Burudani

Mixtape ya Antivirus inatetea muziki wa bongo flava? Sugu Azungumzia kukamatwa kwake:

Nyimbo ya I Wanna Kill Ru.., unaopatikana kwenye mixtape hiyo umepelekea Sugu kuitwa na kuhojiwa na polisi. Pamoja na mistari ya nyimbo hiyo kuwa mikali kidogo, lakini je, ni kweli kuwa Sugu anataka kuua au ni utundu tu wa mashairi?

Mixtape hii imeibua hoja kadhaa, moja ikiwa ya uhusiano kati ya redio na wasanii,

pamoja na nafasi ya redio katika kukuza sanaa nahata nafasi ya redio kuuwa sanaa. Neno bongo flava lilizaliwa redioni, na redioni huko huko ndipo bongo flava ilipolelewa na kukuwa mpaka hapa ilipofikia. Lakini je, redio zimefanya kazi ya kutosha kukuza ubunifu katika sanaa hii ya bongo flava? Kwani, swala la ma-Dj kuwa mameneja wa wasanii linapigiwa kelele kila siku, kwani ma-dj hao mamaeneja wanashukiwa kuwapendelea wasanii wao. Kama hii ni kweli, upendeleo huo ni ufa, tena ni ufa unaoweza kuhatarisha maendeleo ya sanaa hii inayoajiri vijana wengi.

Pamoja na yote, mashairi ya Sugu na wenzake katika mixtape hii yanaweza kuangaliwa katika pande mbili. Pande ya kwanza, ni kuwamashairi yao yanachochea chuki na hata kuleta fujo. Pande ya pili, ni kuwa mashairi yao yanaongea ukweli mtupu, na lugha kali waliyotumia ni kutokana na kuchoshwa na unyonyaji katika sanaa ya bongo flava. Inawezekana pia Sugu ameamua kujitoa muhanga na kutuonesha roho ya udhubutu, kwani Watanzania tuna sifa ya kukubali yaishe. Sasa basi, kama mashairi ya mixtape hii yataleta fujo, Sugu na wenzake watakuwa na kesi ya kujibu. Lakini kama tunakubaliana kuwa mabadiliko “changes” huja mara nyingi kutokana na mapambano ya aina fulani, basi Sugu ndio anatuonesha njia, kama Bob Marley alivyoimba Get Up Stand Up.

Swali, je Mixtape ya Antivirus inatetea muziki wa bongo flava dhidi ya wachache wanaouyumbisha au inataka kuchochea fujo zinazotokana na chuki kibinafsi? Sasa soma tamko rasmi alilotoa Sugu kwa vyombo vya habari juu ya kasheshe zilizomkumba siku mbili hizi tangia Mixtape ifike mtaani.
**********************************************************************************
Barua Ya sugu
napenda kuchukua fursa hii kuwafahamisha wananchi wenzangu wa Mbeya Mjini, wapenzi wa muziki wangu, wanachama wenzangu wa CHADEMA na watanzania kwa ujumla tarehe 28 Juni 2010 nilikamatwa na polisi kwa kile walichonieleza kuwa kuna malalamiko dhidi yangu kuwa nimemtishia kwa maneno kumuua Ruge Mutahaba kupitia wimbo uitwao “Wanna Kill” uliopo kwenye album iitwayo “Anti Virus”.

Walinikamata saa 5 asubuhi nikiwa naingia ukumbi wa Baraza la Sanaa Tanzania (BASATA) kwa ajili ya kutoa Mada kuhusu “Tathmini ya Muziki wa Kizazi Kipya na Hatma yake nchini” na kunihoji kwa takrabani masaa matano mpaka saa 10 jioni.

Wameniachia kwa kile walichonieleza kuwa ‘dhamana ya kujidhamini mwenyewe’ na kunitaka niripoti kwao siku ya jumatano tarehe 30 Juni saa 5 asubuhi siku ambayo nilipanga kwenye ratiba zangu kurejea nyumbani Mbeya Mjini kwa ajili ya kuchukua fomu ya kugombea ubunge kabla ya tarehe ya mwisho ya utoaji na upokeaji fomu ndani ya CHADEMA.

Katika mahojiano nao yaliyofanyika Makao Makuu ya Upelelezi Wizara ya Mambo ya Ndani; maofisa usalama (CID) walionihoji walirejea mstari mmoja katika kiitikio cha wimbo husika wenye maneno “I Wanna Kill Right Now” na kusema kwamba mlalamikaji ameutafsiri mstari huo kuwa ni tishio la kutaka kumuua.

 

Napenda kuwajulisha mashabiki wangu na watanzania wenzangu kwamba nimelieza wazi jeshi la polisi kwamba hakuna wimbo wala maneno niliyowahi kutamka kwa lengo la kukusudia kumuua binadamu yoyote. Niliwaeleza jeshi la polisi kwamba sanaa ya muziki inalugha zake zake za kifasihi.

Maadhui ya wimbo mzima yamejikita katika harakati zangu za siku zote za kupambana na wanyonyaji dhidi ya maslahi ya wasanii Tanzania na wimbo huo una maudhui ya kutaka “Kuondoa ama kuiua dhamira ya mbovu na nia zao ovu”.

Ni vyema mashabaki wangu, wanachama wenzangu na watanzania kwa ujumla wakarejea katika Kamusi mbalimbali za kimataifa ambapoo neno KILL linamaana zaidi ya 10 zikibeba pia maana ya KUKOMESHA, KUONDOA nk.

Katika wimbo huo nimeghani kwa kutumia fasihi mambo ya ukweli yanayotokea katika sekta ya sanaa na wala hauna dhamira yoyote wala maudhui ya kufanya kosa lolote la jinai; hivyo kama kuna mtu ameguswa na ukweli uliomo katika wimbo huo na hakubaliani nao basi aupinge kwa hoja ama akafungue madai badala ya kukimbilia kutaka kuliingiza jeshi la polisi kwenye masuala ya sanaa.

Aidha nimeshangazwa na hatua ya jalada hilo la polisi kufunguliwa ndani ya Makao Makuu ya Jeshi la Polisi Wizara ya Mambo ya Ndani yaliyopo Wilaya ya Ilala wakati mimi na mlalamikaji wote ni wakazi wa Wilaya ya Kinondoni.

Baada ya maelezo niliyoyatoa ni matumaini yangu kuwa jeshi la Polisi ambalo lina kazi muhimu zaidi ya kukabiliana na ujambazi na vitendo vingine vya uhalifu ambavyo vinazidi kuongezeka katika Mkoa wa Dar es salaam ambapo Makao Makuu ya Jeshi la Polisi yapo litaelekeza nguvu zake katika kukabiliana na vitendo hivyo vya makosa ya Jinai badala ya kupoteza muda wake kushughulikia masuala ya kifasihi ambayo yana sura ya madai yasiyo na uzito wowote.

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents