Habari

Mkapa Afurahia Uamuzi Kuibinafsisha Benki ya NMB

Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu Mhe. Benjamin Mkapa, akimkabidhi kitabu Kaimu Mkurugenzi wa Benki ya NMB- Ruth Zaipuna wakati wa hafla ya kutambulisha na kutia saini kitabu chake iliyofanyika jijini Mwanza.

Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Benjamin Mkapa amesifu uamuzi wa Serikali yake kwa kuamua kuibinafsisha Benki ya NMB.

Akizungumza jijini Mwanza juzi wakati wa hafla ya kutambulisha kitabu chake cha: My Life, My Purpose – (Maisha Yangu, Dhamira Yangu), Rais huyo Mstaafu alisema suala la ubinafsishaji taasisi hiyo ulitokana na uamuzi wa mwanzoni mwa utawala wake mara baada ya kuingia madarakani mwaka 1995.

Ilipofika mwaka 1997, Serikali ya Rais Mkapa iliamua kuundwa kwa Benki ya NMB baada ya kugawanywa kwa iliyokuwa Benki ya Taifa ya Biashara (NBC).

Baada ya kuundwa kwa NMB mwaka 1997, mwaka 2005 serikali ya Rais Mkapa iliuza asilimia 49 ya hisa za NMB kwa wawekezaji wa Rabobank ya Uholanzi.

“Nafarijika kuona NMB ni miongoni mwa mabenki makubwa yenye mtandao mkubwa nchini ikihudumia wananchi wa kawaida hadi vijijini,” alisema Mkapa
Akionyesha kuchukizwa na wanaokosoa uamuzi wa ubinafsishaji uliochukuliwa na serikali yake, Rais Mkapa alisema watu wanatakiwa kuelewa kuwa wakati huo ilikuwa ni lazima kufanya uamuzi ili kuokoa pesa za walipakodi zilizokuwa zikipotea kwa kutolewa kama ruzuku ya kuendeshea mashirika ya umma.

Ndani ya kitabu chake, kuna aya inayosema wanaokosoa uamuzi wa ubinafsishaji wanapaswa kuelewa kuwa wakati huo, mashirika ya umma yalikuwa na hali mbaya kifedha kiasi kwamba serikali ililazimika kutumia kiasi kikubwa cha pesa za walipakodi kugharamia uendeshaji wa mashirika hayo. “…hiyo siyo kazi moja wapo ya pesa za serikali,” anaandika Mkapa.

Kaimu Mkurugenzi wa Benki ya NMB – Ruth Zaipuna akitoa mada kuhusu ubinafsishaji wa benki hiyo wakati wakati wa hafla ya utambulisho wa kitabu cha “My Life, My Purpose” kilichoandikwa na Mhe. Benjamin Mkapa, Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Akizungumzia mafanikio ya benki hiyo, Kaimu Mkurgenzi Mtendaji wa NMB, Ruth Zaipuna alisema kwa kipindi cha miaka 22 iliyopita, benki hiyo imejipambanua kuwa mfano bora wa uamuzi wa ubinafsishaji baada ya kufikia kuwa kimbilio la wafanyabiashara wadogo, kati na wakubwa kwa mitaji na ushauri wa kitaalam.

Kwa miaka 22 ya uwepo wake, Benki ya NMB imetoa jumla ya Shilingi trillioni 1.2 kusaidia biashara ndogo na za kati na mikopo mingine Shilingi trilioni 2.2 kusaidia wateja binafsi. Katika kusaidia wakulima, Bi. Zaipuna alisema mwaka huu wa 2020, Benki imepanga kufungua akaunti zaidi ya 300,000 za wakulima ili kuhakikisha kuwa wakulima wanapata malipo yao kupitia mfumo rasmi wa fedha na hivyo kuchangia katika kukuza huduma jumuishi za fedha (financial inclusion) hapa nchini.

Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu Mhe. Benjamin Mkapa katika picha ya pamoja na uongozi wa Benki ya NMB.

Bi. Zaipuna alisema Benki ya NMB imeendeleza ushirikiano wake na Mfumo wa Kielektroniki wa Malipo ya Serikali (Government's electronic payment system – GePG), ambapo mpaka hivi sasa taasisi 590 za serikali zimeunganishwa katika mfumo huo. Kupitia mfumo wa GePG, Benki ya NMB huwezesha kukusanya kwa jumla ya mapato ya serikali yapatayo Shilingi trilioni 2.1.

“Tunafanya hivyo kwa kutambua kuwa ni wajibu wetu kuunga mkono miradi ya kimkakati ya serikali.NMB ndiyo iliyokuwa benki ya kwanza kuunganishwa na mfumo wa GePG,” alisema.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents