Habari

Mauaji ya askari magereza yazua hofu

HALI imerejea kuwa shwari mjini hapa baada ya kuwa tete mwishoni mwa wiki kutokana na mauaji ya askari mmoja wa Magereza yanayodaiwa kufanywa na Polisi na kusababisha wenzake warande huku na kule wakiwa na silaha na kusababisha hofu kwa raia.

Eline Shaidi, Babati

HALI imerejea kuwa shwari mjini hapa baada ya kuwa tete mwishoni mwa wiki kutokana na mauaji ya askari mmoja wa Magereza yanayodaiwa kufanywa na Polisi na kusababisha wenzake warande huku na kule wakiwa na silaha na kusababisha hofu kwa raia.

Habari zinasema kwamba askari huyo, sajini James alikufa kwa kupigwa risasi zaidi ya sita kichwani ambazo inasemekana zilifyatuka kutoka katika bunduki ya polisi aliyekuwa amekaa nyuma yake katika gari la polisi alimokuwa ameomba lifti. Risasi hiyo inasemekana ilifyatuka wakati gari hilo likiwakimbiza watuhumiwa wa ujambazi.

Kutokana na mauaji hayo ilibidi zifanyike jitihada za ziada Jumamosi usiku kuzuia idadi kubwa ya askari wa Magereza baadhi yao wakiwa na silaha, waliovamia kituo cha polisi cha Babati wakitaka maelezo kuhusu nini kilichosababisha mwenzao afe baada ya kupigwa risasi kadhaa na polisi.

Chanzo cha vurugu hizo ilikuwa ni taarifa zilizotolewa awali kwamba askari huyo wa Magereza ambaye mara ya mwisho alionekana akipewa lifti katika gari la polisi, aliuawa kwa kutuhumiwa jambazi.

Polisi wanadaiwa pia kwamba waliwazuia askari wa Magereza wasiende kuitambua maiti yake katika chumba cha maiti bila idhini. Tukio la mauaji lilitokea saa moja na robo Jumamosi usiku katika Kitongoji cha Sinai, umbali wa kilometa moja na nusu kutoka Babati Mjini.

Mwandishi wa habari hizi alipofika katika kituo cha polisi muda mfupi baada ya tukio alikuta kundi kubwa la askari magereza waliokuwa wamevalia kiraia na wengine wamevalia sare huku wakiwa wameshika silaha wakimuamuru mkuu wa kituo kutoa taarifa za kina juu ya kifo cha mwenzao.

Askari hao ambao walipelekwa na gari ya KIA namba STJ 2336 huku wengine wakiwa wanatembea kwa miguu na Mkuu wa Gereza hilo, SSP Kapungu. Baada ya kufika kituoni mkuu wa polisi hakutaka kutoa taarifa zozote juu ya kifo hicho akidai kuwa alikuwa kwenye kikao kilichokuwa kinajadili suala hilo. Jibu hilo halikuwaridhisha askari wa Magereza ambao nusura waanze fujo wakilazimisha kupewa maelezo.

Vurugu hizo zilizidi baada ya mkuu huyo wa kituo cha polisi kuwatishia askari wa magereza kuwa ataamuru askari wake wawapige risasi endapo hawatafuata taratibu walizoelezwa na wao wakamjibu kwamba wapo tayari kushambuliwa.

Hali ilitulia baada ya saa moja baada ya kuwasili kwa Kamanda wa Magereza wa Mkoa, Abel Chitama aliyewasihi wawe na subira wakati akifanya mazungumzo na mkuu wa kituo.

Askari hao walikuwa na hasira kutokana na madai kuwa askari hao baada ya kumuua askari magereza walienda kuuhifadhi mwili huo katika chumba cha kuhifadhia maiti katika hospitali ya Mrara mjini hapo na kumuamuru mlinzi wa chumba hicho kutoruhusu askari yeyote wa magereza kuingia ndani kuona mwili huo ambao askari hao walidai kuwa ni jambazi.

Uchunguzi uliofanywa na HabariLeo ulibaini kuwa siku hiyo ya tukio Sajini James Ngollo alipewa lifti kwenye gari la polisi Land Rover 110 namba DFP 7253 ambalo hufanya doria kwenye barabara kuu ya kutokea Babati Mjini kwenda Arusha likiwa na askari kanzu wawili, akiwamo mmoja mwenye silaha.

Ofisa Mnadhimu wa Polisi, Simon Mgawe alithibitisha kutokea kwa tukio hilo akidai kuwa tukio hilo lilisababishwa na uzembe uliotokana na askari huyo baada ya kushika vibaya silaha hiyo ambayo kutokana na mtikisiko wa gari ilifyatuka na risasi kumpata askari magereza huyo.

Alisema kuwa askari huyo ameshikiliwa na atafikishwa mahakamani uchunguzi utakapokamilika. Mwili wa marehemu unatarajiwa kupelekwa nyumbani kwao Dar es Salaam kwa mazishi.

 

Source: Habari Leo

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents