Michezo

Mechi ya Yanga Sc na Kagera yamponza Muamuzi ndani ya Kamati ya saa 72

By  | 

Kamati ya Bodi ya Uendeshaji na Kusimamia Ligi inayojulikana kama ‘Kamati ya Saa 72’ katika kikao chao cha Mwishoni mwa juma kimeibuka na maamuzi mazito baada ya kurejea kupitia mchezo mmoja baada ya mwingine.

Katika mechi namba 212 (Yanga 2 Vs Kagera Sugar 1), kamati imefuta kadi nyekundu ya moja kwa moja aliyopewa mchezaji wa Kagera Sugar, Mbaraka Yusuf, baada ya kubaini mchezaji huyo hakutenda kosa lililosababisha muamuzi ampe adhabu hiyo. Uamuzi huo umefanywa kwa mujibu wa Kanuni ya 9(8) ya Ligi Kuu.

Pia Muamuzi wa mechi hiyo, ameondolewa kuchezesha Ligi Kuu ya Vodacom kwa vile uamuzi aliofanya haukuwa sahihi. Hatua dhidi ya Muamuzi Mwangole imechukuliwa kwa kuzingatia Kanuni ya 38(1a) ya Ligi Kuu.

Hii ni mara ya pili kwa Ngole kushindwa kutafsiri sheria uwanjani kwani katika duru la kwanza alionywa baada ya kukataa bao la JKT Ruvu ilipocheza na Mtibwa Sugar katika mchezo wa Ligi Kuu ya msimu huu wa 2016/17.

Mechi namba 214 (JKT Ruvu 2 Vs Azam 2). Klabu ya Azam FC imepigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) kwa kosa la kutoingia vyumbani, na badala yake kukaa nje. Kitendo hicho ni kwenda kinyume na Kanuni ya 14(13) ya Ligi Kuu, na adhabu imetolewa kwa mujibu wa Kanuni ya 14(48) ya Ligi Kuu.

Mechi namba 215 (Mbao FC 1 Vs Tanzania Prisons 0). Mchezaji Jeremiah Juma wa Tanzania Prisons amefungiwa mechi tatu na kupigwa faini ya sh. 500,000 kutokana na kuonyeshwa kadi nyekundu baada ya kumpiga ngumi mpinzani wake. Adhabu hiyo imetolewa kwa mujibu wa Kanuni ya 37(3) ya Ligi Kuu.

Pia timu ya Tanzania Prisons imeagizwa kurudisha mpira uliochukuliwa na mshabiki wake baada ya kumalizika kwa mechi hiyo iliyofanyika Aprili 16, 2017 kwenye Uwanja wa Nyamagana jijini Mwanza.
Msimamizi Msaidizi wa Kituo cha Mwanza aliripoti kwa Meneja wa Prisons, Bw. Enock Mwanguku, tukio la shabiki huyo aliyechukua mpira huo na kuingia kwenye gari la timu hiyo. Meneja huyo aliahidi kufuatilia, lakini hadi timu yake inaondoka uwanjani hakutoa mrejesho wowote.

Mechi namba 220 (Majimaji 3 Vs Mwadui 0). Klabu ya Majimaji imepigwa faini ya sh. 500,000 kutokana na timu yake kuingia uwanjani kwa kutumia mlango usio rasmi. Adhabu hiyo ni kwa mujibu wa Kanuni ya 14(48) ya Ligi Kuu.

Klabu zote zimepigwa faini ya sh. 500,000 kila moja kwa timu zao kutoingia vyumbani na kusababisha wachezaji wakaguliwe wakiwa nje ya vyumba. Adhabu hiyo ni uzingativu wa Kanuni ya 14(48) ya Ligi Kuu.

BY HAMZA FUMO

Jiunge na Bongo5.com sasa

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook, Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Bongo5!

Add a comment

comments