Habari

Mfahamu Kipepeo dume anayegombewa na majike kwa uzuri wake, yadaiwa aingiza mapato mengi Pwani ya Kenya

Je, una habari vipepeo ni kitega uchumi? Baadhi ya wakaazi wa kaunti ya Kilifi pwani ya Kenya kwa muda mrefu sasa wamejikidhi kimaisha kupitia biashara hiyo ya vipepeo.

Makavasi ya Gede ndilo soko kubwa la wafanya biashara hao wa vipepeo

Kulingana na mfanya biashara mzoefu Charo Ngumbao wao zaidi hushika vipepeo wa kike lakini kuna kipepeo wa kiume ambaye anasema huwapa mapato mazuri sana.

Mbali na mapato, kipepeo huyo ni kipenzi cha wale wa kike ambao humtamani na kumfuata kwa wingi kutokana na uzuri wake na madaha aliyo nayo.

Kipepeo huyo mwanamume ni aina ya pupilio derdnus. Ngumbao anasema kipepeo huyo huwapatia kipato cha juu zaidi katika biashara yao.

“Huyo kipepeo tunamuita dhahabu ya Arabuko ambaye ni pupilio derdnus wa kiume. Ana maringo mno mpaka wanawake hupigana kumpata awazalishe. Anapepea kwa madaha maanake anajua yeye ndiye dume anayependwa zaidi na vipepeo wa kike katika msitu wa Arabuko Sokoke, na sokoni zile pupa zake zinang’ang’aniwa sana, waeza kupata dola mbili na nusu ama tatu kwenda juu,” anasema Ngumbao ambaye amejehusisha na biashara ya vipepeo kwa zaidi ya miaka ishirini sasa.

”Aina ya vipepeo wengine wa kike ambao hutufaa kibiashara ni pupilio nirius, chraxes protoclea na pupilio constatinus. Maisha ya vipepeo ni wiki nne ndio maana tunawapeleka sokoni kila wiki kwa sababu ya mda mfupi wa maisha ya vipepeo.”

Ngumbao anaeleza jinsi biashara hii imebadilisha maisha yake.“ Ukweli ni kwamba ni biashara nzuri sana, watoto wangu wamesoma na ni biashara ambayo haina hasara kubwa kuindeleza. Nilikua muharibifu wa msitu kwa ukataji wa miti lakini nilipoanza biashara hii nimeona mabadiliko makubwa. Napata kati ya shilingi za Kenya elfu ishirini hadi arobaini kwa mwezi. Kuna wengine hata wamenunua mashamba kwa mapato haya ya vipepeo.Mfanyabiashara wa vipepeo Kilifi Charo Ngumbao anasema biashara hii imewasaidia sana kuwaingizia kipato na kuweza kuyakidhi maisha yao

Mfanyabiashara wa vipepeo Kilifi Charo Ngumbao anasema biashara hii imewasaidia sana kuwaingizia kipato na kuweza kuyakidhi maisha yao

”Tuna njia mbili za kushika hawa vipepeo, kwanza kuna ile ya mtego na nyingine ya neti. Katika hiyo ya mtego, tunaweka tembo la mnazi tumechanganya na ndizi. Waeza nasa vipepeo kama hamsini, wakulima tunachagua wale unawahitaji. Zaidi huwa tunaangalia wale wa kike kisha hao wengine tunawarudisha waendelee kuzaana. Tunawapeleka nyumbani tunawaweka kwenye banda zao tumejenga wanaendelea kuzaa halafu tunapeleka sokoni kuuza zile pupa.”

Makavasi ya Gede ndilo soko kubwa la wafanya biashara hao wa vipepeo.

Naibu msimamizi wa makavazi hayo Mathias Ngonyo anatusimulia zaidi:“ Hapa huwa wakulima wanaleta pupa ama vizeruzeru. Wana viongozi wao huleta hizo pupa. Kwanza tunavikagua tuone kwamba viko hali nzuri kisha tunaziweka kwa maboxi halafu tunazipeleka uwanja wa ndege kusafirishwa kwa wateja wetu huko Uingereza na Uturuki ambazo ndizo soko zetu kubwa.”nyumba ya vipepeo

Miongoni mwa wanabiashara waliozungumza na BBC wanasema biashara hiyo imewasaidia sana.

”Kama si hii biashara ya vipepeo sidhani ningeweza kusomesha watoto wangu na kujenga nyumba,” anasema Msanzu Karisa.

Naye Asha Ali Omar amesema kuwa biashara ya vipepo ina manufaa makubwa.

“Hii ni biashara kwanza inatusaidia kuhifadhi msitu wa Arabuko Sokoke. Nina watoto wanne na wote nimewasomesha kwa uuzaji wa vipepeo maanake si biashara ngumu. Waeza ifanya huku ukiendelea na kazi zako zingine,” anasema Asha..

Mbali na uuzaji wa vipepeo, kuna sehemu hapo katika makavazi ya Gede utapata vipepeo wa kila aina ambao naibu msimamizi Mathias Ngonye anasema wanatumia kama kivutio cha watalii.

”Watalii huja hapa kutizama hawa vipepeo lakini wanalipa. Mwisho wa mwaka hayo mapato tunayagawa kwa wafanya biashara wa vipepeo,” anasema Ngonye.

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents