Tragedy

Mauaji Dar…polisi wabaki vinywa wazi

Mauaji ya kutatanisha yametokea Jijini Dar es Salaam ambapo mtu mmoja
amekatwa katwa sime mwili mzima hadi kufa wakati mwingine amelambwa
risasi kibao.

Na Sharon Sauwa, Jijini

Mauaji ya kutatanisha yametokea Jijini Dar es Salaam ambapo mtu mmoja amekatwa katwa sime mwili mzima hadi kufa wakati mwingine amelambwa risasi kibao.

Hata hivyo polisi hadi sasa wamebaki vinywa wazi kutokana mazingira ya tukio zima kuzingirwa na utata mtupu.

Kamanda wa mkoa wa kipolisi wa Kinondoni, Jamal Rwambow amesema aliyeuawa ni mlinzi anayejulikana kama Kapteni Komba ambaye analinda grosari iitwayo Iloganzala iliyoko kule Mbezi, Goig, Jijini.

Amesema aliyelambwa risasi ni Nassoro Mussa, 22 ambaye kwa bahati amenusurika kifo lakini akapata majeraha mwilini. Amesema huyo Nassoro ni sungusungu.

Kwa mujibu wa Kamanda Rwambow, tukio hilo limetokea usiku wa kuamkia leo saa 8.30 katika eneo hilo la Mbezi, Goig.

Akielezea tukio zima, Kamanda huyo amesema sungusungu huyo alikwenda katika eneo lake la ulinzi ambalo ni nyumbani kwa Bw. Renatus Paul, 40. akiwa amejeruhiwa kwa risasi huku damu nyingi ikimtoka.

Akasema Bw. Renatus alipiga simu polisi kuomba msaada na walipokuwa wakielekea katika tukio, umbali mfupi kutoka katika grosary ya Ilongazala walimuona Kapteni Komba akiwa hoi.

Akasema baada ya kushuka na kumuangalia, walimkuta yuko hoi na muda si mrefu alikata roho.

Hata hivyo, akasema katika eneo hilo walipomkuta Kapteni Komba hakukuwa na damu, hali ambayo inaashiria tukio hilo halikufanyika eneo hilo.

“Bado tunaendelea kuchunguza mazingira ya kifo na kujeruhiwa kwa watu hao kwa sababu ni tata kidogo,“akasema.

Akasema utata huo unatokana na kutokuwa na taarifa zozote za ujambazi katika eneo hilo na sungusungu kutokuwa na wenzake wakati huo wa lindo.

Amesema majeruhi huyo amelazwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na hali yake inaendelea vizuri.

Kamanda ameomba watu wenye kufahamu kuhusiana na tukio hilo, kuisaidia polisi ili waweze kubaini ukweli tukio hilo.

Source: Alasiri

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents