Habari

Mh. Kangi Lugola atoa agizo kwa Duwasa

Naibu Waziri Ofisi ya Makamu Rais Mazingira, Kangi Lugola ameiagiza Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka Dodoma (DUWASA) kutoa elimu kwa wananchi wanaozunguka maeneo ya mabwawa yanayohifadhi maji taka kutoyatumia maji hayo kwa kilimo au matumizi yoyote ya nyumbani.

Lugola ametoa agizo hilo leo, mjini Dodoma alipofanya ziara katika mabwawa yanayohifadhi maji taka yaliyopo maeneo ya Swaswa, ambapo wananchi wa maeneo hayo wameonekana wakiyatumia maji hayo katika kilimo na wengine kwa ajili ya matumizi mbalimbali ya nyumbani.

“Mnapofungulia maji taka kutoka katika mabwawa hakikisheni mnaweka ulinzi wa kutosha ili maji taka hayo yasielekezwe kwenye mashamba na makazi ya watu,” alisema Lugola.

Aidha amemtaka Mkurugenzi Mkuu wa DUWASA kuhakikisha kuwa ana kibali cha kutiririsha maji taka kutoka bonde la mto Wami-Ruvu, vile vile maji hayo yawe yametibiwa na kutiririshwa kwa kiwango kinachotakiwa.

Pia ameitaka Mamlaka hiyo kuhakikisha mabwawa mawili ambayo hayatumiki kuhifadhi maji taka yanafufuliwa na kutumika kufikia tarehe 31/12/2018 ili kukidhi idadi ya watu inayoongezeka mkoani Dodoma kutokana na Makao Makuu ya Nchi kuhamia mkoani humo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa DUWASA Mhandisi David Pallangyo amesema ameyapokea maagizo ya naibu waziri huyo, ikiwa ni pamoja na kuyafufua mabwawa mawili ambayo yalikuwa hayatumiki ili kukidhi ongezeko la watu mkoani humo.

Hata hivyo amesema, mamlaka hiyo ipo katika mpango wa kujenga mabwawa ya kisasa katika eneo la Nzuguni ambalo litakidhi na kuendana na ongezeko la watu katika mkoa wa Dodoma.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents