Mbunge aliyemtwanga msaidizi wake atajwa

MBUNGE mmoja wa Wilaya ya Kinondoni, anayedaiwa kumpiga msaidizi wake wa zamani na kumjeruhi, sasa amejulikana

na Mwandishi Wa Tanzania daima

MBUNGE mmoja wa Wilaya ya Kinondoni, anayedaiwa kumpiga msaidizi wake wa zamani na kumjeruhi, sasa amejulikana.

Mbunge huyo ni Idd Azzan, wa Jimbo la Kinondoni, anadaiwa kumpiga
msaidizi wake wa zamani, Shawej Mkumbuli, ambaye kwa sasa ni Mwenyekiti
wa Kata ya Magomeni.

Sababu kubwa ya ugomvi huo, imeelezwa kuwa ni
hofu ya uchaguzi, ambapo mbunge huyo anadai Shawej amekuwa akijenga
mtandao na kuandaa mkakati maalumu wa kumng’oa katika jimbo lake,
kwenye uchaguzi mkuu ujao.

Akizungumza katika ofisi za Tanzania Daima
juzi, Shaweji alisema ugomvi kati yake na mbunge huyo, ulitokea
Jumatano iliyopita, katika eneo la wazi linalotumika kuegeshea magari,
katika ofisi ya Halmashauri ya Wilaya ya Kinondoni.

Akiwa ameongozana na Katibu Mwenezi wa kata
hiyo, Juma Matandika na viongozi wengine waliodai kushuhudia ugomvi
huo, Shawej alisema siku hiyo kulikuwa na uchaguzi wa naibu meya,
ambapo mbunge huyo na naibu meya aliyemaliza muda wake, Tulian Bujugo,
walikuwapo kwenye ukumbi wa Manispaa ya Kinondoni.

Alisema katika uchaguzi huo, yeye (Shewej)
pamoja na viongozi wengine wa kata hiyo, walikuwa wakimpigia debe
Diwani wa kata yao, Bujugo, ili atetee kiti chake lakini alishindwa na
badala yake, Diwani wa Kata ya Goba, Ibrahim Kisoki, ndiye aliyeibuka
mshindi.

“Sisi tulikuwa tumekaa kwenye sehemu ya
wageni ukumbini. Wakati kura zinaendelea kuhesabiwa, ghafla nilimwona
mgombea wetu ambaye muda wote alikuwa amekaa jirani na Idd Azzan,
akitoka nje kwa haraka, nikaamua pia kutoka na kumfuata, lakini
sikumwona.

“Badala yake nikakutana na viongozi wetu
wengine wako nje, tukawa tunabadilishana mawazo, hasa baada ya kubaini
kuwa mgombea wetu alikuwa anaelekea kushindwa.

“Tukiwa katikati ya mazungumzo, Idd Azzan,
alikuja kuungana nasi na baada ya kusalimiana naye, akaanza kusema
Shawej nimepata habari zako siku nyingi kuwa unanichimba, unanifitini
eti una mgombea wako wa ubunge na unajenga mtandao wa kuniangusha,”
alisema Shewej.

“Nilitaka kujibu, lakini
alinibeza kwa kunitaka nisijibu chochote, lakini nami nikawa mbishi
kutaka nijibu, ndipo ghafla alinirukia na kunipiga ngumi ya kichwa,
kofi na kurusha teke ambalo lilinikosa.

“Kanipiga vibaya ndugu yangu, lakini sikutaka
kurudishia, ingawa ninaweza kupigana naye, bahati nzuri viongozi
niliokuja nao hapa ofisini kwako, walikuwapo, wakaamua kuingilia kati
kuamlia ugomvi huo,” alisema Shaweji, huku akionyesha sehemu ya jicho
na mkono, alivyodai kuumizwa.

Alisema malalamiko ya Azzan dhidi yake,
amekuwa akiyasikia muda mrefu, lakini aliyapuuza kwa madai kuwa mbunge
huyo ni mtu wake wa karibu, hivyo kama ana malalamiko angeweza kumwita
na kuzungumza naye kindugu.

Shawej alimtaja mtu anayedaiwa kuanza
kumpigia debe kuwa ni Tarimba Abbas, jambo ambalo alisema si la ukweli,
bali inatokana na hofu ya mbunge huyo.

Akizungumzia uhusiano wake na Azzan, tangu
mbunge huyo alipoingia madarakani, alisema amekuwa msaidizi wake,
lakini ilipofika Mei mwaka jana, aliacha kazi hiyo kutokana na majukumu
mengine aliyokuwa nayo kichama.

“Yeye mwenyewe Azzan, ndiye aliyeniambia kuwa
sasa niache kuwa msaidizi wake kutokana na kazi nyingi nilizokuwa nazo
kichama na tulikubaliana nimchagulie msaidizi mwingine na tangu wakati
huo, nimekuwa na maelewano na mbunge wangu vizuri,” anasema.

Shawej alisema yeye ndiye aliyechangia Azzan
kuwa diwani wa kata yao na hata baadaye kuwa mbunge, hivyo alielezea
kushangazwa kwake na hatua ya mbunge huyo kutoa kipigo kwake kwa tuhuma
zisizo za ukweli.

Hata hivyo, alisema kama mwenyekiti wa kata,
ameamua kulipeleka suala hilo kwenye kamati ya siasa ya kata,
inayotarajia kukutana wiki hii na kupeleka taarifa ya tukio hilo la
aibu kwenye ngazi za juu za chama.

Mbali na kulipeleka kwenye chama, suala hilo
limeripotiwa katika Kituo cha Polisi cha Magomeni, ambapo Idd Azzan,
ndiye aliyefungua jalada la kudai kuwa ametukanwa na Shawej.

Habari kutoka ndani ya kituo hicho cha
polisi, zilikiri kuwapo kwa tukio hilo, lakini mlalamikaji akiwa Idd
Azzan, ambaye amedai kutukanwa na Shawej.

Tanzania Daima ilipowasiliana na Tarimba juu
ya kuwapo kwa malalamiko dhidi yake ya kutaka kuwania jimbo hilo,
alikataa katakata huku akizitaka pande hizo mbili zinazotofautiana,
zisimhusishe kwenye ugomvi wao.

“Mimi ndugu yangu haya mambo sijui yanatokea wapi. Ila wasinihusishe kwenye ugomvi wao,” alisema kwa kifupi Tarimba.

Juhudi za kumtafuta Azzan kwa simu yake ya mkononi, hazikufanikiwa, kwani muda wote ilikuwa imezimwa.

Azzan amekuwa mbunge wa jimbo hilo mwaka 2005, baada ya kumshinda aliyekuwa mbunge wa Kinondoni, Peter Kabisa.

 

Source: Tanzania Daima

 

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents