Habari

Mikataba Tanesco watoto mapacha

RIPOTI ya timu maalumu ya wataalamu iliyochunguza mikataba mingi kati ya kampuni za kuzalisha umeme na Shirika la Umeme nchini (TANESCO), inaeleza kuwa inafanana mithili ya watoto mapacha.

na Mwandishi Wetu

 

 

 

RIPOTI ya timu maalumu ya wataalamu iliyochunguza mikataba mingi kati ya kampuni za kuzalisha umeme na Shirika la Umeme nchini (TANESCO), inaeleza kuwa inafanana mithili ya watoto mapacha. Mikataba ambayo imeelezwa kufanana ni ile iliyoingiwa kati ya Tanesco na Richmond; Tanesco na Aggreko International Projects Ltd; Tanesco na Independent Power Tanzania Ltd ( IPTL); Tanesco na Alstom Power Rentals Energy (LLC) na mkataba kati ya Tanesco na Songas Limited.

 

Mkataba pekee ambao umeelezwa kuwa haufanani na hiyo ni ule baina ya Tanesco na Kampuni ya Wartsila.

 

“Tathmini linganifu ya mikataba husika iliyoelezwa hapo juu inaonyesha wazi kwamba, kutokana na muundo (form/format) uliotumika, mikataba yote ina vifungu ambavyo mpangilio wake na maneno yanafanana pasipo tone la tofauti,” inasema sehemu ya ripoti hiyo iliyoandaliwa na wataalamu watatu, ambayo Tanzania Daima ina nakala yake.

 

Timu hiyo ya wataalamu watatu (majina tunayo) iliundwa ili kutathmini mikataba ya uzalishaji na ununuzi wa umeme kati ya Tanesco na kampuni hizo, baada ya kuibuka kwa kashfa ya Richmond.

 

Ripoti hiyo, kimsingi, ndiyo inaimarisha hoja zilizotolewa na kamati teule ya Bunge, kuchungza mkataba wa Richmond Development Company LCC ya Marekani, ili kujiridhisha kuhusu uhalali wa masharti ya mkataba na gharama, kwa kulinganisha masharti yaliyomo kwenye mikataba mingine ya aina hiyo.

 

Kamati hiyo teule ya Bunge, iliyokuwa chini ya uenyekiti wa Dk. Harrison Mwakyembe (Kyela-CCM), ili kutekeleza ipasavyo maelekezo ya hadidu hiyo ya rejea, ilipendekeza kuwa kazi ya kufanya uchambuzi wa mikataba ya uzalishaji na uuzaji wa umeme na kutoa ushauri wa kitaalamu kwa kamati hiyo, ifanywe na timu ya wataalamu (wanasheria) wa Ofisi ya Bunge.

 

Timu hiyo iliundwa na watu watatu ambao ripoti yao ya kurasa zaidi ya 50 inabainisha kuwa Tanesco iliingia mikataba sita ambayo mitano kati yake inafanana kwa kiasi kikubwa.

 

Kwa mujibu wa ripoti ya timu hiyo, mikataba hiyo yote inafanana, isipokuwa ule wa Tanesco na Wartsila ya Finland, na kuwa kufanana huko kumeiweka Tanesco katika hali ngumu, kwani vipengele vingi vinayapendelea makampuni hayo.

 

Ikinyambulisha vipengele kadhaa katika mikataba hiyo, timu hiyo ya wanasheria ilibainisha kuwa katika baadhi ya mikataba, Tanesco ilikuwa na uhuru wa kujitoa, tofauti na ilivyowahi kuelezwa na viongozi wa serikali kuwa Tanesco haikuwa na uwezo wa kujitoa katika mikataba hiyo.

 

Mkataba ambao umeonyeshwa kama mfano katika ripoti hiyo ni ule wa Tanesco na Richmond, ambapo baadhi ya vipengele vinaipendelea Tanesco, kwani vilikuwa vinairuhusu kujitoa katika mkataba huo.

 

Timu hiyo ilibainisha kuwa Richmond ilibainika kutoa taarifa za uongo kuhusiana na usajili wake na suala hilo, kwa mujibu wa moja ya vipengele katika mkataba huo, vinaipatia Tanesco nguvu ya kujitoa katika mkataba huo.

 

“Utafiti wetu umebaini kuwa Kampuni ya Richmond Development Company LLC, ilitoa taarifa za uongo kuhusu uhalali wake kisheria wakati wa kuingia mkataba na TANESCO.

 

“Kitendo hicho ni cha ukiukaji wa mkataba kwa mujibu wa masharti ya kifungu 12.1(g) yanayotamka kwamba, Richmond Development Company LLC itakuwa imekiuka mkataba iwapo itatoa maelezo au taarifa ambazo itathibitika kuwa ni za uongo wakati zilipotolewa na ambazo zinaathiri uwezo wa kampuni hiyo kutekeleza majukumu yake yaliyoainishwa katika mkataba,” inasema sehemu ya ripoti hiyo.

 

Kwa mujibu wa masharti ya kifungu cha 12.3(c), Tanesco inayo haki ya kuvunja mkataba huo kutokana na kitendo hicho cha Richmond Development Company LLC cha kukiuka mkataba.

 

Pia Tanesco ilikuwa na uhuru na haki ya kuvunja mkataba kutokana na kujaa kwa maji katika mabwawa yanayozalisha umeme kama inavyofafanuliwa katika kifungu cha 12.4 cha mkataba huo.

 

Kwa mujibu wa kifungu hicho, hakuna madhara yoyote ambayo yangetokea kutokana na Tanesco kuvunja mkataba baada ya kuridhika na ongezeko la maji katika mabwawa yanayozalisha umeme.

 

Kifungu kingine ambacho Tanesco ingeweza kukitumia kuvunja mkataba huo ni ikiwa Richmond ingechelewa kutekeleza majukumu yake kama ilivyotokea, lakini Tanesco ikashindwa kuitumia fursa hiyo.

 

Wataalamu hao wanabainisha katika ripoti yao kuwa pamoja na Tanesco kuwa na haki ya kuvunja pia haki ya kulipwa fidia kwa mujibu wa kifungu cha 4.4 cha mkataba, shirika hilo la umma halikuzitumia kabisa haki hizo.

 

Wataalamu hao wanabainisha pia kuwa katika baadhi ya mikataba hiyo, vipo vifungu ambavyo vinainufaisha Tanesco na kuutaja mkataba baina ya Tanesco na Songas kuwa ni moja ya mikataba yenye vipengele vingi vinavyoinufaisha Tanesco.

 

Wakitoa mfano, wanasema kuwa kwa mfano, kifungu cha 2.3 cha mkataba baina ya Tanesco na Songas, Tanesco hailazimiki kununua umeme wote unaozalishwa na Songas, bali itanunua kwa kiwango kinachokidhi mahitaji yake, tofauti na ilivyo kwa mikataba mingine yote.

 

Aidha, chini ya kifungu cha 3.4, Songas inawajibika kulipia gharama za umeme wa Tanesco iwapo itautumia kwa ajili ya kufanya majaribio ya mitambo yake, dharura au kuwashia mitambo wakati katika mikataba mingine yote, Tanesco hailipwi gharama hizo.

 

Pia, kwa mujibu wa kifungu cha 4.9, Tanesco ina haki ya kurejeshewa gharama zote ambazo itakuwa inaziingia katika utekelezaji wa mradi wa Songosongo, iwapo Songas itakatisha mkataba kabla ya mradi huo kukamilika.

 

 

 

 

 

Source: Tanzania Daima

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents