Habari

Mataifa makubwa yaitenga Marekani kwa kuirejeshea vikwazo Iran

Muda mchache baada ya Marekani kutangaza kurejesha vikwazo vya Umoja wa Mataifa dhidi ya Iran, washirika wake muhimu duniani – Ufaransa, Uingereza na Ujerumani – wamejitenga nayo, wakisema haina uhalali huo.

USA | Außenminister Mike Pompeo (AFP/M. Segar)

Mataifa hayo kwenye migogoro mbali ya kidunia yamekuwa yakisimama nyuma ya Marekani, yametowa msimamo wa pamoja siku ya Jumapili (Septemba 20) yakisema kuwa uamuzi huo wa Marekani hauna nguvu za kisheria.

Kauli kama hiyo ilitolewa pia na Urusi, hasimu mkubwa wa Marekani. “Hatua na vitendo vilivyo kinyume na sheria vya Marekani kimsingi haviwezi kuwa na athari ya kisheria kwa nchi nyengine,” ilisema taarifa ya mambo ya nje ya Urusi.

Kwa upande wake, Iran ilisema kuwa Marekani inakabiliwa na kushindwa kwenye hatua yake hiyo. Rais Hassan Rouhani alisema kupitia hotuba iliyorushwa kwenye televisheni siku ya Jumapili (Septemba 20) kwamba nchi yake kamwe haitopiga goti mbele ya Marekani na kwamba itaijibu Marekani kama inavyostahiki.

Awali msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Iran, Saeed Khatibzadeh, alisema Marekani, imetengwa na ulimwengu baada ya kutangaza uamuzi wa peke yake kurejesha vikwazo vya Umoja wa Mataifa dhidi ya taifa hilo la Kiislamu, ambavyo vimekataliwa na mataifa mengine makubwa ya dunia.

Khatibzadeh alisema kuwa Marekani imekosa mshirika hata mmoja wa kumuunga mkono, na hivyo “imetengwa kabisa kwenye madai yake. Dunia nzima inasema hakuna kilichobadilika.”

Marekani yatishia kuwaandama watakaokaidi vikwazo

Iranian Präsident Hassan Rouhani PK (picture-alliance/dpa/Iranian Presidency)Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Siku ya Jumamosi (Septemba 19), serikali ya Marekani ilitangaza kuwa kipengele kinachoitwa “kurejesha” vikwazo” kimeanza kazi na kutishia kuikabili nchi yoyote mwanachama wa Umoja wa Mataifa ambayo ingelishindwa kukiheshimu.

Vikwazo hivyo viliondolewa mwaka 2015 baada ya Iran na mataifa mengine sita duniani – Uingereza, China, Ufaransa, Ujerumani, Urusi na Marekani yenyewe – kufikia makubaliano ya kihistoria yaliyofahamika kama Mpango Mkakati wa Pamoja.

Lakini Rais Donald Trump aliitowa Marekani kwenye makubaliano hayo mwaka 2018, akisema mkataba uliosainiwa na mtangulizi wake Barack Obama ulikuwa hautoshi. Badala yake akatangaza vikwazo vipya na kuongezea makali vilivyokwishakuwepo.

Licha ya kujitowa kwenye makubaliano, Marekani inasisitiza kwamba bado ni mshiriki wake, lakini ilifanya hivyo kwa makusudi tu ya kutumia fursa ya kipengele cha kurejesha vikwazo iliyoitangaza mnamo Agosti 20.

Trump ajikuta peke yake

USA Coronavirus | PK Trump (picture-alliance/Photoshot/Liu Jie)Rais Donald Trump wa Marekani.

Hata hivyo, wanachama wengine wote waliobakia wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wanakataa ikiwa Marekani inao uhalali wa kisheria kuchukuwa hatua hiyo, na tangu hapo chombo hicho cha juu cha Umoja wa Mataifa hakijafanya uamuzi mwengine wowote.

Iran ilisema kwa uamuzi wake huo, Marekani inaifanya dunia ione haja ya kuungana pamoja dhidi ya “vitendo vya ovyo” vya Marekani.

“Lote hili ni zogo tupu, na nadhani hizi ni siku mbaya sana kwa Marekani,” alisema Khatibzadeh, akiongeza kwamba ujumbe wa Iran kwa Marekani ni mmoja na wazi. “Rudi kwenye jumuiya ya kimataifa, kwenye ahadi zako, acha uasi na dunia itakupokea.”

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Mike Pompeo, alitangaza hatua hiyo ya nchi yake kwenye taarifa iliyosema kwamba: “Leo, Marekani inakaribisha kurejea kwa vikwazo vyote vya Umoja wa Mataifa dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, ambavyo vilikuwa vimesitishwa,” akitishia nchi yoyote itakayokiuka vikwazo hivyo, ingeliadhibiwa vikali.

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents