Siasa

‘Mashangingi si magari ya kifahari’

SERIKALI imewashangaa watu wanaoyaita magari aina ya Toyota Land Cruiser VX, maarufu kama mashangingi, ambayo hutumiwa na viongozi wa serikali kuwa ni magari ya kifahari.

na Mwandishi Wa Tanzania Daima, Dodoma


SERIKALI imewashangaa watu wanaoyaita magari aina ya Toyota Land Cruiser VX, maarufu kama mashangingi, ambayo hutumiwa na viongozi wa serikali kuwa ni magari ya kifahari.


Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais (Utawala Bora), Philip Marmo, alisema kuwa magari hayo hayastahili kuitwa ya kifahari kwani ni magari ya kazi.


Alitoa msimamo huo jana wakati akijibu baadhi ya hoja zilizotolewa na wabunge kuhusiana na hotuba ya bajeti ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, iliyowasilishwa juzi jioni na Waziri mwenye dhamana hiyo, Hawa Ghasia.


“Suala hili linafanyiwa kazi lakini hayo magari ya kifahari ni yepi? Huwezi kusafiri kutoka Dar hadi Kibondo au Mpanda kwa kutumia saloon. Haya yanachukuliwa kama magari ya kazi,” alisema.


Kauli yake hiyo ilitokana na hoja iliyotolewa na Waziri Kivuli katika eneo hilo, Shoka Khamis Juma (Micheweni-CUF), ambaye katika hotuba yake alibainisha kuwa magari hayo yanaongeza matumizi ya serikali bila sababu za msingi kama ilivyowahi kusemwa na muungano wa vyama vya wafanyakazi (TUCTA).


Ili kubainisha hilo, Juma alinukuu sehemu ya hotuba iliyosomwa na Katibu Mkuu wa Tucta, Nestory Ngula, wakati wa maadhimisho ya Sikukuu ya Mei Mosi, Mwanza.


Alisema matumizi ya magari hayo ni gharama kubwa kuyatunza, hakulingani na hali ya uchumi wa nchi.


“Takwimu kutoka Wizara ya Miundombinu zinaonyesha kwamba hadi kufikia mwishoni mwa mwaka wa fedha wa 2005/06 jumla ya magari makubwa na ya kifahari yapatayo 6,000 yalikuwa yamenunuliwa na serikali kwa gharama kubwa inayokadiriwa kufikia sh bilioni 160,” alisema Juma.


Alisema kuwa miongoni mwa magari yaliyonunuliwa, ni Toyota Land Cruiser (VX/GX, STD, Prado) yapatayo 1,655, Nissan patrol na Land Cruiser 885, Mitsubishi Pajero 400 na mengineyo.


“Serikali ingekuwa inafanya matumizi yake kulingana na hali ya uchumi kama inavyofanya kwa wafanyakazi kwa kuwalipa mishahara isiyotosheleza mahitaji muhimu ya maisha,” alisema.


Kuhusiana na mishahara, Juma alionyesha masikitiko yake kwa serikali kushindwa kutamka moja kwa moja kiasi cha nyongeza ya mshahara, hata ule wa kima cha chini.


“Tofauti na matarajio ya wengi, hususan wale walipwao kima cha chini, hali imeendelea kuwa ngumu kutokana na kutopanda kwa mshahara kwa kiwango kinachoridhisha. Bajeti kuu ya serikali ya mwaka 2007/08 inaonyesha kwamba mshahara utaongezeka kwa asilimia 12. Hili ni ongezeko dogo sana,” alisema.


Alibainisha kuwa maboresha ya masilahi ya watumishi ni jukumu muhimu kwa menejimenti na ndiyo maana serikali iliahidi maisha bora kwa kila Mtanzania.


Alisema inashangaza kuwa wakati katika risala yao kwa Rais Kikwete wakati wa maadhimisho ya Mei Mosi wafanyakazi waliomba nyongeza ifikie sh 350,000, nyongeza iliyotangazwa na serikali haifikii hata robo ya kiwango kilichopendekezwa.


“Kambi ya upinzani inatambua kwamba kutokana na hali ya uchumi, ongezeko hili kwa ghafla lisingeweza kufikiwa. Pamoja na hayo, bado tunaamini ya kwamba kama serikali ingepokea ushauri wa kuboresha bajeti uliotolewa na kambi ya upinzani, ongezeko hilo lingeweza kufikiwa angalau nusu,” alisema.


Juma aliwatetea pia watumishi wasiokuwa wa sekta ya umma na kuitaka serikali kupanga pia kima cha chini cha mishahara ya watumishi katika sekta binafsi.


Alisema kuwa kiwango cha sasa kwa watumishi wa sekta hiyo cha kati ya sh 35,000 na sh 48,000 kinatosheleza mahitaji kwa muda wa wiki moja tu.


Naye Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala, Tatu Ntimizi (Igalula-CCM), alisema kuwa licha ya maboresho yanayofanyika katika sekta ya utumishi wa umma, bado zipo ofisi nyingi za serikali ambazo baadhi ya watumishi wake hufanya kazi kwa mazoea bila kuzingatia maadili na masharti ya kazi zao.


“Mbali ya serikali kuwahimiza na kuwakumbusha watumishi juu ya utendaji bora wa kazi kupitia nyaraka, semina na vikao mbalimbali, bado kuna baadhi ya watumishi wanaofika kazini muda wanaotaka na kutoka katika vituo vyao vya kazi kushughulikia masuala yao binafsi huku viongozi wao wakiwatazama,” alisema.


Aidha, aliitaka serikali kuhakikisha kuwa viongozi wenye dhamana ya kujaza fomu za kutoa tamko la mali na madeni yao na kuwasilisha Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, wanafanya hivyo mapema kwa mujibu wa sheria na kwa wakati uliowekwa.


Bunge lilitarajiwa kupitisha bajeti hiyo jana jioni baada ya kujadiliwa kwa siku moja.


Source: Tanzania Daima

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents