Mfahamu CAG mpya aliyeteuliwa na Rais Magufuli na orodha ya waliowahi kuteuliwa mwanzo- Video

Mfahamu CAG mpya aliyeteuliwa na Rais Magufuli na orodha ya waliowahi kuteuliwa mwanzo- Video

Rais wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli amemteua Charles Kichere kuwa Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali(CAG). na tayari ameshaapishwa na Rais magufuli mapema hivi leo Ikulu jijini Dar Es Salaam. Kichere anaichukua nafasi ya Profesa Assad Mussa, mkaguzi anayeondoka kufuatia kumalizika kwa muda wake wa uhudumu hapo kesho tarehe 4 Novemba.

Kabla ya wadhifa huu mpya, Kichere alikuwa katibu tawala wa Mkoa wa Njombe nchini.Nafasi ya Kichere itachukuliwa na Katarina Revocati ambaye kabla ya wadhifa huu mpya alikuwa Msajili Mkuu wa Mahakama.

Charles Kichere ni nani?

Alisomea elimu ya juu katika Chuo Kikuu cha Dar-Es-Salaam na chuo kikuu cha Tumaini, mjini Dar Es Salaam.

Kichere aliwahi kuwa naibu kamishna mkuu wa TRA.

Mnamo tarehe 25 Machi mwaka 2017, aliteuliwa na rais Magufuli kuwa kamishna mkuu wa mamlaka ya mapato Tanzania (TRA).

Aliipokea nafasi hiyo kutoka kwa Alphayo Kidata ambaye aliteuliwa wakati huo kuwa katibu mkuu ikulu Tanzania.

Charles Kichere alihudumu kama kamishna wa TRA kuanzia Machi 2017 hadi Juni mwaka huu 2019, wakati aliondoshwa katika mamlaka hiyo ya TRA, katika mageuzi ya rais Magufuli aliyotoa ikulu mjini Dar es Salaam kupitia taarifa rasmi ya mkurugenzi wa mawasiliano ya rais.

Kichere aliteuliwa badala yake kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Njombe.

Yuko kwenye bodi ya Benki ya CRDB Tanzania.

Zamani alikuwa mkaguzi mkuu wa shirika la Kitaifa la barabara, mweka hazina na pia mkaguzi mkuu wa hesabu katika kampuni ya majani chai ya Unilever nchini Kenya na Tanzania.

Amepokea wadhifa wa mkaguzi na mdhibiti wa hesabu za serikali kutoka wa Profesa Mussa Assad.

Ripoti ya CAG: Yabainisha hali mbaya ya kifedha kwa mashirika ya umma

Orodha ya wadhibiti na wakaguzi wa hesabu za serikali Tanzania

  • Bwana. R.W.A. McColl aliyehudumu 1961 hadi 1963
  • Bwana. Gordon. A. Hutchinson aliyehudumu 1964 hadi 1969
  • Bwana. Mohamed Aboud aliyehudumu 1969 hadi 1996
  • Bwana. Thomas Kiama aliyehudumu 1996 hadi 2005
  • Mr. Ludovick S. L. Utouh aliyehudumu 2006 hadi 2014
  • Prof. Mussa Juma Assad aliyehudumu 2014 hadi 2019
Spika Job Ndugai aliagiza CAG ahojiwe mwezi Januari akidai kuwa amelidharau BungeHaki miliki ya pichaBUNGE TZ
Image captionSpika Job Ndugai aliagiza CAG Assad ahojiwe mwezi Januari akidai kuwa amelidharau Bunge

Bunge lakataa kufanya kazi na (CAG) Assad

Bunge la Tanzania halikuvutiwa na kauli ya CAG Profesa Musa Assad wakati katika mahojiano na Idhaa ya Kiswahili ya redio ya Umoja wa Mataifa (UN) jijini New York mwezi Disemba 2018, alisema kuwa Bunge hilo la Tanzania halina meno na hivyo limeshindwa kuiwajibisha ipasavyo serikali.

Mvutano mkali ulizuka baina yake na Bunge la taifa kufuatia kauli yake hiyo.

Mnamo Aprili mwaka huu Bunge la Tanzania liliazimia kutofanya kazi na CAG huyo anayeondoka Prof Musa Assad, baada ya kumtia hatiani kwa tuhuma za kukidharau chombo hicho cha taifa.

Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai alionyesha wazi kukerwa kwa namna ambavyo Assad hakujutia kauli yake iliodaiwa kuwa ya dharau dhidi ya Bunge la Tanzania.

”Tatizo letu ni maneno ambayo Profesa Musa Juma Assad aliyasema kule Marekani, na majuzi alipowaita waandishi wa habari Dodoma akarudia tena kwamba ataendelea kuyasema maneno hayo. Maneno yale sisi tumeyakataa kuwa si maneno ya kistaarabu hilo ndio tatizo, na sio taarifa iliyotolewa.” Alisema Ndugai.

Mvutano wa CAG na Bunge Tanzania

Hatahivyo sio wote waliokuwa na msimamo huo.

Muungano wa vyama nane vya upinzani nchini Tanzania, (Chadema, ACT-Wazalendo, NCCR-Mageuzi, NLD, DP, UPDP, CHAUMMA na CCK) vilivyodai kuwa

kama kuna anayetakiwa kijiuzulu kwenye sakata hilo ni Spika Ndugai na sio Assad.

Katika kuzungumzia mgogoro huo, Prof Assad alisema: “Tafsiri ya kuwa (Bunge) hatuwezi kufanya kazi na CAG ni tafsiri pana sana na inatakiwa tuijue vizuri.”

Kadhalika Assad alieleza kuwa ataendelea kutekeleza majukumu yake kama ilivyoainishwa kwa mujibu wa katiba Tanzania.

Prof Assad amemaliza awamu ya kwanza ya miaka 5.

Muda wake unakwisha rasmi kesho tarehe 4 Novemba 2019.

Kwa mujibu wa sheria ya mwaka 2008 ya Ukaguzi wa Hesabu za Umma, Rais alikuwa na mamlaka ya kumteua tena lakini ameamua kumteua mwengine.

By Ally Juma.

 

Related Articles

Back to top button
Close
Bongo5

FREE
VIEW