Siasa

Miaka miwili ya JK Ikulu Utendaji wa mawaziri waanikwa

WAKATI Serikali ya Rais Jakaya Kikwete, ikitimiza miaka miwili siku tano zijazo, hali ya mambo inazidi kuwaelemea mawaziri wake wengi na sasa uchunguzi wa kina wa Majira Jumapili, umezidi kuonesha ni kwa nini imani dhidi ya Baraza la Mawaziri inazidi kushuka.

Na Mwandishi Wa Majira


WAKATI Serikali ya Rais Jakaya Kikwete, ikitimiza miaka miwili siku tano zijazo, hali ya mambo inazidi kuwaelemea mawaziri wake wengi na sasa uchunguzi wa kina wa Majira Jumapili, umezidi kuonesha ni kwa nini imani dhidi ya Baraza la Mawaziri inazidi kushuka.


Kilicho dhahiri kwa sasa, uchunguzi huo umeonesha, ni kwamba wananchi hawataki mjadala tena, wameamua, mabadiliko ya watendaji hao ni muhimu sasa kuliko wakati wowote.


Malalamiko hayo ambayo yalikuwa yakionekana kupuuzwa, sasa yamepata nguvu baada ya utafiti wa asasi ya Utafiti wa Elimu ya Demokrasia ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, (REDET) kuonesha kuunga mkono, dhana kwamba utendaji wa mawaziri wengi hauwaridhishi wananchi, ingawa pia Serikali juzi ilikuja na tafsiri yake ikionesha kuwa inapendwa sana na wananchi.


Lakini pamoja na Serikali kuonekana inataka ‘kuunga unga ili kura zitoshe,’ utafiti wa REDET (bila kuingizwa tafsiri za kuunga unga) na maoni ya jumla ya wananchi wa kawaida na wachambuzi makini wa mambo,kwa pamoja vinaonesha kuna udhaifu mkubwa.Katika uchunguzi hii tunalichambua Baraza zima la Rais Kikwete na kuona udhaifu na nguvu zilizomo.


John Magufuli


Ni mtaalamu mwenye Shahada ya Uzamili kitaaluma na utendaji wake unafahamika. Huwa hana mchezo katika kusimamia taratibu za kazi, sheria na kanuni. Wataalamu wa sheria wanamweleza kama mtu anayefuata sheria kama zilivyo. Hakwepeshi.


Lakini hakuna kwa hakika ajuaye nini hasa kimemsibu, kwani makeke na kasi yake vimepungua, tangu alipohamishwa kutoka Wizara ya Ujenzi na kwenda Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, aliko sasa.


Pamoja na ukimya wake amekuwa akitamka bayana kutetea haki za wananchi katika masuala ya ardhi. Huyu ni jemedari ambaye kama Rais Kikwete anataka kumtumia katika maeneo yanayoonekana kuwashinda wengine, na akampa rungu kamili, wachambuzi wa masuala ya siasa na utawala, wanasema bado ni mtu muhimu.


Nazir Karamagi


Si mzoefu katika siasa, kitaaluma ni mtaalamu wa biashara na fedha. Kwa sasa ni Waziri wa Nishati na Madini, wizara ambayo imekuwa ikipigiwa kelele sana kiasi kwamba jina lake kila siku limo kwenye mijadala.


Kabla ya hapo, hakuwa akijulikana sana miongoni mwa mawaziri wa JK, lakini ameibuka tangu mjadala kuhusu mkataba wa Buzwagi ulipoibuliwa bungeni na Mbunge wa Kigoma Kaskazini (CHADEMA), Bw. Zitto Kabwe.


Bahati mbaya kwa Karamagi mbali na utata wa Buzwagi, ni kauli zake tata kuhusu mkataba huo, manufaa ya madini kwa ujumla na pia mambo yanavyoendelea katika shirika la Umeme nchini (TANESCO).


Hali hiyo imewapa wananchi fursa zaidi ya kumjadili Karamagi kwa kuegama katika matokeo ya matendo na uamuzi wake. Mtazamo wa wengi ni kuwa anahitajika mtu makini zaidi katika eneo la madini na nishati.


Bernard Membe


Anasifika kwa umakini na kutopenda ubabaishaji, na huwaambia ukweli hata viongozi wenzake wanapoonekana kukwamisha mambo. Ni mtaalamu wa utatuzi wa migogoro ya kimataifa, mwenye Shahada ya Uzamili aliyoipata Marekani.


Amechukua Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, ambayo ni nyeti na kuonesha makeke yake aliporejea ziarani kutoka Korea, Japani na China kwa kuwashangaa watendaji warasimu serikalini, ambao alisema alipokuwa huko aligundua kuna maeneo nyeti ya uwekezaji yanakwamishwa na urasimu.


Hana jambo zito kwa sasa linalowafanya wananchi wahoji utendaji wake, na wataalamu wanasema kama kuna watu JK anawahitaji katika kusafisha uzembe serikalini na kufikia visheni yake, basi huyu ni mmoja wao.


Dkt. Ibrahim Msabaha


Huyu kwa sasa unaweza ukashindwa kumzungumzia, kwa sababu tangu alipohamishiwa Wizara ya Ushirkiano wa Afrika Mashariki akitokea Nishati na Madini, amekuwa kimya. Akiwa Nishati na Madini, Dkt. Msabaha alipambana na wakati mgumu kiutendaji, pale nchi ilipogubikwa na mgao mkubwa wa umeme na huku jitihada za kuleta umeme wa dharura zikionekana kugubikwa na ‘usanii’, ambao sasa umelifanya hata Bunge kuunda Tume kuichunguza kampuni ya Richmond, iliyoelezwa kuletwa ili kuleta umeme wa dharura, lakini ‘ikaingia mitini’ katika mazingira tatanishi.


Dkt. Msabaha hawezi kuhukumiwa kwa alipo sasa, lakini kama ni kujadiliwa na kuhukumiwa, anaweza kufanyiwa hivyo kwa kuzingatia nafasi aliyokuwa nayo mwanzo.



Profesa Peter Msolla


Kama alivyokuwa mtangulizi wake katika Wizara ya Sayansi, Teknolojia na Elimu ya Juu, Dkt. Pius Ng’wandu, Profesa Msolla ni mmoja wa mawaziri ambao wamekuwa na wakati mgumu kutokana na wizara yake kuwa ni ya ‘hakuna kulala.’


Suala la utata wa utoaji wa mikopo kwa elimu ya juu, mbali na masuala ya kudumaa kwa Sayansi na Teknolojia nchini, ni kitanzi chake. Wakati fulani wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, waliwahi kumpigia kelele mbele ya Rais Thabo Mbeki wa Afrika Kusini alipofika kwenye ukumbi wa Nkrumah chuoni hapo.


Wanaoufahamu uwezo wa Dkt. Msolla, utendaji na ugumu aliokumbana nao katika miaka hii miwili, wanasema bayana, kuna wakati ameonekana kulemewa. Lakini kwa ujumla mikopo, ndilo suala linalomtia kitanzi.


Stephen Wassira


Ni mwanasiasa mkongwe vile vile amepewa wizara nyeti ya Kilimo, Chakula na Ushirika, akitokea ya Maji. Unyeti wa wizara hiyo na ukubwa wa majukumu na mageuzi ambayo Watanzania waliyatarajia, ni kitu cha kumpima.


Anaweza kuelezwa kuwa kutokana na muda wa miaka miwili aliyokaa, bado kuna mikakati mingi ukiwamo wa Kuboresha Sekta ya Kilimo, ndiyo imeanza kutekelezwa, lakini wasomi wanasema bado wizara hiyo ina mengi ya kuwatimizia Watanzania yanayopaswa kuonekana.


Dkt. Shukuru Kawambwa


Ni Daktari wa Falsafa kitaaluma, na amepewa wizara nyingine ‘korofi’ ya Maji. Bado ni mwanasiasa kijana na katika kipindi hiki, hajaonesha jambo lolote baya wala zuri sana kiutendaji. Wanaamini wachunguzi wa mambo bado anaweza kuwa ‘rasilimali’ kiutendaji, ingawa anatakiwa kuongeza kasi na kujiamini.


Zakia Meghji


Ni mwalimu kitaaluma, aliyehitimu Chuo Kikuu cha Dar es Salaam muda mfupi kabla ya akina Jakaya Kikwete, Edward Lowassa hawajajiunga na chuo hicho na zaidi mama huyu ni mwanasiasa mkongwe aliyekabidhiwa wizara nyeti ya Fedha, ambayo imetikiswa kutokana na misukosuko ya kiuchumi na tuhuma za ubadhirifu kwenye Benki Kuu.


Lakini mama huyu amesimama imara kusimamia uchumi na wahisani kuendelea kuwa na imani na Tanzania, lakini naye kama walivyo wengine waliojikuta wizara zao zikikumbwa na matatizo, anajadiliwa zaidi kwa udhaifu uliojitokeza katika wizara na mfumo wa uchumi wa nchi zaidi, kuliko utendaji wake binafsi.


Hawa Ghasia


Ameshika wizara ya Utumishi wa Umma ambayo nayo ni nyeti, kwa sababu ndiyo inayobeba matumaini ya watumishi wengi wa Serikali na ni mtawala kitaaluma.


Kwa sasa hawezi kuhukumiwa pamoja na kuwepo matatizo mengi katika sekta ya utumishi kwa sababu kuna mabadiliko makubwa yanafanyika kisheria na kiprogramu.



Dkt. Batilda Burian


Ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Bunge), utendaji wake bungeni umekuwa ukihojiwa sana hasa jinsi anavyozikabili hoja kutoka upande wa upinzani, lakini anatetewa kuwa waziri ana wajibu wa kusimamia sera za Serikali.


Zaidi ya hapo hana jambo kubwa linaloweza kumfanya atiwe kitanzini na kwa taaluma yake na uzoefu anaoendelea kuupata, anaweza kuelezwa kuwa ni rasilimali ya baadaye.


Kingunge Ngombale-Mwiru


Ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Siasa na Uhusiano wa Jamii). Ni mkongwe wa siasa ambaye alitarajiwa kuwa angeweza kusaidia katika eneo la uhusiano wa jamii na vyama vya siasa, hata hivyo imani ya wengi ni kuwa pamoja na utaalamu wake katika uhusiano wa jamii, kwani kitaaluma ni mwanasosholojia, ni kuwa Mzee Kingunge kwa umri na vipindi alivyoitumikia Serikali, alipaswa kupumzika na kuwapisha vijana.



Muhammad Seif Khatib


Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, katika kipindi chake, masuala mawili makubwa yameigubika wizara hiyo; Timu ya Taifa na mjadala wa Sheria mpya za habari nchini.


Akiwa mwanahabari na mwanamichezo, Seif amejipambanua na kujituma kuyashughulikia masuala hayo. Mafanikio katika sekta ya michezo bado yako katika mchakato wa habari. Hata hivyo wizara hii kuwa kiungo cha upatikanaji wa habari sahihi, Serikali imekuwa changamoto kuu. Hata hivyo hakuna jambo kuu linaloweza kuelezwa kuwa baya.


Bakari Mwapachu


Kama kuna wizara ambazo zimekumbwa na changamoto ni ya Usalama wa Raia inayoongozwa na waziri huyu. Ujambazi uliotikisa nchi na kukithiri kwa vitendo vya wananchi kulalamikia huduma za kipolisi na kwa namna fulani migomo ya wafungwa, viliwahi kuwafanya hata baadhi kufika mbali na kumjadili si kwa utendaji wake, bali kwa umri wake.


Dkt. Mary Nagu


Ni mtawala kitaaluma, lakini alionesha upeo mkubwa katika masuala ya sheria. Katika kipindi alichokaa amekuwa akisimamia ipasavyo masuala ya sheria. Lakini hata hivyo wizara yake imeendelea kubaki na changamoto ya wananchi kupata haki zao za kisheria kwa wakati na bila ‘kununua haki.’


Mjadala wa Katiba pamoja na kuwa katika wizara yake, umeonekana kupungua katika kipindi hiki. Naye anaweza kuelezwa kuwa ni ‘rasilimali’, kwa JK.



Basil Mramba


Yuko wizara ya Viwanda, Biashara na Masoko. Muundo wa wizara hiyo unaweza kumfanya mtu asione nini hasa kinafanyika, lakini amekuwa na kazi kubwa ya kuiuza Tanzania kimataifa na kushikiri katika uwekezaji taratibu nzuri za kibiashara. Ni mtaalamu wa biashara kitaaluma mwenye Shahada ya Uzamili, anaweza akapewa muda na akasaidia zaidi Taifa.


David Mwakyusa


Haonekani kama mwanasiasa, lakini yawezekana ni mtendaji zaidi. Hata hivyo wizara yake imekuwa na changamoto nyingi kuanzia uwajibikaji wa madaktari, rushwa na matatizo mengine ya kimaadili na ufikishaji wa huduma muhimu afya kwa wananchi.


Hata hivyo kama kuna jukumu zito zaidi na linaloweza kutumika ‘kumhukumu’, ni sakata la hivi karibuni la madaktari wa Muhimbili kuwafanyia wagonjwa wawili operesheni tofauti na walizopasa kufanyiwa.


Profesa Mark Mwandosya


Ni mtaalamu aliyebobea katika Mawasiliano. Wizara ya Mazingira aliyopewa inaonekana kuwa na changamoto nyingi zaidi huku yeye akionekana kupunguza kasi. Ni rasilimali nzuri, lakini inawezekana kuna baadhi ya maeneo yanamkwamisha kiutendaji.



Joseph Mungai


Naye kama Bw. Mwapachu, ana balaa la kukumbana na matatizo katika eneo lake kwa wafungwa kugoma. Lakini pia anahukumiwa sana kutokana na uamuzi wake wa nyuma kama vile kufuta michezo ya sekondari shuleni na masomo ya biashara.


Kinachoonekana kwa Mungai ni kwamba jinamizi la uamuzi wake wa nyuma, linaendelea kumwandama na maoni ya wengi ni kuwa akipumzishwa hakuna atakayeshangaa.


Dkt. Juma Ngasongwa


Ni kizingiti katika uchumi akiwa ni mtaalamu mwenye Shahada ya Uzamivu katika taaluma hiyo. Akiwa Waziri wa Mipango, Uchumi na Uwezeshaji, amekuwa mhimili katika mikakati ya kuimarisha uwezeshaji.


Hana kashfa kiutendaji na anaonekana ni mhimili katika midahalo muhimu ya kisomi kwa hulka yake ya kutokuwa na jazba, lakini ana changamoto kuu na inaelezwa ni kama vile Wizara yake imeshindwa kutafsiri takwimu za kukua kwa uchumi na kuwafikia wananchi. Hii inaweza kuwa hukumu yake.


John Chenge


Ni mwanasheria mwandamizi kitaaluma na baada ya kuwa Wizara Mpya ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki sasa ni Waziri wa Miundombinu.


Kikubwa kinachoweza kumfanya ahukumiwe ni utata wa masuala ya vivuko vingi nchini kuendelea kuwa kero kwa wananchi. Suala la sakata la mahujaji na utendaji wa kutia shaka katika Shirika la Ndege (ATC) ambalo kiutendaji liko chini yake, zinaweza kuwa sababu za yeye kuwekwa kitanzini zaidi.


Lakini hayo ni ya juzi tu, kubwa, wanasema wachambuzi wa mambo, Chenge hajaweza kufikia kasi katika usimamizi wa ujenzi wa barabara kama aliyokuwa nayo Magufuli. Hili linashangaza na kuacha swali: “Nini kimetokea?”



Mizengo Pinda


Naye ni mwanasheria mwingine katika Baraza la Kikwete ambaye anasifika kwa umakini wake katika kusimamia Sheria za Serikali za Mitaa na utendaji. Umakini wake ulipata kumfanya atajwe kuwa mmoja wa watu waliokuwa na uwezo wa kuchukua moja ya nafasi za juu zaidi kiutawala.


Hata hivyo, naye amekuwa kimya kiasi katika siku za karibuni, haoneshi makeke, haijulikani kama anabanwa kimfumo au anaendesha shughuli zake chini kwa chini, lakini anajitahidi, hakai ofisini, mara nyingi yuko mikoani.


Dkt. Hussein Mwinyi


Ni daktari wa binadamu kitaaluma, mwenye Shahada ya Uzamili (masters). Alipokuwa Wizara ya Afya akiwa Naibu Waziri katika Serikali ya Awamu ya Tatu, alikuwa mahiri zaidi hasa katika kujibu maswali bungeni na kusimamia utendaji.


Tangu alipopewa Wizara ya Muungano pamoja na kwamba anahusika katika mchakato wa masuala kama ya kutatua kero za Muungano na mchakato wa muafaka, inakubaliwa kuwa amekuwa kimya mno. Lakini kwa elimu na umri wake, bado wachambuzi wa masuala ya siasa, wanakiri ni rasilimali.


Kapteni John Chiligati


Ni mtawala kitaaluma na utendaji wake haujawahi kuibua shaka kuu, ingawa majukumu katika Wizara ya Kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana alikopelekwa akitokea Mambo ya Ndani, yanaonekana kuwa mengi na si ya matokeo yake kuonekana hivi karibuni.


Pia jukumu la kichama alilopewa hivi karibuni (Katibu Mwenezi CCM),linaweza kuonekana litaibua migongano ya kibiashara na kuwapa watu hoja ya kupingwa kwake kuendelea katika wadhifa wa kiserikali. Ana changamoto ya kutenganisha kati ya majukumu ya chama na ya Serikali.


Athony Diallo


Ana aina fulani ya utendaji usiopenda ubabaishaji kama alivyoonesha alipokuwa Wizara ya Maliasili na Utalii, lakini naye kama ilivyo kwa watendaji wengine inaonekana amekuwa kama vile amekuwa ‘akibanwa’ kimfumo, kutokana na maslahi ya baadhi ya watendaji wenzake.


Hata hivyo, Diallo alionekana kusimama kidete, japo wizara zilikuwa zikijikanganya katika utoaji wa taarifa, wakati wa suala la mlipuko wa ugonjwa wa Homa ya Bonde la Ufa. Akiwa Waziri wa Maendeleo ya Mifugo, bado sekta hiyo ina changamoto nyingi, athari hazijaonekana.


Phillip Marmo


Ni mwanasheria kitaaluma na anaongoza wizara nyeti ya katika Ofisi ya Rais, Utawala Bora. Ni mtu makini naye lakini kasi yake katika kutoka nje ya ofisi na kusimamia au kufuatilia masuala ya changamoto zinazoukabili utawala bora hasa masuala kama ya viburi vya watumishi wa umma na rushwa katika zabuni, utendaji wa umma na maofisi ya Serikali, anaonekana kuvishughulikia akiwa ofisini zaidi.


Margaret Sitta


Ni Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, ambaye kitaaluma ni mwalimu na ametoka katika harakati za vyama vya walimu. Mtazamo wa wengi ni kuwa anajitahidi kufuatilia kwa karibu ujenzi wa madarasa lakini bado wizara yake imekuwa na changamoto nyingi, pamoja na kuwspo miradi mingi ya kuboresha elimu, ubora wa elimu ya msingi na lengo la kuifanya angalau imfanye mtu awe na ujuzi wa kujitegemea uko mbali. Lakini mama huyu ni rasilimali kama ataongeza kasi na ubunifu zaidi.


Profesa Jumanne Maghembe


Kwa sasa ni Waziri wa Maliasili na Utalii. Ameingia katika wizara yenye changamoto nyingi kama vile za kuhakikisha misitu yetu haifutiki kwa biashara haramu ya magogo.


Suala la vitalu pia linaendelea kumbana, ingawa hivi karibuni ameonekana kupewa msukumo baada ya kufanyika mageuzi kadhaa katika watendaji kwenye Idara ya Wanyamapori.


Ni msomi na wakati fulani msimamo wake ni muhimu kwa nchi inayohitaji maendeleo na kasi ya haraka, lakini anahitaji kuongeza kasi na kujiamini zaidi huku pia akihitaji kuhakikisha anasimamia uamuzi wake.


Sophia Simba


Ni Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto. Ana uzoefu wa kutosha katika siasa, ingawa anaonekana naye kusumbuliwa na muundo wa wizara na majukumu husika.


Kwa wengi pamoja na majukumu ya wizara hiyo kutokuwa bayana sana na ikionekana yanashughulikiwa zaidi na wizara nyingine, hajaonesha ubunifu na neno jinsia limekuwa likionekana kuwa ni masuala ya wanawake.
Wakosoaji wanasema wizara hii haijaonesha jinsi gani inashughulikia na kutatua masuala ya jinsia (kwa maana ya wanawake na wanaume) na matatizo yanayowakabili.


Juma Kapuya


Baada ya miaka mingi katika masuala ya michezo, ilipoingia Serikali ya Awamu ya Nne, mtaalamu huyu wa masuala ya Baiolojia, amepelekwa jeshini. Kwa sasa hawezi kuhukumiwa vyema hasa kutokana na eneo aliko, lakini kwa ujumla anaonekana kama vile mmoja wa mawaziri ‘walioko likizo.’


Ajali aliyoipata hivi karibuni na kulazimika kulazwa India pia vimemfanya asiwe na nguvu zake za kawaida.



Hitimisho


Kwa ujumla, baadhi ya mambo ambayo wananchi wengi waliozungumza na gazeti hili, wanayaona ni kutowajibika kwa mawaziri ikiwa ni pamoja na wengi kuonekana ‘wamepumzika’.


Baadhi wanasikika kutoka ofisini zaidi kuliko kuonekana kwa wananchi huku wengine wakionekana kufanya kazi kwa kukurupushwa kwa amri kutoka juu, wao wakiwa hawana ubunifu wala mikakati mipya.


Mifano mingi imetajwa ukiwamo wa kuzunguka mikoani kwenda ‘kuitangaza bajeti’ na hata sasa ambapo wanaonekana wameibuka kuzungumza na wanahabari kuelezea mafanikio na mikakati ya wizara zao, ni dalili kuwa mawaziri wengi ama hawakuielewa vema visheni ya Serikali ya Awamu ya Nne au hawana mbinu za kuitekeleza falsafa ya Serikali hiyo.


Lakini pia baadhi yao wamekuwa wakionekana kutumia mtindo wa Zimamoto katika kupambana na matatizo au kero za wananchi na hatimaye kukosekana usimamizi wa dhati na matatizo kurudia palepale.


Maoni ya wananchi wengi pia waliozungumza na gazeti hili yanaonesha kwa hali hiyo, si tu inashinikiza kupatikana kwa mabadiliko ya haraka, bali pia ukubwa wa Baraza na visheni za watendaji watakaopewa nafasi kwa sababu, wataalamu wa masuala ya utawala na siasa, wanaona, hoja si kubadili watu, bali kuona utendaji wao makini, ni la muhimu zaidi kwa watanzania.


Source: Majira

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents