Habari

Matumizi ya Ikulu yanatisha – CUF

Chama cha Wananchi (CUF), kimedai kwamba, matumizi ya Ofisi ya Rais yamefikia zaidi ya Sh. bilioni 50, ikiwa ni maradufu ya makadirio ya bajeti yake.

Na Mwandishi Wa Nipashe



Chama cha Wananchi (CUF), kimedai kwamba, matumizi ya Ofisi ya Rais yamefikia zaidi ya Sh. bilioni 50, ikiwa ni maradufu ya makadirio ya bajeti yake.


Mwenyekiti wa chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba, alitoa madai hayo mbele ya waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana.


Profesa Lipumba alifafanua kuwa, makadirio ya ofisi hiyo katika kipindi cha robo mwaka wa fedha 2006/2007, ni Sh. bilioni 23.4 lakini hadi sasa Ofisi ya Ikulu tayari imetumia Sh. bilioni 54.


“Ofisi ya Rais, inaongoza katika ukosefu wa nidhamu wa matumizi ya fedha za serikali. Matumizi katika robo ya kwanza ya mwaka huu wa fedha ambayo hujumuisha bajeti ya Ikulu, fedha za kulipia madeni na Usalama wa Taifa, yalikuwa Sh. bilioni 54 zaidi ya mara mbili ya bajeti yake,“ alidai.


Profesa huyo wa uchumi, alidai kwamba, miongoni mwa sababu zinazochangia hali hiyo, ni safari za nchi za nje za mara kwa mara za Rais.


Aidha, alishauri kwamba, hakuna sababu ya kwenda Amerika au Ulaya na badala yake anaweza kukutana na Mabalozi wa nchi hizo na kuwapata wawekezaji.


“Ukitengeneza umeme ukawa wa kutosha na uhakika zaidi, utapata wawekezaji kuliko kwenda ng�ambo mara kwa mara,“ alisema Profesa Lipumba.


Kwa mujibu wa Profesa Lipumba, safari za Rais za mara kwa mara, zimekuwa zikilalamikiwa hata na baadhi ya watu, lakini yeye husema zinatokana na mialiko ya viongozi wa nchi husika.


Alitoa mfano wa Waziri Mkuu, Bw. Tony Blair kwamba alimwalika Uingereza na kwenda kuwashawishi wawekezaji ili nchi isonge mbele kwa kasi mpya.


Hata hivyo, Profesa Lipumba, hakuanisha matumizi ya Ofisi ya Rais katika awamu nyingine za uongozi uliotangulia kwa kipindi cha robo mwaka.


Alikuwa akitoa madai hayo kwa kukariri taarifa za matumizi ya robo ya kwanza ya mwaka huu wa fedha na kueleza kuwa, robo ya pili haijatolewa.


Kuhusu ugonjwa wa Homa ya Bonde la Ufa (RVF), Profesa Lipumba alisema maradhi hayo yanasambaa na kuligharimu taifa fedha nyingi kwa sababu yanashughulikiwa kisiasa zaidi kuliko kitaalamu.


“ Mwaka 2002, Shirika la Chakula na Kilimo Duniani (WHO), lilitoa maelekezo kwa watalaamu kuandaa mikakati ya kuzuia kuenea RVF.


Walizishauri serikali za maeneo yanayoathirika ikiwemo Tanzania, kuandaa mikakati ya kuzuia maradhi hayo mara yanapozuka,“aliongeza.


Alidai kuwa, ni wazi mkakati haukuandaliwa na Wizara ya Maji na Maendeleo ya Mifugo, kwa wakati ule ikiongozwa na Waziri Mkuu wa sasa, Bw Edward Lowassa.


“Hata mashine za kupima virusi vya mifugo iliyoathirika, zimeingia nchini mwaka huu huku viongozi wakiwachanganya wananchi kwa kutoa kauli za kisiasa,“ alisisitiza.


Kwa mfano, alimkariri Waziri wa Maendeleo ya Mifugo, Bw. Anthony Diallo akiwaeleza wananchi kuwa wasifadhaike kwa kuwa serikali imedhibiti RVF huku ugonjwa huo ukiwa umesambaa na kuua watu wengi hasa mkoani Dodoma.


Profesa Lipumba ambaye alikuwa akichambua hotuba ya Rais aliyoitoa mwisho wa mwezi uliopita, alisema, anashangaa kutolewa chanjo ya RVF kwenye maeneo ambayo ugonjwa umesambaa.


“Cha kushangaza, chanjo inasambazwa kwenye maeneo yenye ugonjwa na kuwachanja wanyama wanaoumwa ambapo ni kuyapa maradhi nguvu mpya, tena unaweza kusababisha yakabadilika na kuwa hatari zaidi,“ alidai Profesa Lipumba.


Aliwashauri wanasiasa wa awamu ya nne, kusikiliza na kutekeleza ushauri wa wataalamu, badala ya kutunga sera kwenye majukwaa.


Kuhusu mikopo ya ujasiriamali, aliilinganisha na fedha za mikopo ya wanawake zilizoitwa “Mikopo ya Nsekela“ zilizopewa jina hilo kwa heshima ya marehemu Amon Nsekela ambazo hadi sasa alidai kwamba hazijarejeshwa.


Alisema awamu ya nne isipokuwa makini fedha hizo hazitarejeshwa na zitaishia mikononi mwa watu wachache.


Aidha, alihoji utekelezaji wa ahadi ya CCM ya kutoa ajira 200,000 kila mwaka.


“Au mikopo ya ujasiriamali ndiyo sasa mbadala wa ajira?“ Alihoji.
Kwa mujibu wa Profesa Lipumba, hadi sasa hakuna ajira zinazotolewa kwenye viwanda wala kwenye makampuni ingawa Ilani ya CCM iliahidi ajira milioni moja katika awamu ya utawala wake, kati ya 2005 na 2010.


Source: Nipashe

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents