FREE
VIEW