Habari

Mbowe ajitetea kuhusu ufisadi

MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, amesema anaamini habari za yeye kudaiwa mamilioni na Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF) na amri ya kukamatwa kwake, zinakuzwa na wapinzani wake katika siasa aonekane fisadi na apunguze kasi ya kutaka kuchukuliwa hatua kwa waliozoa mabilioni Benki Kuu (BoT) kupitia Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA).

Mwandishi Wa Habari Leo

 

 

 

MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, amesema anaamini habari za yeye kudaiwa mamilioni na Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF) na amri ya kukamatwa kwake, zinakuzwa na wapinzani wake katika siasa aonekane fisadi na apunguze kasi ya kutaka kuchukuliwa hatua kwa waliozoa mabilioni Benki Kuu (BoT) kupitia Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA).

 

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mbowe alikiri kuwa kampuni yake ya Mbowe Hotels Ltd ilikopa Sh milioni 15 kutoka NSSF mwanzoni mwa miaka ya 1990, lakini ameshindwa kumalizia kulipa mkopo huo kutokana na utata uliopo kwenye riba, licha ya kuwapo kwa amri ya Mahakama Kuu tangu mwaka 2004 ya kutaka akamatwe kwa kushindwa kulipa.

 

“Habari hizi zinazojaribu kunipaka matope leo hii zikigeuza kesi ya Mbowe Hotels ambayo kimsingi ni ya biashara ili ichukue sura ya siasa na ufisadi…zinalenga kuniharibia heshima yangu kwa jamii na kunichonganisha na wanachama wa Mfuko (NSSF),” alisema Mbowe huku akitamba kwamba ataendelea kupigania haki.

 

Alisema kutokana na vuta nikuvute hiyo ya deni la NSSF, mkewe, Dk. Lillian Mbowe, alikamatwa mwaka jana na kupelekwa Mahakama Kuu mbele ya aliyekuwa Jaji Kiongozi Amiri Manento, ajieleze kwa nini asifungwe kwa kushindwa kuheshimu amri ya kulipa deni.

 

Wakati huo Freeman alikuwa masomoni Uingereza. Habari za mkopo unaolalamikiwa na Mbowe na riba juu yake ziliripotiwa kwa mara ya kwanza magazetini wiki iliyopita, huku ikielezwa kuwa deni hilo limefikia Sh bilioni 1,200 na kwamba Mahakama Kuu imetoa amri ya kukamatwa kwa wakurugenzi wa Mbowe Hotels.

 

Akijitetea jana, Mbowe alisema kampuni yake ilipewa mkopo huo kwa ajili ya upanuzi na uboreshaji wa hoteli yake Dar es Salaam na wakati anakopa riba iliyokuwa inatolewa na NSSF, ilikuwa asilimia 31 na hadi kufikia Juni mwaka jana, kampuni yake ilikwisha kulipa Sh milioni 75.5, kiasi ambacho alisema ni mara tano ya kiwango kilichokopwa.

 

Alisema ugomvi wake na NSSF ni riba, kwani kampuni yake imekuwa inaiandikia NSSF ipitie upya mkataba wa mkopo huo, jambo alilodai ni la kawaida kwa kila taasisi ya fedha inayojua wajibu wake na yenye nia njema kwa wateja wake. “Mchanganuo wa kitaalamu wa deni la sasa la Mbowe Hotels Ltd pamoja na riba ni Sh milioni 43.2.

 

Hili mimi ndilo ninalojua kwamba bado wanatudai na tumekuwa tunawaomba tukae nao turejee mkataba juu ya mchanganuo huu, lakini hawataki,” alisema. Alisema kama mfanyabiashara, amekuwa anakopa katika benki mbalimbali kwa ajili ya uwekezaji katika miradi mbalimbali na amekuwa analipa bila matatizo.

 

“Iweje hawa NSSF wagome kufanya hivyo…na wao ndiyo wamekuwa chanzo cha kuchelewesha kulipwa kwa deni hilo, kwani hawataki kukaa na sisi kurejea mkataba huo,” alisema Mbowe anayemiliki baadhi ya biashara nchini, zikiwamo za hoteli. Mbowe alisema mkataba na NSSF ulioingiwa mwaka 1990 uligubikwa na mizengwe mwaka mmoja tu tangu kuingiwa.

 

Alisema kampuni yake iliomba kuongezewa mkopo kukamilisha mradi uliokusudiwa, lakini ilichukua mwaka mmoja kutoa jibu la kukataa kwa madai kuwa kutoa fedha za ziada siyo sera yao. Mfanyabiashara huyo alisema baada ya kukataliwa alianza upya mchakato wa kutafuta mkopo na akaenda benki ya CRDB ikakubali kumkopesha.

 

“Wakati hali hii ikiendelea, NSSF ilianza kudai marejesho ya riba kwa mkopo waliotoa kwa mradi walioufadhili na kuutekeleza.” Alisema mwaka 1996 ukiwa mwaka mmoja baada ya Uchaguzi Mkuu wa kwanza wa mfumo wa vyama vingi ambao alishiriki kama mgombea wa upinzani katika Jimbo la Hai, wadhamini wa NSSF walifungua kesi ya madai katika Mahakama Kuu wakidai malipo ya Sh milioni 80.1 ikijumuisha salio la deni mama la Sh milioni 12 na riba ya Sh milioni 68.1.

 

Alisema tangu mwaka 2003 walikubaliana na NSSF wakae wazungumze, lakini baadaye shirika hilo likawa kimya. Alisema mwaka jana, kampuni yake iliiandikia tena NSSF kuomba wakubali mapendekezo ya kumaliza deni hilo na barua nyingine; lakini hawajajibu barua hizo hadi leo, ikiwa ni miezi minane tangu waandikiwe barua hizo.

 

Juhudi za kuwapata maofisa wa NSSF kuzungumzia suala hilo hadi jana jioni hazikufanikiwa. Mbowe alisema anaamini baadhi ya watu wanavitumia vyombo vya habari kumchafua yeye ili Watanzania wageuzie mawazo yao kwenye habari zake na NSSF na wasahau habari za ufisadi wa EPA na Richmond zinazowagusa baadhi ya viongozi.

 

 

 

Source: Habari Leo

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents