Burudani

Mashindano ya Bongo Star Search yaja kivingine, Madam Rita atoa ombi kwa serikali

Serikali imeshauriwa kuangalia kwa jicho la tatu sanaa ya muziki kwa kuwa inaweza kutoa ajira kwa vijana wengi.

Hayo yameelezwa leo Septemba 11 na Mkurugenzi wa kampuni ya Benchmark inayoandaa mashindano ya kusaka vipaji ya muziki, Bongo Star Search (BSS) Rita Paulsen.

Rita ameyasema hayo leo wakati wa uzinduzi wa msimu wa tisa wa BSS unaotarajiwa kuanza kutimua vumbi Septemba 22 mkoani Mwanza.

Amesema muziki ni kiwanda ambacho kikiimarishwa vyema kinaweza kuwa na matokeo chanya ndani ya jamii.

” Tunachokifanya sisi ni kutoa jukwaa kinachofuata hapo msanii anatakiwa kujiongeza na kupata msaada wa wadau wengine ikiwemo serikali ili kumuwezesha kufanya muziki ajira yake,”

“Tunaomba Serikali iangalie vizuri kuhusu muziki wapo vijana wengi hawana ajira lakini wanapenda muziki tukiungana tunaweza kuwasaidia,”

Katika msimu huu BSS imeingia ubia na StarTimes inayomilikiwa na Kampuni ya Star na mashindano hayo yataruka kupitia channel ya ST Swahili.

Meneja Masoko StarTimes, David Malisa amesema kampuni hiyo inajua umuhimu na ukubwa wa mashindano ya BSS.

Amesema lengo la kurusha mashindano hayo ni kutaka kutoa burudani yenye maudhui bora kwa kila mwanafamilia.

“Tunafahamu ukubwa wa BSS ndio maana tumeamua tuonyeshe kwenye channel yetu ya Kiswahili,

“Tunataka kuonyesha vitu ambavyo kila mtu atafurahia kuona burudani ambayo maudhui yake sio ya kuudhi wala kukera,”

Amesema kuanzia sasa mteja wa StarTimes atakapofanya malipo ya king’amuzi moja kwa moja atapata nafasi ya kuingia kwenye usahili wa BSS bila kupanga foleni.

Usahili wa BSS utaanza Septemba 22 na 23 mkoani Mwanza kisha Septemba 29 na 30 mkoani Arusha.

Kwa wakazi wa Mbeya usahili utakuwa Oktoba 6 na 7 huku Dar es Salaam ukifanyika Oktoba 12, 13 na 14.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents