Siasa

Marekani yawaonya wanaovuruga muafaka

SUALA la muafaka wa kisiasa visiwani Zanzibar ambao upo katika hali ya kulegalega, limechukua sura mpya baada ya Balozi wa Marekani Tanzania kuonya watu wanaotaka kuuvuruga.

Na Andrew Msechu


SUALA la muafaka wa kisiasa visiwani Zanzibar ambao upo katika hali ya kulegalega, limechukua sura mpya baada ya Balozi wa Marekani Tanzania kuonya watu wanaotaka kuuvuruga.


Akizungumza mara baada ya mkutano wake na waandishi wa habari katika ubalozi huo, balozi huyo, Michael Ratzer, alisema ni vema Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Wananchi (CUF) vikafikia makubaliano katika mazungumzo hayo yaliyodumu kwa miezi minane sasa.


Alisema ni muhimu maridhiano baina ya pande mbili hizo yakafikiwa haraka kabla hali kisiwani humo haijawa mbaya na akasisitiza kuwa kuna umuhimu wa kuunda serikali ya mseto ili kumaliza mizozo ya kisiasa visiwani humo.


Hatua hiyo imekuja huku kukiwa na utata baina ya pande mbili zinazoshiriki mazungumzo hayo, CUF na CCM, ambapo wakati CUF wamekuwa wakilalamikia mizengwe na kuibuliwa kwa madai mapya nje ya mazungumzo ya vyama hivyo, CCM wamekuwa wakidai kuwa CUF ndiyo wanaogomea kuendelea na mazungumzo hayo.


Hata hivyo, mwanzoni mwa wiki hii CUF walitoa msimamo wao wa kutoendelea na mazungumzo hayo na kuomba msaada wa jumuiya ya kimataifa kuingilia ili kuhakikisha hali ya kisiasa inatengemaa visiwani Zanzibar.


CUF wanadai kuwa pamoja na jitihada zao za kumwandikia Rais Jakaya Kikwete, kutaka aingilie kati mvurugano uliojitokeza katika mazungumzo, Rais amekaa kimya, jambo ambalo wamelitafsiri kuwa ameukataa wito wao.


CUF wanasema itakapofika Agosti 15, mazungumzo hayo yatakuwa yamekufa rasmi na kwamba viongozi watatoa mlolongo wa mazungumzo hayo na viongozi wa CCM tangu yalipoanza Januari mwaka huu.


Awali akiwakaribisha wanafunzi waliokuja kujitolea kwa ajili ya kusaidia kutoa huduma za jamii na kujifunza hali ilivyo katika maeneo ya Karagwe na Pemba, Balozi Retzer, alisema ingawa Tanzania imekuwa na historia ya kuwa kisiwa cha amani, bado imekuwa ikikutana na matukio ya uvunjaji amani, ikiwamo matukio ya kisiasa.


“Kwa sasa tatizo linaloonekana kuwepo ni suala zima la kisiasa Zanzibar, tatizo hili bado halijapatiwa ufumbuzi, lakini tuna matumaini kuwa serikali ya CCM na uongozi wa Chama cha CUF watafikia makubaliano kupitia mpango unaoendelea kabla ya tarehe ya mwisho waliyojiwekea, ambayo ni Agosti 15,” alisema Retzer.


Akitoa ufafanuzi juu ya njia nzuri inayoweza kutumiwa kumaliza matatizo hayo mara baada ya mkutano huo, Balozi Retzer alisema kutokana na hali halisi ya matokeo ya uchaguzi ambao umekuwa ukivigonganisha vyama hivyo viwili, ni jambo zuri iwapo utakuwepo uwezekano wa serikali ya mseto, ikiwa ni njia muhimu kumaliza matatizo yaliyopo.


“Unapokuwa na uchaguzi ambao unavigawanya vyama viwili kwa uwiano unaokaribiana wa uwakilishi, ni vyema kuhakikisha kuwa watu wote wanapata nafasi ya uwakilishi serikalini, suala la serikali ya mseto inayounganisha pande hizo ni muhimu, hii inaonyesha umoja wa kitaifa,” alisema.


Aliongeza kuwa ni vizuri inapofikia hatua kama hiyo kuungana kwa ajili ya maslahi ya wananchi wa maeneo mawili yenye uwakilishi kwa serikali kuhusisha na kuingiza watu wa upinzani.


Alitoa mfano wa namna ambavyo vyama viwili vya kisiasa nchini Marekani vyama vya Republican na Democrat, ambavyo mara kadhaa vimekuwa vikijikuta vikigawana matokeo kwa asilimia zinazokaribiana hivyo kwa kujali maslahi ya wananchi hulazimika kuwa na serikali ya umoja wa kitaifa.


Alisema ni vema kuangalia uwezekano huo wa kuungana na kujumuisha uwakilishi wa sehemu hizo mbili zenye mgongano ili kulinda maslahi ya wananchi waliopiga kura bila kujali itikadi.


Hata hivyo alisisitiza kuwa anaamini kuwa pande hizo mbili zitamaliza tofauti zilizojitokeza na kufikia maelewano mapema.


Wanafunzi hao 26 waliokaribishwa na balozi huyo nchini jana wanatarajiwa kufanya kazi za kujitolea katika maeneo ya Pemba na Karagwe kwa ushirikiano na wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.


Marekani ni nchi pekee duniani ambayo ilikataa kuyatambua matokeo ya uchaguzi kisiwani Zanzibar mwaka 2005, ikisema kulikuwa na ukiukwaji mkubwa wa taratibu za uchaguzi.


Hata hivyo, mazungumzo ya kutafuta muafaka baina ya vyama hivyo viwili yaliyoanza Januari mwaka huu, yalilegeza msimamo wa nchi hiyo dhidi ya uchaguzi wa Zanzibar kiasi kwamba Rais George Bush, alimkaribisha kwa mazungumzo Rais Jakaya Kikwete jijini New York mapema mwaka huu.


Source: Mwananchi

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents