Michezo

Meneja wa TRA achukua fomu ya kuwania urais TFF

Kuelekea uchaguzi mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wadau wa soka wameendelea kumimika makao makuu ya TFF kuchukua fomu ambapo mpaka sasa wapo wagombea wanne wa Urais na mmojawapo ni kigogo kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Shija Richard.

Shija Richard

Shija ambaye ni Meneja ndani ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), amechukua fomu hiyo leo Jumatatu katika ofisi za TFF Uwanja wa Karume, Dar es Salaam, ingawa hakuzungumza lolote kwa maelezo kuwa muda wa kampeni bado.

Mgombea huyo ana Shahada ya Uzamili katika masuala ya Sheria za kodi na utawala kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, pia ana Stashahada ya Uzamili ya Usimamizi wa Fedha kutoka Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) Dar es Salaam na Stashahada ya Juu ya Uhasibu kutoka Chuo Kikuu cha Uhasibu Arusha (IAA).

Pia Shija amehudhuria mafunzo mbalimbali ya uandishi wa habari na ameshawahi kuandikia magazeti mbalimbali hapa nchini kuanzia mwaka 1997.

Mgombea huyo aliwahi kuitumikia Taasisi ya Kuzuia na Kupambaana na Rushwa (TAKUKURU) kabla ya kujiunga na Mamlaka ya Mapato Tanzania. Kwa sasa ni Mhazini Mkuu wa Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo nchini (TASWA), akiwa pia amepata kuongoza klabu mbalimbali za mpira wa miguu kwa ngazi tofauti.

Wadau wengine waliojitokeza ni Ally Mayay, Jamal Malinzi, Imani Madega, Wallace Karia, Fredrick Masolwa na Athuman Nyamlan.

By Godfrey Mgallah

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents