Habari

Mishahara sekta binafsi yakwama

SERIKALI imezidi kujikanganya katika suala la mishahara ya sekta binafsi. Katika hatua ya kushangaza, jana ilitangaza kuundwa kwa kamati mpya, itakayopitia upya viwango hivyo na kutoa mapendekezo mapya.

na Mobini Sarya

 

 

 

SERIKALI imezidi kujikanganya katika suala la mishahara ya sekta binafsi. Katika hatua ya kushangaza, jana ilitangaza kuundwa kwa kamati mpya, itakayopitia upya viwango hivyo na kutoa mapendekezo mapya.

 

Hatua hiyo inatokana na msimamo uliowekwa na baadhi ya waajiri, ambao wamekataa katakata kulipa viwango vipya vya mishahara vilivyopangwa na kutangazwa na serikali mwishoni mwa mwaka jana.

 

Utafiti huo mpya umepangwa kuchukua siku 60, kuanzia Machi 10 mwaka huu, na katika kipindi cha utafiti huo, mishahara itakayolipwa ni ile iliyotangazwa na serikali Novemba mwaka jana.

 

Hata hivyo, katika hatua ambayo inaweza kuwa kilio, serikali imewapiga marufuku waajiri kuendelea kuwapunguza au kuwafukuza wafanyakazi wao kutokana na kisingizio cha mishahara, hadi pale mapendekezo ya utafiti huo yatakapotolewa.

 

Serikali imesema kwamba, hatua hiyo imechukuliwa ili kulinda heshima ya rasilimali watu na kuepuka waajiri kufunga biashara na viwanda, hali itakayoathiri kwa kiasi kikubwa uchumi wa nchi na wafanyakazi.

 

Taarifa ya kufanywa kwa utafiti mpya kuhusiana na viwango vya mishahara katika sekta binafsi, ilitolewa jana na Waziri wa Kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana, Profesa Juma Kapuya, wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salam, kuhusu kile alichokiita wingu kubwa la vurugu kuhusu ulipaji wa mishahara mipya.

 

Profesa Kapuya alisema kuwa serikali imeamua kufanya utafiti upya kwa kutumia wataalamu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, baada ya wizara yake kupokea malalamiko mengi kutoka kwa waajiri kuhusiana na viwango hivyo vipya.

 

Aidha, malalamiko kama hayo yamepokewa pia kutoka kwa wafanyakazi na vyama vya wafanyakazi, yakionyesha kuwa kumekuwepo na hali ya kutokuelewana kati ya waajiri na wafanyakazi kuhusiana na viwango vya mishahara, hali ambayo imesababisha kuwepo kwa vurugu na migomo katika maeneo ya kazi.

 

Alisema kiini cha vurugu hizo ni waajiri kudai kuwa viwango vipya vilivyotangazwa ni vikubwa mno na visivyolipika, ikilinganishwa na uzalishaji mdogo na gharama kubwa za uzalishaji.

 

Hata hivyo, kwa upande wa pili, wafanyakazi nao wamekuwa wakishinikiza kulipwa viwango vipya vya mishahara, wakidai kuwa kutokana na kupanda kwa gharama za maisha, viwango vya zamani vilikuwa havikidhi mahitaji yao ya kila siku.

 

Kufuatia malalamiko hayo, serikali imeomba ushauri kutoka kwa wadau mbalimbali, ikiwa ni pamoja na taasisi ijulikanayo kama LESCO, iliyopewa dhamana ya kuishauri serikali kupitia Waziri wa Kazi katika mambo yanayohusu ajira, uchumi na jamii.

 

Baada ya ushauri huo, serikali imeamua kumtafuta mtaalamu mwekezaji, atakayefanya utafiti wa kina juu ya athari zilizojitokeza kufuatia kutangazwa kwa kima kipya cha mishahara katika sekta binafsi na kuwasilisha matokeo ya utafiti pamoja na mfumo wa viwango vinavyofaa.

 

“Ufukuzaji na upunguzaji wa wafanyakazi kwa kigezo cha ongezeko la mishahara usimame hadi hapo utafiti utakapokamilika na waajiri wahakikishe kuwa matawi ya vyama vya wafanyakazi yanaanzishwa kwenye sehemu zao za kazi ili kurahisisha majadiliano,” alisema Profesa Kapuya.

 

Hata hivyo, Waziri Kapuya alisema kwamba wakati utafiti utahusisha wataalamu kutoka wizarani, vyama vya wafanyakazi na waajiri utakapokuwa unaendelea, wafanyakazi wanatakiwa kuacha kugoma na baadala yake wafanye majadiliano na waajiri wao kuhusiana na kiwango cha mshahara.

 

“Wakati tunasubiri matokeo ya utafiti, mishahara ya kima cha chini katika sekta binafsi kitaendelea kulipwa kama kilivyotangazwa katika tangazo la Serikali namba 223 la Novemba 16, mwaka jana. Majadiliano yafanyike baina ya wafanyakazi na waajiri, wakubaliane kiwango atakachomudu mwajiri, lakini kiwango hicho kisiwe chini ya sh 80,000,” alisema Waziri Kapuya.

 

Aidha, alisema kuwa endapo mwajiri atakaidi kufanya majadiliano na wafanyakazi au vyama vyao, achukuliwe hatua za kisheria na iwapo majadiliano hayo yatashindwa kuleta maelewano, pande zote mbili wanayo nafasi kupeleka malalamiko yao katika Kamisheni ya Usuluhishi.

 

Aliwataka wafanyakazi wafuate taratibu na sheria katika kudai haki zao na waache kuendesha migomo kwa madai ya mapunjo ya mishahara, kwa kuwa hilo si suluhisho la matatizo hayo.

 

Alisema iwapo wafanyakazi wataona kuwa mishahara wanayolipwa si sahihi, wazingatie taratibu, na kuonya kuwa si madai yote yanaweza kusuluhishwa kwa njia ya mgomo.

 

Mwezi Aprili mwaka jana, serikali iliteua Bodi za Mishahara katika sekta binafsi ili zifanye uchunguzi ulioleta mapendekezo ya kima cha chini cha mishahara katika sekta binafsi.

 

Hilo lilifanyika chini ya Sheria mpya ya kazi namba 7 ya Mwaka 2004, kifungu cha 35 (1).

 

Mapendekezo hayo yaliwasilishwa serikalini Septemba 27 na kuridhiwa na kutangazwa Oktoba 2007 na Waziri aliyekuwepo wakati huo, Kapteni John Chiligati, na viwango vipya vilitakiwa kuanza kutumika Novemba 1, 2007, lakini waajiri waligoma wakidai kuwa walikuwa hawajajiandaa kulipa mishahara hiyo mipya.

 

Hilo liliilazimisha serikali kubadili tarehe ya kuanza kulipwa kwa mishahara mipya hadi Januari mwaka huu, lakini hata hivyo migogoro baina ya waajiri na wafanyakazi iliendelea kila sehemu.

 

 

 

Source: Tanzania Daima

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents