Habari

Miswada kukwama tena

KUNA kila dalili za kukwama kwa muswada wa kutunga sheria ya Petroli na ile ya Umeme, inayotarajiwa kuwasilishwa na kujadiliwa katika kikao kijacho cha Bunge, endapo hakutafanyika marekebisho ya baadhi ya vipengele katika miswada hiyo, hasa ule wa umeme.

na Irene Mark

 

 

 
KUNA kila dalili za kukwama kwa muswada wa kutunga sheria ya Petroli na ile ya Umeme, inayotarajiwa kuwasilishwa na kujadiliwa katika kikao kijacho cha Bunge, endapo hakutafanyika marekebisho ya baadhi ya vipengele katika miswada hiyo, hasa ule wa umeme.

 

Kukwama kwa muswada huo kutasababishwa na msimamo wa awali wa wabunge waliodai marekebisho ya baadhi ya vipengele, kikubwa ni kutoingizwa kwa washindani binafsi kushindana na Tanesco katika sekta ya umeme.

 

Wabunge waliozungumza na gazeti hili juzi na jana baada ya kutolewa kwa ratiba ya vikao vya kamati za Bunge, walisema kuwa hawapingi kuanzishwa kwa ushindani katika sekta ya umeme, bali wanachotaka ni maandalizi yatakayohakikisha kuwa ushindani huo unalinufaisha shirika hilo la umma pamoja na mamilioni ya Watanzania wanaohitaji huduma ya umeme.

 

Walisema kwa upande mmoja, kabla ya kutungwa kwa sheria itakayoruhusu watu na makampuni binafsi kuwekeza katika sekta hiyo, serikali inapaswa kuifanyia marekebisho makubwa Tanesco, ili iweze kushindana katika mazingira ya kuimarika kibiashara.

 

Aidha, wanataka yafanyike marekebisho katika miswada hiyo ili wawekezaji hao walazimike pia kwenda katika maeneo ambayo kwa sasa hayajapata huduza za umeme, yakiwamo maeneo ya vijijini.

 

“Tunachoogopa ni kuwa sheria hii inaweza kutumika kuiua Tanesco, kwa sababu hali yake hivi sasa haitamudu ushindani, hivyo kuwaleta watu binafsi itakuwa ni kama kusaini kifo cha Tanesco,” alisema mbunge mmoja wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambaye hakuwa tayari kutajwa jina lake.

 

Mbunge mwingine, pia aliliambia gazeti hili kuwa iwapo miswada hiyo itaachwa kama ilivyo, kuna hatari wawekezaji wapya wakajazana katika maeneo ya mijini, ambako kimsingi huduma ya umeme inapatikana kwa kiwango kikubwa na kuyaacha maeneo ya vijiji yakiendelea kuwa gizani.

 

Wabunge hao wawili walisisitiza kuwa sheria hiyo itaiua Tanesco, na wao hawawezi kuliacha jambo hilo likitokee wakati wakiwa wawakilishi wa wananchi.

 

Katika mahojiano yake, Mbunge wa Wawi na Kiongozi wa Kambi ya Upinzani bungeni, Hamad Rashid (CUF), alisema, makubaliano ya wabunge baada ya semina iliyofanyika Februari 3 mwaka huu mjini Dodoma, ni kuwepo kwa marekebisho makubwa katika miswada hiyo kabla ya kuwasilishwa tena bungeni.

 

“Awali tulionyesha wasiwasi na concern yetu, katika semina iliyopita tuliwataka kusitisha suala hilo hadi baada ya kumalizika kwa sakata la Richmond.

 

“Tuliomba kupatiwa semina, watatuelimisha kwanza katika maeneo tuliyoyakataa awali, tukikubaliana wataupeleka bungeni na kama hawajatimiza tuliyotaka, tunao uhuru wa kuukataa muswada huo,” alisema Rashid.

 

Kwa upande wake, Mbunge wa Karatu, Dk. Willibrod Slaa (Chadema), alisema katika semina iliyopita wabunge walishauri mikataba yote itizamwe upya na kasoro zirekebishwe.

 

Aidha, wabunge pia walitaka sheria iliyounda Tanesco irekebishwe kabla ya kuletwa kwa muswada huo kutokana na ukweli kwamba kupitishwa kwa muswada mpya wa umeme ni kuliua shirika hilo.

 

“Kuletwa kwa muswada huu bila marekebisho ya sheria iliyounda Tanesco ni sawa na kuliua kabisa shirika hilo, kwani hakutakuwa na fair competition (ushindani wa haki), kwa sababu muswada huo unaruhusu exemption (msamaha) wakati kwenye Tanesco hakuna.

 

“Tunasema Tanesco ni uhai na usalama wa taifa, watakaporuhusu fair competition ikatokea kwamba nchi ipo kwenye hali ya hatari, makampuni hayo hayatakuwa tayari kutusaidia wakati huo Tanesco haijiwezi kiutendaji, unafikiri ni nini kama si ufisadi huo,” alisema.

 

Dk. Slaa alikwenda mbali zaidi na kusema kuwa kupelekwa kwa muswada huo bungeni na kuharakishwa kwa upitishwaji wake, kunaashiria sura na harufu ya rushwa.

 

Aliishangaa serikali kwa kuamua kuuleta muswada wa umeme hivi sasa wakati tayari kuna kampuni mbili binafsi zimeshaanza kazi katika sekta ya umeme bila ya kuwepo kwa sheria inayoruhusu kufanya hivyo.

 

“Sababu ya kuletwa kwa muswada huo na kuharakishwa kuupitisha kuna sura ya rushwa inayoonekana ndani yake. Kuna kampuni mbili tayari zimeanza kazi kwa lengo la kunufaika na muswada huo.

 

“Majina ya kampuni hizo ninayo, lakini nitayaweka wazi baadaye, siyo sasa. Tunalazimishwa kupitisha ili kuhalalisha utendaji wa makampuni hayo ambayo tunahitaji kujua yalianza kazi kwa sheria ipi,” alisema Dk. Slaa baaada ya kutakiwa kutaja majina ya kampuni anazozituhumu.

 

Alisema hata kama wabunge wa CCM wakiamua kutumia wingi wao na kuikubali miswada hiyo, wao wapinzani watasimamia haki ya walio wengi na kuipinga miswada hiyo kwa nguvu zao zote.

 

Taarifa iliyotolewa hivi karibuni kwa vyombo vya habari na kusainiwa na Ofisa Habari Mkuu wa Bunge, Ernest Zulu, inaeleza kwamba, wabunge watakuwa na semina kati ya Machi 25 na 26 mwaka huu, kuhusu miswada ya sheria ya serikali, wa petroli na wa umeme, iliyoandaliwa na Wizara ya Nishati na Madini.

 

Katika mkutano uliopita, wabunge waliicharukia serikali na kukataa kuwa kutumika kama chombo cha kupitisha ajenda binafsi kwa masilahi ya wachache, kutokana na upungufu uliobainika kuwamo kwenye miswada hiyo.

 

Miongoni mwa wabunge waliozungumza kwenye semina hiyo ni George Simbachawene (CCM), ambaye alieleza kuwa kuliko kuupitisha muswada huo wa umeme, ni heri angefariki dunia ili asione hayo yakitokea kwa sababu anaamini kuwa, kwa mtindo huo, baada ya miaka kumi, vinu vyote vya nishati nchini vitakuwa vimeshabinafsishwa.

 

Alisema sheria zilizopendekezwa zinalenga kuviweka vinu vyote vya kuzalisha umeme mikononi mwa wawekezaji huku serikali ikibaki kuwa mtumishi ndani ya nchi yake na wananchi wakiendelea kuwa watumwa.

 

Naye Mbunge wa Longido, Lekule Laizer (CCM), aliishangaa serikali kwa kupeleka muswada mwingine wa umeme huku utekelezaji wa sheria ya kupeleka huduma hiyo vijijini ikisuasua, licha ya kupitishwa zamani.

 

Katika semina hiyo, Mbunge wa Busega, Raphael Chegeni (CCM) alisema wakati umefika wa Bunge kuachwa lifanye mambo yanayotarajiwa na wananchi, kwani kipindi cha mhimili huo muhimu kuwa ‘rubber stamp’ umepita.

 

Alisema Tanesco haikufika hapo ilipo kwa bahati mbaya, bali ni kutokana na mikataba mibovu, ukijumuisha ule wa Net Group Solution, aliodai kuwa uliingizwa kwa nguvu ya serikali.

 

Akizungumza na gazeti hili jana, Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Adam Malima, alishindwa kueleza iwapo kuna mabadiliko yoyote yaliyofanywa katika miswada hiyo.

 

Hata hivyo, alisema kuwa miswada hiyo itafikishwa bungeni na ni imani yake kuwa wabunge wataiunga mkono. Waziri mwenyewe, William Ngeleja, hakupatikana kutoa ufafanuzi na inaelezwa kuwa yuko nchini Marekani.

 

 

 

 

 

Source: Tanzania Daima

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents