Siasa

‘Matumizi bado tatizo serikalini’

MDHIBITI na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, amesema idadi ya matumizi ya fedha yanayotiliwa shaka serikalini, imeongezeka sambamba na kuendelea kukua kwa pato la taifa.

na Martin Malera, Dodoma


MDHIBITI na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, amesema idadi ya matumizi ya fedha yanayotiliwa shaka serikalini, imeongezeka sambamba na kuendelea kukua kwa pato la taifa.



Sambamba na hilo, amesema pia kwamba, fedha zinazotengwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo, zimeendelea kubakia kuwa ni kidogo kuliko zile zinazotengwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida.



Matokeo ya ukaguzi wa fedha za serikali kwa mwaka wa fedha wa 2005/2006, yanaonyesha kwamba, nusu ya wizara, idara na wakala wa serikali, zina hati zinazotiliwa shaka na zisizoridhisha kimahesabu.



Akitoa mfano mbele ya waandishi wa habari mjini hapa jana, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu huyo wa Hesabu za Serikali, Ludovick Utouh alisema, tangu mwaka wa fedha wa 2003/2004, 2004/2005 na 2005/2006 fedha hizo za miradi ya maendeleo hazijawahi kuzidi asilimia 25, wakati zinazotengwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida ni zaidi ya asilimia 75.



Kwa mujibu wa Utouh, katika kipindi cha mwaka wa fedha wa 2004/2005 matumizi ya serikali yaliongezeka kutoka sh 2,138,860,343,786 hadi sh 2,732,455,841,323 wakati mwaka huo wa 2005/2006 fedha za matumizi ya maendeleo zilipungua kutoka 850,353,139,955 mwaka 2004/2005 hadi sh 844,103,204,420 mwaka 2005/2006.



Moja ya mambo yaliyobainika katika ripoti hiyo ni kwamba Wizara ya Usalama wa Raia, hadi Juni mwaka jana ilikuwa inadaiwa sh bilioni 14.1 kwa huduma zilizotolewa na wadai mbalimbali na mpaka sasa madeni hayo hayajalipwa.



Alitaja baadhi ya mambo yaliyochangia kuwa na hati chafu, kwa upande wa Serikali Kuu kuwa ni pamoja na kuwa na madeni yasiyolipwa katika mashirika ya umma, yenye thamani ya sh bilioni 63.2.



“Pia kuna matumizi yasiyokuwa na faida kwa serikali (Nugatory expenditure) ya sh milioni 218.8. Hasara hii inarudiwa kila mwaka bila afisa masurufu kuchukua hatua za kinidhamu,” alisema Utouh.



Kwa upande wa Serikali za Mitaa, alisema mambo yaliyochangia kuwa na hati chafu ni pamoja na kutorejeshwa kwa masurufu yanayofikia sh 800,666,792 katika mamlaka za Serikali za Mitaa 16.



Alisema pia kwamba, mamlaka za serikali za mitaa 46 zilikuwa na matumizi yenye nyaraka ya sh bilioni mbili ambazo zililipwa bila ya hati za malipo.



“Ripoti zinaonyesha dhahiri kwamba, matatizo makubwa bado yapo katika usimamizi na utoaji wa taarifa za fedha katika Serikali Kuu na hasa katika Serikali za Mitaa,” alisema.



Kuhusu hati zinazoridhisha, Utouh alisema katika mwaka wa fedha wa 2005/2006 wizara na idara zinazojitegemea, wakala na sekretarieti 40 kati ya 70 sawa na asilimia 57, zilikaguliwa na kupewa hati zinazoridhisha wakati wakala na sekretarieti za mikoa 27 kati ya 70 sawa na asilimia 39, zilipewa hati zenye shaka.



Kutokana na matokeo ya uchunguzi huo, alisema ametoa taarifa katika mamlaka husika kufanya uchunguzi wa ubadhirifu na matumizi mabaya ya serikali kwa hatua zaidi na kuongeza kwamba, tayari Rais Jakaya Kikwete ameshapata ripoti hiyo na serikali inaifanyia kazi.


Source: Tanzania Daima

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents