Mkakati wa kuhifadhi Mazingira, Dk. Shein.

shein_m.jpgMakamu wa Rais Dk. Ali Mohamed Shein amesema pamoja na kuwepo kwa mafanikio katika utekelezaji wa Mkakati wa Kuhifadhi Mazingira ya Ardhi na Vyanzo vya Maji uliopitishwa mwaka 2006

 

Makamu wa Rais Dk. Ali Mohamed Shein amesema pamoja na kuwepo kwa mafanikio katika utekelezaji wa Mkakati wa Kuhifadhi Mazingira ya Ardhi na Vyanzo vya Maji uliopitishwa mwaka 2006, wananchi hawana budi kuweka jitihada za ziada ili kuyafikia malengo ya mkakati huo.

Aliyasema hayo jana mjini hapa wakati alipozungumza na wananchi wa Mkoa wa Shinyanga katika kilele cha maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani ambayo Kitaifa yamefanyika mkoani humu.

Mkakati huo uliopitishwa mwaka 2006 ambao umelenga katika kuzuia uharibifu wa mazingira kutokana na ukataji miti kwa ajili ya nishati na ujenzi wa nyumba na uchomaji moto, umeelekeza pia ushiriki wa wananchi katika kampeni ya kudumu ya upandaji miti.

“Mafanikio makubwa yameanza kuonekana katika utekelezaji wa mkakati huu, ikiwa ni pamoja na kuwapo kwa mtiririko wa kudumu wa maji katika mto Ruaha, hasa baada ya kuchukua hatua za kuwaondoa wafugaji waliovamia katika bonde la Usangu na kudhibiti kikamilifu matumizi ya maji katika bonde la mto huo,” alibainisha.

Aliyataja mafanikio mengine kuwa ni kwa mikoa mbalimbali kuainisha vyanzo vya maji vilivyopo kwenye mikoa yao na kuainisha maeneo yaliyoharibika na kuwataka wananchi kusitisha shughuli za maendeleo kwenye maeneo hayo.

Akielezea zaidi utekelezaji wa mkakati huo, Dk. Shein alisema lengo la upandaji miti kwa mwaka 2006/2007 lilifikiwa kwa asilimia 81 ambapo miti iliyopandwa ilikuwa ni 82,684,635. Hata hivyo, alieleza changamoto kubwa ni kuhakikisha miti hiyo inamea vyema.

Hata hivyo, pamoja na mafanikio hayo Makamu wa Rais alionya kuwa uharibifu wa mazingira bado unaendelea.

“Takwimu zilizopo sasa hivi zinaonyesha kwamba hekta za misitu zipatazo 91,300 hupotea kila mwaka hapa nchini. Upotevu huu wa misitu husababishwa zaidi na uvunaji usio endelevu wa mazao ya misitu na uchomaji ovyo wa misitu na nyika,” alieleza.

Kwa hiyo, Dk. Shein alitoa mwito wa kuendelea kuchukuliwa kwa hatua madhubuti kukabiliana na vitendo vya uchomaji moto ovyo wa misitu ambapo baadhi ya mikakati imependekezwa ni kwa vijiji kutumia elimu ya jadi na sheria ndogondogo katika ulinzi wa misitu dhidi ya uchomaji moto.

Awali, akimkaribisha Makamu wa Rais, Mkuu wa Mkoa huo, Yohana Balele alielezea hatua mbalimbali ambazo mkoa wake umekuwa ukizichukua kukabiliana na uharibifu wa mazingira, ikiwamo kuchukuliwa hatua za kisheria kwa wahalifu.

 

 

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents