Fahamu

Mfahamu mtu mwenye uwezo wa kukokotoa hesabu kwa kasi zaidi duniani

Unaweza kusema kasi ya kufanya hesabu ya Neelakantha Bhanu Prakash ni sawa na kasi ya mkimbiaji Usain Bolt. Akiwa na umri wa miaka 20, aliishindia India medali ya kwanza ya dhahabu na kuwa bingwa kwa kufanya hesabu kwa akili duniani.

Anasema hesabu ndio mchezo mzuri wa kuchangamsha ubongo lengo lake likiwa ni kuondoa hofu ya kufanya hesabu.

Bhanu kama anavyofahamika – kila wakati huwa anafikiria nambari na sasa hivi ndio mwanadamu mwenye kufanya hesabu kwa kasi ya juu zaidi duniani yaani kikokotoo mwanadamu kama wanavyomtambua wenyewe.

Analinganisha kufanya hesabu kwa akili sawa na kasi ya wanaokimbia.

“Tunasherehekea mtu kama Usain Bolt anapokimbia mbio za mita 100 kwa sekunde 9.8,” ameiambia BBC Radio 1 Newsbeat, “lakini hatusemi umuhimu wa kukimbia kwa kasi ya juu duniani sawa na magari na ndege.”

“Ni kuhusu kuhamasisha watu kwamba mwili wako unaweza kufanya kitu kisichoweza kufikirika – ni sawa kufanya hesabu.”

‘Inafanya ubongo wako kuwa na kazi ya kufanya kila wakati ‘

Unaweza kufikiria alizaliwa akiwa na kipawa cha kufanya hesabu lakini sio hivyo kwa Bhanu.

Alipokuwa na miaka mitano alikuwa mgonjwa sana kiasi cha kuwa kitandani kwasababu ya jeraha la kichwa kwa mwaka mmoja na huo ukawa uvumbuzi wa safari yake ya kufanya hesabu.

“Wazazi wangu waliambiwa kwamba majeraha yangu yangeathiri uwezo wangu wa akili wa kufikiri.

“Na mkombozi wangu akawa ni kufanyakazi kwa akili niweze kujinusuru ili ubongo wangu upate kazi ya kufanya kila wakati.”

Bhanu amekuwa akuwasaidia watu katika maeneo ya vijijini kupenda hesabu wakati wa marufuku ya kutotoka nje

Anasema kutoka kwa familia ya kipato cha kati nchini India, lengo kawaida huwa ni kupata kazi nzuri au kufungua biashara na wala sio kuingia kwenye nyanja kama ya hesabu.

Lakini kwasababu ya uelewa wake katika hilo, sasa hivi Bhanu anakaribia kumaliza shahada yake ya hesabu.

‘Mchezo mzuri wa kuchangamsha ubongo’

Kama washindani wengine wa ngazi ya juu, Bhanu anasema mafanikio yake yametokana na kazi nzuri anayofanya.

Sio rahisi kama kuketi tu kwenye dawati, badala yake, anachukulia hesabu kama”mchezo mzuri tu wa kuchangamsha bongo”.

“Nimejifunza sio tu kuwa na kasi ya juu ya kufanya hesabu lakini pia ni mfikiriaji wa haraka.”

Akiwa na umri mdogo, Bhanu alikuwa akifanya mazoezi ya hesabu kwa saa sita hadi saba kwa siku mbali na kuingia darasani.

Lakini tangu alipokuwa mshindi wa tuzo ya ubingwa na nyinginezo, amepunguza muda wa kufanya mazoezi kwa siku.

Badala yake, anategemea “mazoezi ambayo si rasmi ambapo kila wakati huwa nafikiria kuhusu namba tu”.

“Huwa nafanya mazoezi ya hesabu kwa kusikiliza muziki, nikiwa nazungumza na watu na wakati ninacheza kriketi, kwasababu hapo ndio ubongo hufunzwa kufanya mambo kadhaa kwa wakati mmoja.”

Anaonesha weledi wake katika hilo kwa kukariri hesabu ya kuzidisha namba 48 katikati ya mahojiano haya aliofanyiwa na BBC.

“Nitaongeza kila nambari ya taxi inayopita mbele yangu. Wakati ninazungumza na mtu nitahesabu ni mara ngapi amepepesa macho – licha ya kwamba inasikika kuwa jambo lisilowezekana – inafanya akili yako iendelee kufanya kazi.

‘Inahusu kuwatia wengine moyo’

Kwa Bhanu, lengo lake sio tu kuvunja rekodi – ingawa pia anapenda kufanya hivyo.

“Kuvunja rekodi na weledi wake wa kufanya hesabu ni sitiari tu kusema kwamba dunia inahitaji ambao ni weledi wa hesabu. Na hesabu inastahili kuwa kitu cha kufurahia kwetu na kusema kwamba hili ni somo tunalolipenda.”

Lengo lake la mwisho ni kuondoa hofu ya hesabu, na anasema watu wengi wana hofu ya kufanya hesabu.

“Kuwa na hofu ya kufanya hesabu kuna washawishi kufuata taaluma walizonazo lakini sio hesabu.”

Anasema kwamba ambao ni weledi wa hesabu wanafahamika kwa kuwa “wapole na wajinga”, lakini kushindana katika ngazi ya kimataifa kunamaanisha kwamba ana jukumu la kutukuza hesabu kama kitu cha kufurahiwa.

Kwa mujibu wa BBC. Akiwa na tuzo za dunia nne na mafanikio mengine chungu nzima, familia ya Bhanu bila shaka inajionea fahari kubwa.

Anapongeza familia yake kwa kumtia moyo na kuhakikisha anakuwa na msingi imara wa kufanya hesabu.

“Baada ya kushinda tuzo yangu ya kwanza kimataifa, mjomba wangu alinishauri niwe na kasi kuliko mwingine yeyote duniani.

“Wala sikuwahi kufikiria kwamba ninaweza kuwa kikokotoo mwanadamu mwenye kasi ya juu zaidi ya kufanya hesabu.”

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents