Habari

Meghji afunga mjadala wa bajeti kwa hasira

WAZIRI wa Fedha, Zakia Megheji ameitimisha hotuba yake ya bajeti kwa kutoa hotuba ya majumuisho huku akionyesha kuwa na hasira dhidi ya vyombo vya habari na baadhi ya wabunge walioonyeshwa kukerwa na vipengele kadhaa katika hotuba yake wiki iliyopita.



Waandishi Wa Mwananchi Dar na Dodoma


WAZIRI wa Fedha, Zakia Megheji ameitimisha hotuba yake ya bajeti kwa kutoa hotuba ya majumuisho huku akionyesha kuwa na hasira dhidi ya vyombo vya habari na baadhi ya wabunge walioonyeshwa kukerwa na vipengele kadhaa katika hotuba yake wiki iliyopita.


Mbali na kuvishambulia vyombo vya habari kwa madai ya kupotosha dhana nzima ya bajeti hiyo, pia aliwashambulia baadhi ya wabunge waliochangia bajeti hiyo, akisema wana upeo mdogo wa kuelewa mambo.


Akijibu hoja mbalimbali za wabunge wakati akihitimisha mjadala wa bajeti hiyo jana, Meghji alionekana zaidi kujibu hoja kisiasa, mfano ukiwa ni pale aliposema wabunge wa upinzani wanafanya jambo la maana kwa kubeba ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) wakati walipokuwa wakitoa hoja juu ya bajeti.


Megheji akitetea bajeti yake, alitumia muda mwingi kujibu hoja za wapinzani na akasema alifurahishwa na kipengele cha bajeti ya wapinzani ambacho kilieleza kuwa nia ya bajeti hiyo ni kuikosoa serikali pale palipotokea upungufu kwa ajili ya maendeleo.


Waziri huyo alisema katika hotuba ya bajeti hakuzungumzia kwamba wananchi wafunge mkanda bali bajeti yake ina muelekeo wa kuwataka wananchi wajifunze kujitegemea.


“Kuna baadhi ya wabunge walisema bajeti yangu ni ya kufunga mkanda. Ukweli ni kwamba bajeti niliyoitangaza ni bajeti ya kujitegemea. Ni bajeti ambayo wanafunzi watajifunza kujitegemea na ninaamini wako tayari kujitegemea kupitia bajeti mpya na si kama wabunge walivyosema,” alisema waziri huyo na kuongeza:


“Sijasema tufunge mikanda, bali nilitamka kwamba ni bajeti ya kuanza kujitegemea…wabunge walikuwa na wasiwasi na kodi ya mafuta hasa ya taa, lakini hakuna haja ya kufunga mikanda chakula tunacho, barabara zitajengwa…nilichosema ni kuwa kupanga ni kuchagua.”


Meghji akionekana mwenye hasira na jazba, alivigeukia vyombo vya habari vya hapa nchini na kusema kuwa viliripoti tofauti na alivyosema katika bajeti yake.


Vyombo vya habari vimepotosha na kuwachochea wananchi badala ya kuwaelimisha. Ni jambo la kushangaza vyombo vya habari vya nje vimeelezea bajeti hiyo vizuri sana…sijui uzalendo uko wapi?� alihoji Meghji na kuongeza:


“Nendeni mkasome magezeti ya nje hasa The East African. Nimezungumza na hawa vijana (waandishi wa habari), wamesema wao wanaandika habari zao vizuri, lakini zinabadilishwa na wahariri baada ya kuzituma kwao,” alisema Waziri huyo kwa jazba huku sauti ikiwa imemkauka na akishangiliwa na wabunge.


Meghji pia aliwashambulia wabunge waliosema kuwa bajeti hiyo ilikuwa ni ya marudio na kwamba haikuwa na tofauti na bajeti zilizowahi kutangazwa miaka ya nyuma. Alisema bajeti hiyo ni mpya na wala haifanani kabisa na bajeti zilizopita.


Katika hatua nyingine, Waziri Meghji alisema serikali imekubali mapendekezo ya wabunge ya kuondoa ongezeko la kodi kwa mafuta ya taa na leseni za magari zilizokuwa zimependekezwa kwenye bajeti ya mwaka huu.


Akijibu hoja mbalimbali zilizotolewa na wabunge jana, Meghji alisema Sh4 zilizokuwa zimependekezwa kuongezwa kwenye lita ya mafuta ya taa, zitahamishiwa kwenye petroli, dizeli, mafuta mazito na dizeli nzito.


Meghji alisema pia serikali imeondoa ongezeko la kodi ya leseni za magari na kwamba, hivi sasa pikipiki na bajaji zitatozwa Sh50,000 badala ya Sh80,000, magari yenye ukubwa wa zaidi ya 1,500cc Sh80,000 badala ya Sh230,00.


Alisema magari yenye ukubwa wa 2,500cc sasa watalipia leseni ya Sh150,000; yenye ukubwa wa 5,000cc itakuwa Sh330,000 na zaidi ya 5000cc ni Sh175,000 akisema hatua hiyo imezingatia ushauri na mapendekezo yaliyotolewa na wabunge.


Mjadala wa bajeti hiyo bungeni ulighubikwa zaidi na ongezeko la kodi hizo na vyombo vya habari vimekuwa vikiripori michango ya wabunge pamoja na maoni ya wananchi wa kada mbalimbali.


Meghji alisema kutokana na ongezeko la kodi kwenye mafuta, hatarajii bei mafuta kupanda kwa kiasi cha kutisha na kuagiza Mamlaka ya Kudhibiti Nishati na Maji (Ewura) na Mamlaka ya Kudhibiti vyombo vya usafiri wa majini na nchi kavu (Sumatra) kusimamia bei za walaji kutopandishwa kiholela.


Alisema kutokana na bei ya sasa kwa Dar es Salaam, lita moja ya petroli ni Sh1,275, hatazamii kuongezeka zaidi ya Sh1,400 mara baada ya kodi mpya kuanza kutozwa Julai mosi mwaka huu.


Kuhusu tuhuma za ubadhirifu dhidi ya Gavana wa Benki Kuu Tanzania (BoT), Daudi Balali, Waziri Meghji alisema serikali ina taarifa hizo, lakini hawawezi kufanyia kazi taarifa za tovuti na kwamba, vyombo vyake vinafanya uchunguzi.


Waziri Meghji alisema Ofisi ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Serikali (CAG), inakamilisha uteuzi wa kampuni kutoka nje ya nchi kwa ajili ya kuuchunguza upotevu wa fedha za madeni ya nje zinazodaiwa kulipwa kwa matapeli.


Awali, Naibu Waziri wa Fedha, Mustafa Mkullo, alisema utaratibu mpya wa kuondoa mizigo bandarini bila kufanyiwa ukaguzi ni mzuri na utasaidi Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kukusanya Sh300 bilioni ambazo imepangiwa kwa mwezi.


Tayari TRA imewabaini wafanyabiashara waadilifu 80 ambao mizigo yao haitasubiri ukaguzi ingawa nyaraka zitafanyiwa ukaguzi wa kawaida, utaratibu wa ukaguzi utafanyika baada ya kuondoa mizigo hiyo na udanganyifu ukigundulika, watachuliwa hatua kulingana na sheria,� alisema Mkullo.


Kuhusu Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kupewa ruzuku, Mkullo alisema serikali iliamua kufanya hivyo kutokana na upandaji wa mafuta kwenye soko la dunia na kwamba, bila kufanya hivyo, hali ya mgawo ingekuwa mbaya zaidi na mfumko wa bei uongezeka.


Alisemaserikali inasaidia Tanesco iweze kukopa kwa ajili ya mpango wake wa uwekezaji ambao unahitaji dola za Marekani 1.3bilioni. Mkullo pia alisema serikali imeshafanya marekebisho ya Benki ya Rasilimali (TIB) kuanza kutoa mikopo ya muda mrefu kwa kuiongezea mtaji.


Naye Abdisalaam Issa Khatib, alisema Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) inaruhusiwa kukopa kutoka kwenye mashirika ya kimataifa kulingana na itakavyokuwa inapanga miradi yake na kuongeza kuwa mwezi huu itasaini mkataba na Benki ya Dunia wa dola za Marekani 42 milioni kwa ajili ya miradi ya maendeleo.


Khatib alisema, fedha zinazoleta matatizo ni zile zinazopelekwa moja kwa moja kwenye miradi na wafadhili katika mikoa na wilaya ambazo wanashindwa kuziingiza kwenye vitabu vya serikali.


Waziri wa Mipango, Uchumi na Uwezeshaji, Dk Juma Ngasongwa, alisema kipimo cha ukuaji wa pato la taifa, kinatakiwa iwe ni fedha ya nchi husika, sio kutumia fedha ya nchi nyingine


Souce: Mwananchi

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents