Tragedy

Mauaji Kenya sasa kama kazi

ZAIDI ya watu 20 wameuawa kwa kuchomwa moto na mashamba ya zao la chai yameharibiwa vibaya katika miji ya Kericho, Sotik na Kisii mkoani Rift Valley, nchini Kenya.

Dismas Lyassa na Mashirika ya Kimataifa

 

 

 

ZAIDI ya watu 20 wameuawa kwa kuchomwa moto na mashamba ya zao la chai yameharibiwa vibaya katika miji ya Kericho, Sotik na Kisii mkoani Rift Valley, nchini Kenya.

 

 

 

f0Kuanzia juzi jioni na usiku wa kuamkia jana katika miji hiyo mitatu (Kericho, Sotik na Kisii) vijana wasiojulikana walivamia nyumba na kuzichoma moto watu wakiwa wamelala.

 

 

 

Ingawa wengine walifanikiwa kukimbia baada ya nyumba zao kuanza kuteketea kwa moto, baadhi ya watoto, wazee, walemavu na wagonjwa ambao hawakuwa na uwezo wa kukimbia waliungua hadi kufa.

 

 

 

Hata hivyo wafanyakazi wa misaada wana wasiwasi kuwa idadi ya waliouawa huenda ni zaidi, kuna wengine huuawa kwa kuviziwa kisha maiti kutupwa porini.

 

 

 

Machafuko hayo ambayo yalianza nchini humo mara baada ya kutangazwa matokeo tata ya kura za urais yamesababisha watu zaidi ya 1,000 kuuawa na zaidi ya 500,000 kuwa wakimbizi pamoja na kuathiri uchumi wa Kenya kwa kiasi kikubwa ambapo thamani ya shilingi yake sasa imeporoka kwa asilimia 15 dhidi ya dola ya Marekani.

 

 

 

Hali kadhalika biashara katika soko la hisa zimeporomoka kwa zaidi ya asilimia 14 katika mwezi Januari pekee, huku baadhi ya wawekezaji wakifikiria kufunga biashara zao kama hali ya usalama itaendelea kuwa tete kama ilivyo sasa.

 

 

 

“Wiki ya kwanza na wiki ya pili baada ya kutokea machafuko hatukuwa na mashaka sana tuliamini mambo yangerudi kawaida, lakini inasikitisha kuona hali hii mbaya inaendelea kwa zaidi ya mwezi sasa,� alilalamika Meneja wa kampuni inayojishughulisha na utoaji wa mikopo ya fedha iitwayo Standard Africa equity, Stephane Bwakira.

 

 

 

“Mauaji yanayoendelea na uharibifu mwingine unaofanyika unaathiri sana uchumi. Kwa sekta ya benki ni wazi tunapata hasara, kutakuwa na ugumu wa kurudishiwa fedha tulizowakopesha watu na hasa wafanyabiashara kutokana na baadhi yao kufunga shughuli zao,� alisema Bwakira.

 

 

 

Hali ya amani inaendelea kuwa mbaya nchini Kenya licha ya Katibu Mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa, Kofi Annan pamoja na timu yake kuwepo nchini humo kwa zaidi ya wiki sasa kwa ajili ya kutafuta njia za kulipatia ufumbuzi tatizo hilo.

 

 

 

“Acha Annan apatanishe, lakini hapatakuwa na suluhu hadi Kibaki aondoke madarakani, hatukumchagua ameingia kwa nguvu Ikulu,” alisikika akisema kijana mmoja mkazi wa Kericho.

 

 

 

Juzi jioni kundi kubwa la vijana likiwa na viberiti, mafuta ya petroli, panga na silaha zingine za jadi, zilivamia eneo la Kericho kwa lengo la kuendesha mauaji, lakini walijikuta wakiangukia kwenye mtego wa polisi.

 

 

 

Hata hivyo, baada ya kushindwa kufanya mauaji, walivamia mashamba ya chai waliyoamini kuwa ni ya jamaa wa Kibaki na kuyaharibu kwa kuyafyeka na kuchoma moto.

 

 

 

Akiwa kwenye mkutano wa viongozi wa Umoja wa Afrika wiki iliyopita, Rais anayedaiwa kuwa hakushinda alisisitiza kuwa hakuiba kura na kusema kama Raila anaona ameibiwa aende mahakamani ili haki itendeke kupitia mkondo wa sheria kwa mujibu wa Katiba ya Kenya.

 

 

 

Naye Raila akijibu kauli hiyo, alisema Kibaki ndiye kikwazo cha harakati za kurejesha amani nchini Kenya, kwa kuwa anaendesha mabishano hayo juu ya nani alishinda katika uchaguzi wa Desemba 27, wakati anajua kuwa alijitangazia ushindi wakati hakushinda.

 

 

 

“Dunia isikubali kudanganywa na Kibaki kuwa eti alishinda kwenye uchaguzi,” alionya Raila.

 

 

 

Vurugu zinazoendelea nchini humu hivi sasa zimefikia kwenye hali ngumu zaidi, ambapo pamoja na watu wengi tayari wabunge wawili wa chama cha ODM wameshauawa katika mazingira ya kutatanisha.

 

 

 

Wabunge hao ni Melitus Were aliyekuwa Mbunge wa Embakassi ambaye aliuawa akiwa nje ya lango la nyumba ndani ya gari lake akisubiri kufunguliwa na Mbunge wa Ainamoi, David Too ambaye aliuawa kwa kupigwa risasi na askari mmoja wa Usalama Barabarani kwa madai kwamba alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na mpenzi wake.

 

 

 

Mwanamke huyo ambaye pia alikuwa askari polisi alikuwa kwenye gari la mbunge siku hiyo ambalo askari huyo alilifukuza kwa muda. Inadaiwa kuwa kabla ya kumuua askari huyo, mwanamke alitoka kwenye gari na kuanza kukimbia akapigwa risasi na hatimaye kufia hospitalini wakati madaktari wanafanya juhudi za kuokoa maisha yake.

 

 

 

Vifo hivyo vilichochea hasira za wananchi ambao walianza kufanya ghasia kubwa kwa madai kuwa wabunge hao wameuawa kwa makusudi, licha ya Jeshi la Polisi la Kenya kutoa maelezo kuwa hayahusiani kabisa na masuala ya kisiasa.

 

 

 

Hata hivyo, viongozi wa ODM wamedai kuwa mauaji hayo ni njama za serikali za kutaka kupunguza wabunge wa chama hicho na wameomba upelelezi ufanyike kwa kuwatumia makachareo wa Marekani (FBI).

 

Source: Mwananchi

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents