Habari

Marekani yalivalia njuga suala la kupotea mwandishi Khashoggi,yaiomba Uturuki kutoa kanda za ushahidi

Trump amewaambia waandishi akiwa White House kuwa "Tumeomba kupewa nakala kanda hiyo, kama ni kweli ipo

Marekani imeomba Uturuki kutoa ushahidi wa kanda ya sauti inayodai kuwa mwanahabari wa Saudi Arabia Jamal Khashoggi aliuawa ndani ya ubalozi wa Saudi Arabia mjini Istanbul. Rais Trump amewaambia waandishi katika ikulu ya White House kuwa, “Tumeomba kupewa nakala kanda hiyo, kama ni kweli ipo,”.

Mtoto mdogo akishikilia picha ya mwanahabari wa Saudi Arabia Jamal Khashoggi

Bwana Khashoggi hajawahi kuonekana tangu alipoingia jengo la ubalozi wa Saudi Arabia tarehe mbili mwezi huu wa Oktoba.  Saudi Arabia amekanusha madai yakuhusika na kutoweka kwa mwandishi huyo.

Huku hayo yakijiri, Gazeti la Washington Post limechapisha makala ya mwisho yaliyoandikwa na bwana Khashoggi kabla ya kutoweka kwake. Katika makala hayo anazungumzia umuhimu wa uhuru wa vyombo vya habari katika eneo la Mashariki ya kati.

Mhariri wa kimataifa wa gazeti hilo Karen Attiah amesema uchapishaji wa makala hayo ulisitishwa kwa ajili ya kuwa na matumaini kwamba bwana Khashoggi atarejea salama. Aliandika akisema “Sasa sina budi kukubali: Kwamba hilo halitafanyika. Hii ndio makala yake ya mwisho nitakayosahihisha”.

Upekuzi unaendelea katika jengo la ubalozi wa Saudi Arabia mjini Istanbul

Bi Attiah pia aliongezea kusema, “Makala haya yanaangazia kwa kina kujitolea kwake kupigania uhuru katika mataifa. Uhuru ambao alipigania kwa maisha yake.”

Kuwepo kwa ushahidi kwamba bwana Khashoggi – mkosoaji mkuu wa viongozi wa Saudi – aliuawa kulifichuliwa na wachunguzi wa Uturuki. Ripoti katika vyombo vya habari vya taifa hilo zinaelezea taarifa za kutisha za dakika za mwisho za mwandishi huyo. Gazeti moja la Uturuki linasema sauti ya balozi wa Saudi Arabia mwenyewe Mohammed al Otaibi inasikika katika kanda hiyo iliyonasa kifo cha bwana Khashoggi.

Yeni Safak, ambayo ina uhusianaop wa karibu na serikali imemnukuu balozi huyo akidai kuwa Saudia ilituma maajenti mjini Istanbul: “Msiseme hili. Mtanitia mashakani.”

Polisi ndani ya makaazi ya balozi wa Saudi Arabia mji Istanbul

Bwana Otaibi alirejea mjini Riyadh siku ya Jumanne.

Saudi Arabia ni moja ya washirika wa karibu wa Washington na kupotea kwa Khashoggi kumeiweka utawala huo katika hali ya kutatanisha. Akigusia sauti iliyorekodiwa na ambayo inadaiwa kuwa na ushahidi wa mauaji ya Khashoggi ,Trump aliongeza: “Sina uhakika ya kuwepo kwa sauti hiyo, lakini huenda ikawa ni kweli ipo.”

Bwana Trump amesema anatarajia ripoti kutoka kwa waziri wa wake wa mambo ya nje Mike Pompeo ambaye alikua nchini Saudi Arabia na Uturuki. Rais Trump amesema ukweli kuhusiana na suala hilo utajulikana “Kufikia mwisho wa wiki”.  Amekanusha madai kwamba anajaribu kusaidia Saudi Arabia kutakasa jina lake: “Hapana, hilo haliwezekani, Kile ninachofanya ni kufahamu kile kinachoendelea.”

Katika kipindi cha siku chache zilizopita Trump amegusia uwezekano wa “Wauaji katili” kuhusika na kutoweka kwa mwandishi Jamal Khashoggi. Pia aliwaomba watu kutokimbia kuwalaumu viongozi wa Saudia kabla ya kuthibitisha kuhusika kwa viongozi hao katika kisa hiki.

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Mike Pompeo(kushoto) alikutana na raisi wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan(kulia) mjini Ankara.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters, siku ya Jumatano na Alhamisi, kundi la maafisa wa wachungizi wa Uturuki walipekua makaazi ya balozi wa Saudi Arabia mjini Istanbul kwa karibu saa tisa na baadae kuelekea katika jengo la ubalozi lililopo mita 200 kutoka makaazi hayo.

Kundi hilo la wachunguzi lilihusisha viongozi wa mashtaka pamoja na watalamu wa upasuaji waliokuwa wamevalia mavazi meupe. Magari kadhaa ya Saudia yaliyo na nambari ya usajili ya kidiplomasia yalinaswa katika picha ya CCTV yakiingia makaazi ya balozi chini ya saa mbili baada ya bwana Khashoggi kuingia ubalozi huo siku alipotoweka.

Ubalozi huo ulipekuliwa kwa mara ya kwanza siku ya Jumatatu. Siku ya Jumanne waziri wa mambo ya nje wa Marekani alisafiri mjini Riyadh kufanya mazungumzo na mfalme Salman wa Saudi Arabia na mwanamfalme Mohammed bin Salman, ambaye amekanusha vikali kuhusika kwake na kotoweka kwa mwanahabari Jamal Khashoggi.

Chanzo BBC

By Ally Juma.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents