Habari

Mbunge wa CCM amtisha Lowassa

MBUNGE wa Nzega, Lucas Selelii (CCM), jana aligeuka ‘mbogo’, akitishia kukwamisha bajeti za wizara tatu, ikiwamo ya Ofisi ya Waziri Mkuu.

na Mwandishi Wa Tanzania Daima


MBUNGE wa Nzega, Lucas Selelii (CCM), jana aligeuka ‘mbogo’, akitishia kukwamisha bajeti za wizara tatu, ikiwamo ya Ofisi ya Waziri Mkuu.


Alitoa msimamo wake huo wakati akichangia hotuba ya bajeti ya serikali kwa mwaka 2007/08, iliyowasilishwa Alhamisi iliyopita na Waziri wa Fedha, Zakia Meghji.


“Mimi leo nimesali na nimefunga. Nia ya kufunga ni kumuomba Mungu aweze kunisadia kuchangia bajeti hii vizuri. Lakini leo nataka kusema ukweli na kila siku msema ukweli ni kipenzi cha Mungu,” alisema Selelii wakati akianza kuchangia.


Katika mchango wake, Selelii, ambaye ni mmoja wa wabunge ambao hutoa mawazo yao kwa uhuru, aliwataka mawaziri kufahamu kuwa ni makosa kuendelea kuwaona wabunge wanaokaa viti vya nyuma kuwa ni ‘hamnazo’ (watu wasio na akili timamu), kitendo ambacho kinapaswa kupingwa.


“Mstari wa mbele wanatuona mstari wa nyuma hamnazo, tulikataa Shirika la Ndege Tanzania (ATC) lisiuzwe kwa mwekezaji wa kutoka Afrika Kusini, hatukusikilizwa kabisa na badala yake walitumia uwezo wote wakafanikiwa,” alisema.


Alisema kuwa uamuzi wake wa kuondoa shilingi katika wizara hizo, unatokana na serikali kushindwa kutekeleza ahadi zake kwa muda mrefu.


Ingawa hakuziorodhesha kwa mpangilio mmoja, katika mchango wake Selelii alisemea kwa uchungu mambo yasiyoridhisha yanayotokea katika sekta za miundombinu, mifugo pamoja na madini.


“Nasema mbali ya Ofisi ya Waziri Mkuu, wizara nyingine ambazo naweza kuweka msimamo wangu ni pamoja na Miundombinu, Maliasili na Wizara ya Nishati na Madini.


Mbunge huyo alisema moja ya wizara ambayo angeondoa shilingi ni Wizara ya Miundombinu, kwa madai kuwa hajaona mpango wa ujenzi wa barabara ulioainishwa katika bajeti iliyopita.


Alisema katika bajeti ya mwaka uliopita, barabara hizo ziliainishwa lakini kwenye bajeti ya awamu hii hazionekani.


Kwa Wizara ya Miundombinu, alisema ‘ugomvi’ wake ni wa kutoanza kwa ujenzi wa barabara katika maeneo mengi, zikiwamo barabara za Manyoni – Itigi, Tabora – Urambo hadi Kigoma na nyinginezo katika maeneo ya magharibi mwa nchi.


Kwa upande wa Wizara ya Nishati na Madini, mbunge huyo alisema kwa muda mrefu serikali imekuwa ikiahidi kupeleka umeme katika vijiji kadhaa jimboni mwake, lakini hakuna chochote kinachofanyika mpaka sasa.


Akionekana kuzungumza kwa hisia kali, Selelii alisema kuna idadi kubwa ya vijana walikamatwa kwa kutuhumiwa kuiba madini lakini wizara inayohusika haijatoa tamko lolote.


Alisema kutotekelezwa kwa ahadi hizo za Serikali huwapa wakati mgumu wakati wa kampeni, kwani sehemu nyingine huonekana zimetengenezwa, na nyingine zikiwa zimeachwa.


“Sisi wengine tunaambiwa tususbiri… tusubiri, hawa wenzetu wao walio mbele (mawaziri) wanatengeneza za kwao, hii ni sahihi?” alihoji kwa hisia kali.


Alisema kama angekuwa na uwezo angeaanza kuwakata mishahara mawaziri hao wa wizara hizo mbili kwa kutotekeleza ahadi zao.


Selelii alisema wakati umefika kwa Wizara ya Mipango, Uchumi na Uwezeshaji, kuongozwa na waziri asiyekuwa mwanasiasa, badala yake awe mtaalamu wa uchumi.


Akizungumzia mifugo, alisema haikupewa kipaumbele kwenye bajeti zote zilizosomwa, na akasema ndiyo maana hata waziri katumia maneno ‘sekta ndogo’ kuielezea sekta ya mifugo.


Alisema Botswana ina ng’ombe milioni tatu, Tanzania ina ng’ombe milioni 19, lakini inazidiwa mapato na nchi hiyo katika sekta ya mifugo.


“Mifugo yetu mingi huishia katika minada hamsini, tisini over basi, ng’ombe anakwenda… hakuna cha zaidi, hivi tutafika kweli? Rais kaunda Wizara ya Mifugo, lakini waziri anasema sekta ndogo!” alishangaa.


Alizungumzia pia utalii na kusema Tanzania haiwezi kuendelea zaidi katika utalii kama itaendelea kutokuwa na shirika lake la ndege.


Alisema mashirika ya ndege yanayohudumia sasa nchini yanaanza katika nchi zao, na hayana uchungu na Tanzania.


“Bajeti hii ingekuwa na kipengele kinachoruhusu mbunge kutoa shilingi kwa kutoridhika na baadhi ya vipengele vya bajeti ningetoa shilingi kwa jambo hili mpaka lirekebishwe.


“Ndugu Spika (huwa mgumu wa kutaja neno Mheshimiwa!) ningeweza kutoa shilingi kwa mawaziri hawa watatu mpaka hapo watakapobadilisha, maana sisi tuliopo majimboni ndio tunaopata shida na wananchi wetu,” alisema.


“Yaani kama bajeti hii ingekuwa inaungwa mkono nusu nusu vipengele hivi nisingekubaliana navyo kabisa, kwani havimo humu wakati vilipaswa kuwepo katika bajeti,” alibainisha.


Alisema miundombinu ni eneo nyeti katika kuinua uchumi wa nchi, hivyo bajeti inapokuwa haionyeshi mwendelezo inawavunja moyo wananchi wa kuendelea kujituma kwani hawana kiunganishi baina yao na wengine ambao ndio wanaoweza kununua kinachozalishwa. 


Selelii pia aliilaumu sekta ya nishati na madini kwa kutopeleka umeme katika maeneo yaliyopaswa kupata umeme mpaka sasa na kutoonyesha mwendelezo wa miradi hiyo kwenye bajeti ya awamu hii.


Alisema pia wizara hiyo haitoi takwimu sahihi ya thamani ya madini yanayosafirishwa nje ya nchi wakati nchi ikiendelea kubaki bila madini maana yanapungua kila kunapokucha.


Alisema sekta ya madini ingesimamiwa vizuri ingeweza kuchangia kwa kiasi kikubwa katika pato la taifa kuliko kuendelea kutegemea kodi za wananchi kwa kuongeza kodi katika sekta mbalimbali.


Mawaziri waliotishiwa kuondolewa shilingi ni Waziri wa Miundombinu, Andrew Chenge, Waziri wa Nishati na Madini, Nazir Karamagi na Waziri Mkuu, Edward Lowassa.


Baada ya kumaliza kuchangia, Selelii aliunga mkono kwa shingo upande sana, akidai ameunga mkono kutokana na kubanwa na kanuni za Bunge pamoja na Ilani ya uchaguzi ya CCM, ambacho ndicho chama chake.


Naye Mbunge wa Viti Maalumu kupitia Vijana, Lucy Mayenga (CCM), ameitaka serikali iainishe maeneo yatakayopunguziwa fedha iwapo bajeti ya serikali haitatosha au kutakuwa na dharura.


Akichangia bajeti ya Wizara ya Fedha, Mayenga alisema kutokana na bajeti kuwa tegemezi, wafadhili wanaoahidi fedha wasipotoa, serikali huwa inahamisha fedha kutoka katika maeneo mengine na kupeleka katika maeneo mengine.


Alisema uhamishaji huo wa fedha umekuwa ukisababisha miradi muhimu kukwama kutokana na kutoangalia uzito wa maeneo yanayopunguziwa fedha kwamba yana umuhimu gani kwa jamii.


Alitoa mfano wa mwaka jana kuwa kutokana na kuwepo kwa upungufu wa fedha katika bajeti ya serikali, fedha ziliondolewa katika mradi wa kupeleka umeme vijijini na kuelekezwa katika maeneo mengine. 


Alisema kuondolewa kwa fedha hizo kumeathiri kwa kiasi kikubwa maeneo yaliyokuwa yakilengwa kupata umeme huo kwani jumla ya vijiji 46 miradi yake ilisitishwa. 


Alisema wananchi wanaoishi vijijini nao wana umuhimu wa kupatiwa umeme, hivyo ni vema serikali iwe inaangalia miradi ambayo haina athari kwa wananchi.


Souce: Tanzania Daima

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents