Mganga atumia wembe mmoja kuchanja wananchi…

Katika hali isiyokuwa ya kawaida, wananchi wa Kitongoji cha Igunguli, Kata ya Fufu, Wilaya ya Chamwino, wamechangishwa kwa nguvu kila mmoja Sh. 1,500, ili kugangwa dhidi ya wachawi

Na Mary Edward, PST, Mtera



 


Katika hali isiyokuwa ya kawaida, wananchi wa Kitongoji cha Igunguli, Kata ya Fufu, Wilaya ya Chamwino, wamechangishwa kwa nguvu kila mmoja Sh. 1,500, ili kugangwa dhidi ya wachawi.

Mganga `anayewagangua` alitafutwa na viongozi wa kitongoji hicho, kwa ajili ya kuwaondolea nuksi na kusafisha wachawi, ambapo amedaiwa kutumia wembe mmoja kuchanja msululu wa wananchi kichwani na kwenye makalio.

Wakizungumza na PST, baadhi ya wananchi, walisema viongozi wao, Bw. Yahaya Njalamoto ambaye ni Mwenyekiti na Katibu wake, Ngage Msangi wakishirikiana na Diwani wa Kata hiyo, Bw. Meshaki Songo, waliitisha mkutano wa kijiji na kuwataka wananchi watoe michango hiyo.

Inadaiwa kwamba hatua hiyo ilikuja kufuatia malalamiko kuwa vitendo vya ushirikina vimekithiri katika kijiji hicho na kusababisha biashara zao za samaki kiwaendea kombo.

Walisema kuwa, baada ya mkutano huo wananchi walichanga jumla ya Sh. 470,000 na kumpatia mganga huyo ambaye alianza kazi ya kuwapatia chanjo wananchi hao, ili kuwaondolea mikosi na kuwakinga na vitendo vya ushirikina.

Hata hivyo, wananachi hao walisema, kinachowatia hofu ni kitendo cha mganga `wao` kuwachanja sehemu za kichwani kwa ishara ya msalaba na kwenye makalio, huku akitumia wembe mmoja.

“Mimi nilichanjwa sehemu za kichwani na kwenye makalio,“ alisema mwananchi aliyejitambulisha kwa jina moja la Chamunga huku akionyesha sehemu hizo bila woga na kuongeza: “Baada ya hapo alitunywesha dawa ambayo ilikuwa chungu sana.“

Baadhi ya wananchi waliokataa kushiriki katika tukio hilo, waliieleza PST kuwa, wamekuwa wakitishiwa maisha na mganga huyo na viongozi wa kitongoji hicho wakidaiwa kuwa wao ndio wachawi.

“Walituambia kama hatutatoa michango na kushiriki katika tukio hilo, tuhame katika kijiji hiki, la sivyo tutachomewa nyumba zetu na au kupoteza maisha,“ alisema Joshua Mbowela mmoja wa wananchi 30 waliokataa kutoa michango na kushiriki katika tukio hilo.

Mganga huyo aliyefahamika kwa jina moja la Shaibu, anayedaiwa kutokea katika Kijiji cha Lifua, Wilaya ya Ludewa, alikuwa akifanya shughuli zake hizo za `kugangua` uchawi kwenye Ofisi ya Chama cha Mapinduzi ya kitongoji hicho.

Hata hivyo, Diwani, Bw. Songo alipohojiwa kuhusiana na suala hilo, alikiri kuhusika na kusema kuwa, kwa upande wake haoni kama kuna kosa, kwa vile waliohitaji �huduma hiyo ya mganga ni wananchi wenyewe.

“Wananchi ndio waliotaka tuwaletee mganga wakidai kuwa hapa kijijini kuna uchawi unaowafanya washindwe kufanya biashara zao za samaki vizuri,“ alisema.

Alisema yeye alipewa taarifa na viongozi wa vijiji baada ya kufanya mkutano wake na yeye hakuwa na pingamizi kwa hilo kwa vile walioamua kufanya hivyo ni wananchi na viongozi wao.

Mganga huyo anadaiwa alishapita kwenye vijiji vya Chungu, Loje, Wanja, Chimendeli na Stafu akiendelea kuwatapeli watu kwa njia ya kuwaondolea mikosi.

Taarifa kutoka kwa wananchi hao zinadai kuwa, baada ya kutoka katika kijiji hicho, mganga huyo alinunua pikipiki kutokana na mapato aliyoyakusanya katika vijiji alivyopita.


 


Source: Nipashe

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents