Mkaguzi Majengo ya BOT Apatikana

UKWELI wa gharama halisi zilizotumika katika ujenzi wa majengo pacha ya Benki Kuu (BoT), utafahamika baada ya kampuni ya Mekon Arch Consult Limited, kushinda zabuni ya kukagua tuhuma za kuwepo ufisadi katika ujenzi wa majengo hayo

UKWELI wa gharama halisi zilizotumika katika ujenzi wa majengo pacha ya Benki Kuu (BoT), utafahamika baada ya kampuni ya Mekon Arch Consult Limited, kushinda zabuni ya kukagua tuhuma za kuwepo ufisadi katika ujenzi wa majengo hayo.


Zabuni ya kutafuta mkaguzi wa miradi ya ujenzi wa majengo hayo yenye ghorofa 18 katika makao makuu ya BoT jijini Dar es salaam na jingine Gulioni, Zanzibar zilitangazwa mara mbili kabla ya Mekon kushinda.


Habari kutoka ndani ya BoT ambazo zimethibitishwa na Gavana wa benki hiyo, Profesa Benno Ndulu, zinasema mchakato wa zabuni umekamilika na kampuni hiyo ilianza kazi Novemba mosi.


Profesa Ndulu alisema kampuni hiyo ni muungano wa makampuni mengine mawili ambayo ni Burea For Industrial na A&E Associate Tanzania Limited.


"Tayari tumeipata kampuni ya wazalendo ya kukagua miradi yetu ya majengo kwa Dar es Salaam na Zanzibar, " alithibitisha Gavana Profesa Ndulu.


"Hii si kampuni ya kigeni, ni kampuni ya nchini na ni ya Watanzania walioungana na wamekidhi vigezo vyetu baada ya kutangaza mara ya pili."


Alisema zabuni hiyo ambayo awali ilitangazwa mwezi Aprili na kushindwa kumpata mzabuni, ilibidi itangazwe upya mwezi Juni.


"Tulitangaza zabuni mara mbili, mara ya kwanza hatukupata kampuni yenye sifa ikabidi tutangaze upya," alisema Prof Ndulu.


"Benki Kuu imekuwa ikitekeleza miradi miwili mikubwa, ambayo ni jengo la ofisi kuu lililopo Mtaa wa Mirambo, Dar es salaam na ujenzi wa tawi la Zanzibar katika eneo la Gulioni. Sasa baada ya malalamiko tukaona bora tuchunguze tujue ukweli uko wapi," alisisitiza Profesa Nduluna kuongeza:,


"Miradi yote karibu imekamilika na mjenzi ameshakabidhi sehemu ya majengo. Benki ingependa kupata na kufahamu thamani halisi ya fedha zilizotumika katika ujenzi hivyo tumetafuta mkaguzi huru kutoka kampuni binafsi ya kitaalamu," alisema Profesa Ndulu na kwamba, katika mchakato huo BoT imezingatia taratibu zote za Sheria ya Mamlaka ya Ununuzi wa Umma (PPRA), ya mwaka 2004.


Mradi wa majengo pacha ya BoT yaliyoko kitalu namba kumi, umekuwa ukidaiwa kwamba ulikuwa wa thamani kubwa tofauti na gharama halisi na tuhuma za kashfa hiyo ziliitikisa taasisi hiyo nyeti ya fedha ya nchi.


Hadi sasa kuna utata kuhusu thamani halisi ya fedha katika majengo hayo, huku taarifa ambazo serikali imekuwa ikizikana zikisema mradi huo umetumia zaidi ya Sh600 bilioni.

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents