Habari

Mfahamu fundi aliyetengeneza gereji inayotembea, Tunduma wanamuita ‘Street Engineer’

Adam Zakaria Kinyekire anajulikana zaidi kwa jina la ‘Street Engineer’, yeye ni fundi mekanika kutoka Wilaya ya Tunduma, Mkoa wa Songwe, nyanda za juu kusini mwa Tanzania.

Adam amewasaidia vijana wengi kwa ajira

Alijifunza kazi hiyo mwenyewe bila kuhudhuria chuo chochote, lakini ni maarufu kwa kuunda helikopta na pia huwafaa madereva kwa gereji inayotembea.

Kwa mujibu wa Shirika la habari la BBC, Adam anasema yeye ni mbunifu ambaye hakupata ujuzi wowote kutoka shuleni maana mara baada ya kumaliza shule ya msingi, alianza kujifunza kutengeneza magari katika karakana ya kawaida na baadaye akaanza kuunda vitu kama vile mashine ya kusagia nafaka, gari la karakana na hata helikopta.

Gereji

“Ubunifu wa kutengeneza vitu mbalimbali huwa sifundishwi na mtu ni kitu tu ambacho kipo kwenye damu, ni kama vile ndoto tu ambapo vitu vinakuja kwenye akili kwamba naweza kutengeneza hiki na hiki lakini sijawahi kupata mafunzo popote,” Adam Zakaria anaeleza.

Kwa sasa anafanya kazi na vijana takribani 40 na wengine zaidi ya 500 walipita katika mikono yake kupata mafunzo.

Gereji

Kwa nini Adam aliamua kutengeneza gereji linaloweza kusafiri?

Sababu iliyompelekea kutengeneza gari la aina hiyo ni baada ya kubaini kwamba kuna wakati watu wanakosa huduma wakiwa mbali ndio maana akaamua kutengeneza mashine ambayo inatembea.

“Watu wengi huwa wanaharibikiwa na magari yao katika maeneo ambayo hakuna msaada.”

Gari hili lina vitendea kazi vyote vya ufundi, mfumo wa umeme na huduma ya kwanza yaani kila kitu kinachopatikana kwenye garage kipo katika gari hili.

Wateja wangu wengi ni Watanzania ambao wana magari makubwa ya mizigo yanayoelekea au yanayotoka Zambia.

Zambia ina pori kubwa hivyo wakikwama inawawia vigumu kutengeneza.

“Kila siku magari yanakatika hivyo unaweza kukuta naenda mara mbili kwa wiki au mara nne kwa mwezi ila lazima niende”, Adam aeleza.

Gari hili ambalo hulitumia kama gereji la kuhama hama, alilitengeneza kwa muda wa mwaka mmoja na sasa liko barabarani ni miaka saba, na anasema gari hilo lina manufaa makubwa sana sio kwake tu bali hata vijana ambao wanafanya nao kazi.

“Hii mashine inajitengeneza yenyewe na tunaweza kulipa ada za watoto shuleni,” anasema Adam.

Hata hivyo bado anakabiliwa na changamoto ya kibali cha gari hilo ingawa anashukuru kuwa nchini Zambia huwa hawamsumbui kwa sababu limeunganishwa na gari jingine lenye namba ya usajili.

Gereji

Gari linasafiri mpaka kilomita 600 kwenda kufuata magari yaliyoharibika nchini Zambia, mteja hulipa gharama ya huduma yake kulingana na kazi na eneo.

Na huwa anafuata utaratibu wote wa kujaza vibali ili kuingia nchi ya pili kufanya kazi yake.

“Ubunifu wangu unatokana na fikra zangu”.

“Niliwaza kuanzisha gereji la namna hii baada ya siku moja kunusurika na ajali baada ya kukutana na gari barabarani limeziba njia,”Adam alisimulia.

Licha ya gari hili Street Engineer amejifunza kutengeneza vifaa vingine.

Magari kuharibika njiani ni dharura na ni kawaida kwa binadamu, huwa inatokea kwa bahati mbaya hata kama madereva wamejiandaa.

Issa Hamza Abdala ni dereva wa magari makubwa, na anasema kuwa aliwahi kumuita fundi huyo mara mbili wakati lake gari lilipokatika chesesi.

“Licha ya kuwa huwa tunatembea na vifaa vyetu lakini gari likikatika inabidi uombe msaada.

“Mafundi wa Zambia na Watanzania ni tofauti, magari mengi sana huwa yanamtumia.

“Kuna wakati nilimkuta hata Matumbo huko, zaidi ya kilomita 15 kutoka Tunduma .

“Ni rahisi kwetu kumtumia fundi ambaye tunamfahamu, ila ubora wa kazi yake pia ndio sababu kubwa ya kuamini kazi yake”, alisisitiza dereva.

Ernest Chikoti anashukuru kwa uwepo kwa huduma hii ya Adam.

“Namba yake kaisambaza na ana vifaa vyote basi unaweza kumpigia simu na kumtumia picha katika whatsapp aone tatizo lililokupata na inakuwa rahisi kumpata na kututengenezea.

Nilimfahamu Street Engineer kwa kuambiwa na watu kuwa kuna fundi ambaye alishawahi kutengeneza helikopta ndio anaweza kutengeneza magari vizuri.

Huyu mtu ameamua kubuni yeye kama yeye lakini ni vyema kwa serikali kuwawezesha wengine wabuni vitu kama hivi licha ya kuwa huyu hakuwezeshwa lakini tunahitaji huduma hii zaidi,” Ernest alisisitiza.

Gereji

Adam Kinyekire ni miongoni mwa Watanzania ambao wamo kwenye historia ya kutengeneza ndege aina ya helikopta.

Adam aliiambia BBC kuwa alifanikiwa kutengeneza ndege hata kabla ya kuiona ndege aina hiyo katika maisha yake yote.

Ilimchukua kipindi cha miezi sita mpaka mwaka kuikamilisha ndege hiyo.

Lakini ndoto yake iliishia patupu baada ya serikali kumpiga marufuku.

Wataalam wa masuala ya anga, wanasema kuwa kuna utaratibu katika kila jambo na wabunifu wanapaswa kutambua kanuni na sheria zilizopo.

“Wazo hilo lilinijia baada ya kuona nimetengeneza gereji linalotembea na kuona kuna umuhimu wa kuanza kupambanua akili kwa kubuni jambo jingine ambalo lingeweza kuwa na manufaa kwangu,” Adam anasema.

Hata hivyo shauku yake hiyo ya kuona ndege ikiruka katika runinga ilimpa hamasa ya kutengeneza ndege iweze kuruka kama nyingine zinavyoruka.

“Nilianza kwa kuangalia ni kitu gani kinachosababisha ndege iruke na kubaini kuwa ni nguvu ya upepo ambayo ikitengenezwa itakuwa na uwezo wa kuinua ndege.

Ndege yangu nimeitengeneza kwa vifaa vya magari na mpaka sasa inaweza kuruka lakini utaalamu wa kuifanya itue bado.

Ingawa nilipata hofu sana baada ya tangazo la gazeti kutoka likitoa onyo kwa watengenezaji wa ndege na nilikata tamaa pia lakini sasa nina nguvu ya kuanzisha vitu vingine pia,” Adam aeleza.

Pamoja na jitihada nyingi ambazo amezitumia kutengeneza ndege hiyo ambayo haikuwa na manufaa, Adam anashukuru kwamba chuo cha sayansi na teknolojia kiliona jitihada zake na kumuwezesha kwenda kuona ndege kwa macho yake na kumpa mafunzo ya kutengeneza mashine ambazo zitanufaisha jamii na yeye mwenyewe.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents