Habari

Milioni 922/- zaibwa ATM ya CRDB

WATU watatu, akiwamo mfanyakazi wa Benki ya CRDB Tawi la Azikiwe, Dar es Salaam, wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakishitakiwa kwa kosa la wizi wa Sh milioni 922, mali ya benki hiyo.

Saida Amini


WATU watatu, akiwamo mfanyakazi wa Benki ya CRDB Tawi la Azikiwe, Dar es Salaam, wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakishitakiwa kwa kosa la wizi wa Sh milioni 922, mali ya benki hiyo.


Mwendesha Mashitaka, Hudson Ndusyepo aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Jackson Sinkolongo (32) mkazi wa Tabata Segerea ambaye ni mfanyakazi wa benki hiyo, Leonard Masanja (45), mhandisi na Paul Kijazi (42) ambaye ni mhandisi wa mazingira.


Mwendesha Mashitaka huyo alidai watuhumiwa hao walitenda kosa hilo kati ya Januari Mosi na Julai 3, mwaka huu, kwa kufanya njama za wizi kwa kutumia kadi za kutolea fedha katika mashine (ATM) na kufanikiwa kuiba Sh 922,760,000, mali ya CRDB tawi la Azikiwe, Dar es Salaam.


Mwendesha Mashitaka huyo alisema katika shitaka jingine, Sinkolongo anashitakiwa pia kwa kosa la kusababisha hasara kubwa kwa benki hiyo akiwa Meneja wa kadi za Visa.


Wakili wa upande wa utetezi, Mouris, aliiomba mahakama iwape dhamana washitakiwa hao, ombi ambalo lilipingwa na upande wa mashitaka.


Mwendesha Mashitaka Ndusyepo alisema washitakiwa hao hawaruhusiwi kupewa dhamana kutokana na kifungu cha sheria namba 76 cha mwaka 2002 kinachohusu uhujumu wa uchumi, kwa sababu kiasi walichoiba ni zaidi ya Sh milioni 10.


Hakimu Sundi Fimbo anayesikiliza kesi hiyo, alikubaliana na upande wa mashitaka na kukataa kutoa dhamana kwa washitakiwa hao, akisema kwa sheria hiyo mahakama haina mamlaka ya kutoa dhamana, ikiwa fedha zimezidi Sh milioni 10.


Kesi hiyo iliahirishwa hadi Agosti 7, mwaka huu, itakapotajwa tena na washitakiwa wamerudishwa rumande.


Source: Habari Leo

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents