Bongo Movie

Mapadre nchini waipiga ‘stop’ filamu ya Ray ‘Sister Marry’ isiingie sokoni

IMG_6885

Staa wa filamu nchini Vincent Kigosi aka Ray, amejikuta katika wakati mgumu baada ya mapadre wa kanisa katoliki nchini kutaka kuzuiwa kuingia sokoni kwa filamu yake ya ‘Sister Marry’.

Jopo la mapadri lilikaa kikao kizito cha saa 5 kilichofanyika Jumanne iliyopita katika Ofisi za Utamaduni jijini Dar es Salaam.

Washiriki wa kikao hicho walikuwa ni pamoja na Ray, Mkurugenzi Mtendaji wa Utamaduni aliyetajwa kwa jina moja la Mwansoke, mapadri wanne na mtu mmoja aliyedaiwa kuwa ni wa kutoka ofisi za usalama wa Taifa.

Kikao hicho kilikuja baada ya hivi karibuni viongozi wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam kumtaka msanii huyo ajieleze kimaandishi ni kwa nini mtawa Sister Marry(Irene Uwoya) alikuwa akifanya matendo ambayo kiuhalisia, Wakatoliki wenyewe huwa hawayafanyi.

Ray akiigiza kama padre
Ray akiigiza kama padre

Kabla Ray hajajieleza kwa maandishi ndipo alipoitwa huko na kukubaliana ana kwa ana na jopo hilo huku mashinikizo kadhaa yakielekezwa kwake. Awali, wajumbe wote wakiwa wamekaa kwenye viti, filamu hiyo yenye saa 3 iliwekwa mwanzo hadi mwisho huku mapadri hao wakiguna kila wakati, hasa wakati Sister Marry akiwa anafanya mambo yake mabaya.

Miongoni mwa waigizaji wa filamu ya Sister Marry
Miongoni mwa waigizaji wa filamu ya Sister Marry

Baada ya kumalizika kwa filamu hiyo Mwansoke alisema vipande vyote vichafu viondolewe na kubakizwa vile ambavyo wajumbe hawakuvigunia.Baada ya bosi huyo kusema hayo, mapadri walikataa na kudai filamu hiyo isiingie mtaani kwakuwa inawadhalilisha wakatoliki.

Watawa
Watawa

Paroko wa Kanisa la Mtakatifu Maximilian Kolbe lililopo Mwenge Kijijini alidai kuwa filamu hiyo ilirekodiwa kwenye kanisa lake na kutaka vipande vyote vya kanisa hilo vitolewe ndipo iingie mtaani, jambo ambalo lilimtoa machozi Ray.

Kwa upande wake Ray anadai ni vigumu kuviondoa vipande vya kanisa hilo kwa sababu asilimia 85 ya filamu nzima imerekodiwa hapo.

“Asilimia 85 ya filamu imerekodiwa Maximilian Kolbe, sasa wanaposema niviondoe ni kuimaliza filamu yote. Filamu ni ya saa 3, ukivitoa vipande vya kanisa si itabaki dakika 5 tu,”alisema Ray.

Waigizaji wengine waliogiza kwenye filamu hiyo ni pamoja na Blandina Chagula na Abdallah Ambua (mtangazaji EATV).

Source: Passion FM

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents