Siasa

Marekani yaiagiza serikali kufanikisha Mwafaka haraka

SIKU tatu zikiwa zimebakia kufanyika kwa Mkutano wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (NEC -CCM), unaotarajiwa kutoa hatima ya Mwafaka kati ya chama hicho na CUF, Marekani imetaka serikali kusimamia upatikanaji wa haraka wa Mwafaka huo.

Na Kizitto Noya

 

 

 

SIKU tatu zikiwa zimebakia kufanyika kwa Mkutano wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (NEC -CCM), unaotarajiwa kutoa hatima ya Mwafaka kati ya chama hicho na CUF, Marekani imetaka serikali kusimamia upatikanaji wa haraka wa Mwafaka huo.

 

 

 

Balozi wa Marekani nchini, Mark Green alisema jana katika mapitio ya miezi sita ya kuwapo wake nchini kama Balozi wa Marekani kuwa, kuchelewa kwa Mwafaka wa kisiasa baina ya vyama hivyo, ni doa kwa serikali ya Rais Kikwete.

 

 

 

“Kukamilika kwa Mwafaka wa Zanzibar ni muhimu kwa Tanzania ambayo ni nchi iliyoweka rekodi ya mafanikio mengi katika kipindi kifupi,” alisema Green na kuongeza:

 

 

 

“Mwafaka ni makubaliano yatakayochochea demokrasia na kutoa uhuru kwa Wazanzibari kuwa na sauti katika serikali ya Muungano na kutoa dira ya umoja wa Watanzania.”

 

 

 

Alisema ni wazi kwamba, Tanzania bado inakabiliwa na changamoto nyingi, lakini kubwa ni ya kupatikana kwa Mwafaka.

 

 

 

Balozi huyo alisema ni katika kutambua umuhimu huo wa Mwafaka, Marekani ilimuunga mkono Rais Kikwete alipotangaza kuwa Mwafaka wa kisiasa visiwani Zanzibar ni moja vipaumbele katika uongozi wake.

 

 

 

Kwa mujibu wa Green, Marekani imeunga mkono kipaumbele hicho baada ya kutambua kuwa kupatikana kwa Mwafaka huo kutawaunganisha Watanzania katika vita dhidi ya ufisadi na kujenga mazingira ya uwazi katika utendaji wa serikali.

 

 

 

Alitaja changamoto zingine katika serikali ya Rais Kikwete kuwa ni vita dhidi ya ukimwi na malaria na kusema kuwa bado kuna safari ndefu kufikia maono ya rais ya kuwa na Tanzania bila ugonjwa wa ukimwi.

 

 

 

“Hata kama changamoto hizi ni kubwa bado nina imani kwamba Tanzania inaweza kuzimaliza kwani watu bado wana imani na maono ya Mwalimu Nyerere ya kuwa na nchi ya amani na utulivu na bado wana ari ya kudumisha maono hayo,” alisema Green.

 

 

 

Balozi Green ambaye alitumia maelezo mengi kuisifia serikali katika mafanikio ya kupambana na mafisadi kwa kuwachukulia hatua za haraka wahusika, alisema changamoto nyingine inayoikabili Tanzania ni kuhakikisha uchumi wake unakua kwa uwiano sawa mijini na vijijini.

 

 

 

“Wakati uchumi wa nchi ukionyesha ishara ya kukua kwa kasi, sote tunatambua kuwa bado kunahitajika mambo mengi ya kufanya ili kasi ya kukua kwa uchumi ionekane nchi nzima,” alisema.

 

 

 

Alisema kwa upande mwingine serikali inapaswa kuunga mkono jitihada za Marekani katika kusisitiza uwazi kwenye matumizi ya rasilimali za umma kwa kudhibiti matumizi mabaya ya rasilimali hizo.

 

 

 

Alibainisha kuwa mpango wa Marekani kufadhili mfumo wa ukaguzi wa mahesabu katika Halmashauri zote nchini una lengo lile lile la kudhibiti matumizi mabaya ya rasilimali hizo kwa faida ya umma wa Watanzania.

 

 

 

Taarifa ya Green imekuja huku CCM ikiwa inajiandaa kutoa tamko makubaliano yaliyofikiwa na kamati ya Mwafaka katika kikao chake kinachofanyika Machi 29 hadi 30 mwaka huu.

 

 

 

Hivi karibuni, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho, John Chiligati alikaririwa na akisema kwamba moja ya ajenda za mkutano huo ni kutoa tamko la chama kuhusu yaliyofikiwa katika suala la Mwafaka wa kisiasa Zanzibar.

 

 

 

Source: Mwananchi

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents