Habari

Marufuku kusafirisha chakula nje ya nchi – Waziri Mkuu

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amepiga marufuku usafirishaji wa chakula kwenda nje ya nchi bila ya vibali.

Waziri Mkuu ametoa agizo hilo Jumatatu hii, wakati akitoa nasaha kwenye Baraza la Eid lililofanyika kitaifa kwenye msikiti wa Masjid Riadha, mjini Moshi, mkoani Kilimanjaro mara baada ya kuswali sala ya Eid.

“Kuanzia leo, ni marufuku kwa mtu yoyote kusafirisha mazao ya chakula kwenda nje ya nchi bila ya vibali. Serikali inahamasisha uwekezaji kwenye ujenzi wa viwanda nchini. Kama tutatoa vibali, ni lazima mtu alazimike kusaga nafaka ili kutoa ajira nchini,” alisema.

“Mimi nasema kuanzia leo(jana), yeyote atakayekamatwa akitorosha chakula kwenda nje ya nchi, chakula hicho kitataifishwa na kupelekwa ghala la Taifa na gari lake tutalitaifisha na litaishia Jeshi la Polisi. Tunafanya hayo kwa lengo la kuwalinda Watanzania tusikumbwe na baa la njaa.”

Akitoa tahadhari kuhusu uuzwaji wa chakula nje ya nchi, Waziri Mkuu amesema kumekuwa na wimbi kubwa la usafirishaji wa chakula kwenda nje ya nchi bila kibali. “Hilo ni kosa kubwa kwa sababu litasababisha nchi yetu kupata baa la njaa huko mbele,” amesema.

Sherehe hizo zilihudhuriwa na Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania, Sheikh Abubakar Zubeir bin Ally; Wajumbe wa Baraza la Ulamaa, Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Mama Anna Mghwira, IGP Mstaafu, Bw. Said Mwema, Mbunge wa Moshi Mjini, Bw. Jaffary Michael, Wakuu wa Wilaya za Mkoa huo na viongozi mbalimbali wa dini na Serikali.

Na Emmy Mwaipopo

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents