Habari

Mauaji ya mfugaji

SUALA la mauaji ya mfugaji Shigella Sahani wa Utengule, Kilombero mkoani Morogoro, limeingia katika sura mpya kufuatia familia ya marehemu kutaka serikali ilipe fidia ya sh 1.5 bilioni, vinginevyo itaiburuza mahakamani.

Na Mwandishi Wa Mwananchi


SUALA la mauaji ya mfugaji Shigella Sahani wa Utengule, Kilombero mkoani Morogoro, limeingia katika sura mpya kufuatia familia ya marehemu kutaka serikali ilipe fidia ya sh 1.5 bilioni, vinginevyo itaiburuza mahakamani.


Hali hiyo imekuja wakati tayari, timu nyingine ya maafisa wa usalama wa taifa, ikiwa iko wilayani Kilombero na tayari imehoji watu mbalimbali baada ya tume ya polisi iliyoundwa na Mkurugenzi wa makosa ya Jinai (DCI), Robert Manumba kumaliza kazi yake.


Familia hiyo imetoa madai hayo kupitia wakili wake Mussa Roma wa Kampuni ya Millenium Law Chambers.


Hati ya madai ya wakili huyo yenye kumbukumbu namba MLC/DN/AG-1/2007 ya Juni 5 mwaka huu ambayo Mwananchi imefanikiwa kupata nakala yake, inasema gharama hizo ni kwa ajili ya hasara ambayo familia hiyo imepata kutokana na kuondokewa na kijana huyo Mei 13 mwaka huu mwenye umri wa miaka 18.


Katika hati hiyo, inaeleza kwamba kifo cha kijana huyo kilitokana na kipigo kilichoagizwa na maafisa wa polisi.


Hati hiyo inafafanua zaidi kwamba, Mei 10, 2007, maafisa wawili wa polisi wakiwa na Afisa Mtendaji wa kata ya Utengule, mwenyekiti wa kijiji cha Utengule na Afisa Tarafa wa Idundembo, inaaminika walipokea amri kutoka kwa Mkuu wa Wilaya ya Kilombero kwenda katika kijiji cha Utengule, ambapo walipofika nyumbani kwa mteja wake, polisi waliamuru wafugaji kuondoa mifugo yote.


Waliamuru kuondolewa kwa mifugo hiyo ambayo ni pamoja na kondoo na mbuzi, kuelekezwa Lindi kama serikali ilivyoelekeza.


Huku familia ikionyesha azma hiyo ya kuishtaki serikali, jeshi la polisi limeendelea kukalia ripoti ya uchunguzi ya sakata hilo.


Vigogo wa jeshi la polisi wamekuwa wakitupiana mzigo kila mmoja akiagiza aulizwe mwingine.


Wiki moja iliyopita Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Kamishna Robert Manumba, aliliambia gazeti hili kabla haijaenda likizo kwamba, alikuwa akisubiri tume hiyo ikamilishe kazi yake.


Kamishna Manumba alisema (wiki hiyo), kwamba tume hiyo ilikuwa ikikamilisha kazi yake na alipoulizwa iwapo ilikuwa iko katika hatuza mwisho, alisema “ndiyo inamalizia”.


Lakini baada ya wiki moja tangu kamishna Manumba kwenda likizo, anayekaimu kiti hicho, Kamishna Msaidizi Mwandamizi, Kasala, alipoulizwa zaidi ya mara tatu wiki iliyopita, alikuwa akikwepa kutoa taarifa kuhusu suala hilo.


Badala yake, alipobanwa zaidi, alisema ” naomba kamuulize Kivuyo (Peter, Mkurugenzi Msaidizi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai)”.


Kasala aliongeza ” lakini kuna wenzako amewaeleza kwamba taarifa zitatolewa baada ya wiki moja”.


Mfugaji huyo kifo chake ambacho kimejaa utata, ni doa jingine kwa watendaji ndani ya jeshi la polisi nchini.


Tayari kumekuwa na utata wa taarifa za kiuchunguzi wa kitalaamu uliofanyiwa maiti ya Shigela, ambapo uliofanyika Hospitali ya Taifa Muhimbili unaonyesha aliuawa na ule wa hospitali ya teule ya St Francis uliofanyika awali ulionyesha kuwa kifo chake kilitokana sababu nyingine na sio kuuawa.


Tayari ofisi ya mkuu wa mkoa wa Morogoro ilishatoa taarifa iliyoambatishwa na maeneo ya wafugaji yaliyopimwa ya wilaya ya Kilombero kwenda kwa watendaji wa serikali wilayani humo ikionyesha kuwa eneo la wafugaji wa kijiji cha Utengule tarafa ya Mlimba wilayani Kilombero lililotengwa kwa ajili ya wafugaji.


Barua ya Katibu tawala wa mkoa wa Morogoro kwenda kwa Mkurugenzi wa halmashauri ya Kilombero ya Mei 16 mwaka huu iliyosainiwa kwa niaba yake na E. Shayo, inaeleza kuwa mkoa wa huo una jumla ya vijiji 102 vilivyotengwa kwa ajili ya wafugaji Utengule kikiwamo.


“Nimeagizwa na katibu tawala mkoa niwarudishe (wafugaji) kwako ili uweze kuwashughulikia suala hilo kwani kufuatana na makubaliano ya kuwa na vijiji 102 vya ufugaji mkoani Morogoro, kijiji cha Utengule ni kati ya vijiji hivyo,” inaeleza sehemu ya barua hiyo.


Mgogoro wa wafugaji na baadhi ya watendaji wa serikali katika tarafa ya Mlimba ulizidi kukua baada ya Shigela kudaiwa kuuawa Mei 13, 2007 polisi wilayani Kilombero wakati wakifanya operesheni ya kuwaondoa wafugaji katika kijiji hicho.


Wakati ndugu wakidai marehemu aliuawa kutokana na kipigo cha askari, polisi wanadai alikufa kutokana na kuishiwa pumzi.


Hata hivyo, uchunguzi uliofanywa na mtalaam wa patholojia katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Dk P. A Ogweyo, unaonyesha kuwa kabla ya kifo chake, Sahani alipigwa na kisha kunyongwa.


Uchunguzi huo, unaonyesha kuwa marehemu alikutwa akiwa amekatwa koromeo kwa ndani, hali inayoonyesha kuwa alinyongwa.


Pia uchunguzi wa Dk Ogweyo unaonyesha marehemu akiwa amevunjika mbavu kadhaa pamoja na damu kuvia kichwani, hali inayoashiria kipigo alichokipata kutoka kwa askari waliomkamata.


Katika tarifa yake ambayo ilikataliwa na wanandugu kutokana na kukiukwa kwa taratibu za uchunguzi wa marehemu, mganga kuu wa hospitali teule ya St Francis Dk Pasians Kibatala anasema marehemu alikutwa na michubuko katika sehemu mbalimbali za mwili wake, hii ikimaanisha kuwa taarifa yake ingeunga mkono maelezo ya polisi waliodai alikufa kutokana na kuishiwa pumzi. 


Kwa mujibu wa maelezo ya Dk Kibatala, uchunguzi wa mwili wa marehemu ulionyesha alikuwa na michubuko midogo usoni, povu mdomoni, kuvimba kwa ulimi, michubuko kuanzia usoni hadi kifuani, jeraha dogo katika mguu, mistari katika mkono na kiwiko cha kushoto pamoja na mistari mingine katika vifundo vya miguu yote miwili.


Lakini taarifa ya uchunguzi ya Dk Ogweyo inaonyesha kuwa mwili wa marehemu ulipata madhara makubwa kabla ya kifo chake, ingawa kwa muhtasari anasema chanzo cha kifo ni kufeli kwa mapafu (Respiratory failure due to severe lung contusion).


Baadhi ya maeneo ambayo ripoti hizo zinazotofautiana ni pamoja na madhara ya ndani aliyoyapa marehemu. Dk Ogweyo anasema mfupa wa shingo ya marehemu ulivunjika kiasi kwamba shingo yake ilikuwa inazunguka kwa zaidi ya nusu mduara na kwamba mapafu yalikuwa yamezidiwa yalikuwa yamejaa damu. Pia kulikuwa na uharibifu katika ubongo.


Maelezo ya Dk Obwenyo kwa kiasi kikubwa yanathibitisha maelezo ya wanandugu kuwa marehemu aliuawa na si kutokana na uchovu wa kukimbia kama ilivyoelezwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Thobias Andengenye, alipozungumza na gazeti hili.


Source: Mwananchi

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents