Habari

Mgombea wa urais aomba kila Mtanzania kuwachangia Sh 100

Mgomea urais kwa tiketi ya Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, amesema vyama vya upinzani vinakabiliwa na hali ngumu kiuchumi na vinafanya kampeni kwa shida.

Akihojiwa katika kipindi cha ‘Dakika 45’ cha ITV kilichorushwa usiku wa kuamkia leo, Profesa Lipumba alisema vyama vinaomba michango kutoka kwa wanachama na wananchi wengine ili kufanya kampeni nchi nzima.

Alisema inabidi kutafuta misaada kutoka kwa wanachama ili kusaidia kufanya kampeni na kwamba chama chake kinaomba Watanzania kukichangia walau Sh. 100 kwa kila mwananchi.

“Kwanza, hali ya uchumi ya Watanzania kwa ujumla ni mbaya, hali ya fedha, agenda ya vyuma vimekaza ni kweli, wafanyabiashara wamekuwa na wasiwasi kwamba wakifanya hivyo (kutoa mchango kwa vyama vya upinzani) inaweza kuwaletea matatizo,” alisema.

“Tunarudi kwa Watanzania kutaka kuleta mabadiliko, tunahitaji kuleta mabadiliko kwa sababu hali ya maisha ni ngumu, tumetoa wito kila Mtanzania ajiwekee Sh.100 kwa siku 50 hadi 60 watatuchangie Sh. 6,000.

“Ikiwa nusu milioni watatuchangia, tupata jumla Sh. bilioni tatu, zitatutosha kufanya kampeni nchi nzima. Hata akiwa na hali ya maisha ngumu, akituchangia Sh. 100 haiwezi kuongeza ugumu wa maisha alionao.

“Kuna wafanyabiashara watuchangie, kwa kuwa chama chetu kinaandaa mazingira mazuri ya biashara na uwekezaji, alipe kodi kwa amani na mazingira mazuri ya biashara,” aliomba.

Profesa Lipumba pia alisema anawania urais kwa kuwa Tanzania ina rasilimali, lugha ya Kiswahili inaunganisha wananchi na hakuna matatizo ya udini na ukabila.

“Tunapaswa kuwa taifa lililopiga hatua, lakini la kusikitisha hadi sasa Watanzania walio wengi ni maskini wa kutupwa. CUF sera yetu ya msingi ni haki sawa na furaha kwa wote,” alitamba.

Alipoulizwa kuhusu hoja ya kuwa yeye siyo mpinzani halisi, Profesa Lipumba alitamba kuwa yeye ndiye mpinzani pekee anayeihoji serikali bila woga, huku akitaka wananchi kupuuza propaganda zilizopo dhidi yake.

Alisema CUF ikishika madaraka ya kuongoza nchi, itawekeza kwenye kilimo ili kuleta mapinduzi ya viwanda ambavyo vitatoa ajira kwa wananchi wengi.

“Katika kila Sh. 100 iliyotumia na serikali fedha iliyokwenda kwenye kilimo ni Sh. tatu, huwezi kuleta mapinduzi ya kilimo kama huwekezi kwenye kilimo. Sisi tutaleta mabadiliko,” alitamba.

“Kaulimbiu yetu ni haki sawa na fursa kwa wote. Nikichaguliwa kuwa rais, nitaunda serikali ya umoja wa kitaifa ili kukamilisha katiba ya demokrasia yenye misingi ya kweli ambayo itakuwa dira ya nchi.

Profesa Lipumba alisema serikali ya umoja wa kitaifa wanayokusudia kuiunda, itasimamia haki za kisiasa, kiuchumi na kijamii, mambo yanayokwenda sambamba na Malengo Endelevu ya Milenia (SDGs).

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents