Siasa

Mbunge atuhumu kampuni ya Meremeta kuchota mabilioni Benki

MBUNGE wa Musoma Vijijini, Nimrod Mkono ameituhumu Kampuni ya Meremeta kuwa ni ya kitapeli na kwamba ilijichotea mabilioni ya shilingi kwa mgongo wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kwa madai ya kununua dhahabu katika Mgodi wa Buhemba (BGM).

Ramadhan Semtawa Dar na Beldina Nyakeke, Musoma

 

 

 

MBUNGE wa Musoma Vijijini, Nimrod Mkono ameituhumu Kampuni ya Meremeta kuwa ni ya kitapeli na kwamba ilijichotea mabilioni ya shilingi kwa mgongo wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kwa madai ya kununua dhahabu katika Mgodi wa Buhemba (BGM).

 

 

 

Mkono alitoa madai hayo wakati akitoa maoni yake kwenye Kamati ya Kuchunguza Mikataba ya Madini iliyoundwa na Rais Jakaya Kikwete, mwishoni mwa mwaka na kuwa chini ya uwenyekiti wa Jaji Paul Bomani.

 

 

 

Akitoa maoni yake, alipendekeza kuwa mikataba yote ya madini nchini ifumuliwe upya ili iwanufaishe Watanzania wote, kuliko hivi sasa ambapo mapato ya madini yanaishia mikononi mwa watu wachache.

 

 

 

Alifafanua kwamba, Kampuni ya Meremeta ilichota fedha kwa ajili ya kununua dhahabu katika mgodi wa Buhemba, lakini kila ilipofikisha mzigo Afrika Kusini, ilidai ya kuwa imeibiwa.

 

 

 

Aliitaka Mkono kamati hiyo kwenda Afrika Kusini kuchunguza ili kupata ukweli kama dhahabu hiyo iliibwa.

 

 

 

Alisema kiasia cha gawaio cha Sh 250 milioni kwa mwaka kutoka kwa baadhi ya makampuni, ni kidogo kwani hakiwanufaishi Watanzania walio wengi iliinganishwa na faida wanayopata wawekezaji wa kwenye sekta hiyo.

 

 

 

Mbunge huyo alifafanua kwamba, dhana ya ‘Maisha bora kwa kila Mtanzania’ imekuwa ni ndoto kwa wakazi wa Kata ya Buhemba kutokana na kuzorota kwa huduma za jamii kulikosababishwa na mgodi huo.

 

 

 

Kwa upande wao, wananchi wengine waliohojiwa walisema mgodi huo unamilikiwa na vigogo ambao ni watuhumiwa wa ufisadi katika Serikali ya Awamu ya Tatu na iliyopo madarakani, tofauti na inavyoelezwa kwamba unamilikiwa na serikali.

 

 

 

Wakazi wa Kata ya Buhemba walisema hayo wakati wakitoa maoni yao kwa kamati hiyo ambayo ujumbe wake uliongozwa na Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto kabwe.

 

 

 

Walisema kutokana na mgodi huo kumilikiwa na mafisadi kwa maslahi yao binafsi, hali za wakazi wa vijiji vinavyozunguka mgodi huo zinazidi kuwa duni kufuatia huduma muhimu za kijamii kukosekana katika kata hiyo.

 

 

 

Walifafanua kuwa huduma mbalimbali za kijamii zilizokuwa zikipatikana katika vijiji hivyo kabla ya kuwepo kwa mgodi huo, hivi sasa hazipo baada ya kuvunjwa na kuharibiwa kabisa na uongozi wa mgodi.

 

 

 

Huduma hizo ni pamoja na maji, elimu, barabara na afya ambazo kwa pamoja zilibomolewa na mgodi kwa maelezo kuwa wangepatiwa huduma bora zadi ya zilizokuwepo awali.

 

 

 

“Awali tulikuwa na vyanzo tisa vya maji vya asili, lakini mgodi ulipokuja uliviharibu vyote kwa vile vilikuwa ndani ya eneo la uchimbaji,” alisema mkazi wa kijiji cha Biatika, Simon Chacha na kuongeza:

 

 

 

“Zahanati yetu tuliyokuwa tukiitegemea kwa ajili ya huduma za kiafya hasa kwa wajawazito, pia ilivunjwa kwa ahadi ya kujengewa nyingine ya kisasa, lakini tuliambulia ramani tu.”

 

 

 

Naye Mchungaji wa Kanisa Anglikana Buhemba, Samwel Nyakarungu alisema:, “Tumefanyiwa hujuma kwani tunasikia kwamba hata viongozi wetu wakuu wa Wilaya ya Musoma na mkoani Mara, wana maslahi kwenye mgodini huo, hivyo katika suala hili tunaamini kwamba hawatweza kututatua kero zetu.”

 

 

 

Mchungaji huyo aliendelea kusema: “Hii hali imechangia kwa kiasi kikubwa wakazi wa Kata ya Buhemba kuendelea kutumnia maji ya sumu kutoka kwenye mashimo yaliyokuwa yakitumika kuchimba dhahabu”.

 

 

 

Alisema wananchi wa Kata hiyo wanaishi katika lindi la umasikini ktuokana na kutokuwa na shughuli za kufanya, kwa ajili ya kujiletea maendeleo kufuatia ardhi waliyokuwa wakiitegemea kwa ajili ya kilimo kuchukuliwa na mgodi.

 

 

 

Mchungaji huyo alifafanua kuwa wakati hali ikiwa ni hivyo bado hakuna mrahaba unaotolewa na uongozi wa mgodi huo kwa ajili ya kuendeleza miradi mbalimbali ya kimaendeleo katika kata hiyo.

 

 

 

Wananchi waliitaka Kamati hiyo kuwahoji viongozi hao wa wilaya na mkoa juu ya mmiliki halisi wa mgodi huo ambao sasa umefungwa. Mgodi huo ulianza uzalishaji mwaka 2002 na kufungwa Januari, mwaka huu.

 

 

 

Kampuni ya Meremeta imejaa utata kutokana na kuelezwa kwamba ni ya serikalini, lakini huku nafasi ya serikali ikwa haijulikani.

 

 

 

Kampuni ya Meremeta imehusishwa na aliyekuwa Gavana wa BoT Daud Ballali, ambaye mkewe Anna Muganda na vigogo mbalimbali wa serikali iliyopo na iliyopita akiwemo Andrew Chenge.

 

 

 

Kamati ya Madini iliundwa na Rais Kikwete mapema mwishoni mwaka uliopita, kama moja ya hatua za kuhakikisha madini yanayochimbwa yananufaisha nchi na watu wake.

 

 

 

Source: Mwananchi

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents