Habari

Mgodi wa Bulyanhulu wapunguza wafanyakazi

Ilikuwa kama tetesi, lakini sasa imebainika kuwa ni kweli.Mgodi wa Dhahabu wa Bulyanhulu unaomilikiwa na Kampuni ya Acacia umepunguza wafanyakazi 2,000 kutokana na mgodi kupunguza uzalishaji.

Hatua hiyo inatokana na mgodi huo kuingia mgogoro na Serikali baada ya kuzuiwa kusafirisha makinikia kwenda nje ya nchi.

Meneja Mkuu wa Mawasiliano wa Kampuni ya Acacia, Asa Mwaipopo alisema hayo juzi wakati wa hafla ya kuwaaga wafanyakazi hao waliopunguzwa.

Mwaipopo alisema kati ya wafanyakazi 2,000 waliopunguzwa, 1,200 ni waajiriwa wa Bulyanhulu na 800 ni kutoka kwenye kampuni zenye zabuni zinazofanya kazi katika mgodi huo.

Alisema kutokana na zuio la Serikali la kusafirisha mchanga wa dhahabu (makinikia) nje ya nchi, mgodi huo umebadili mfumo wa utendaji kwa kuanzisha mtambo mpya utakaochenjua mabaki ya awali kwa kutumia kemikali ya Cyanide.

Meneja huyo alisema njia hiyo imeelezwa itatoa kiwango kidogo cha dhahabu, tofauti na uchimbaji wa awali wa mtambo mkubwa uliokuwa ukizalisha makinikia yenye dhahabu nyingi zaidi.

Hata hivyo, Acacia iliwahi kueleza kuwa kiwango cha dhahabu kinachobaki kwenye makinikia ni kidogo.

Mwaipopo alisema katika mfumo mpya wa mtambo wa uzalishaji kwa kutumia kemikali hiyo, wataajiri upya wafanyakazi 150 wa kampuni na wengine 150 kutoka kwenye kampuni zenye zabuni ambao watakuwa wakifanya usafi, ulinzi na huduma ya chakula.

Alisema mtambo mkubwa uliokuwa ukitumika kwa uzalishaji umekamilisha kazi Jumamosi, hivyo kufikia mwisho wa uzalishaji makinikia katika mgodi huo.

Mwaipopo alisema licha ya mgodi kupunguza uzalishaji na wafanyakazi, lakini ulipaji wa ushuru wa huduma kwa halmashauri na kodi za Serikali utaendelea ingawa kwa kiwango kidogo.

Kuhusu wafanyakazi waliopunguzwa, Mwaipopo alisema licha ya kuagana nao wamewapa mafunzo ya ujasiriamali na kuwaandaa kisaikolojia kwa kuwafundisha namna ya kuishi maisha mbadala tofauti na waliyokuwa nayo wakati wa ajira.

Chanzo: Mwananchi

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents