Habari

Mkataba wa Buzwagi wasambazwa kama njugu

VYAMA vya upinzani vilivyoko katika ushirikiano wa kisiasa, vimegawa kama njugu nakala za mkataba wa uchimbaji wa madini wa mradi wa Buzwagi, wilayani Kahama ambao hoja yake ilimfanya Mbunge wa Kigoma Kaskazini Zitto Kabwe kufungiwa kuhudhuria vikao vya Bunge hadi Januari mwakani.

Na Muhibu Said


VYAMA vya upinzani vilivyoko katika ushirikiano wa kisiasa, vimegawa kama njugu nakala za mkataba wa uchimbaji wa madini wa mradi wa Buzwagi, wilayani Kahama ambao hoja yake ilimfanya Mbunge wa Kigoma Kaskazini Zitto Kabwe kufungiwa kuhudhuria vikao vya Bunge hadi Januari mwakani.


Umoja huo unaoundwa na vyama vya Chadema, CUF, TLP na NCCR-Mageuzi, ulianza kusambaza nakala za mkataba huo kwa kuwagawia waandishi wa habari katika mkutano ulioitishwa na vyama hivyo, makao makuu ya Chadema, jijini Dar es Salaam jana.


Katika tamko lao lililosomwa na Kaimu Katibu Mkuu wa Chadema, Victor Kimesera kwa niaba ya viongozi wenzake, vyama hivyo vimeeleza kuwa vimefikia uamuzi huo ili kutoa fursa kwa umma kuufahamu mkataba huo, kuujadili na kuujua mchakato uliosababisha usainiwe haraka.


Tamko la vyama hivyo, lilisainiwa na Katibu Mkuu wa TLP Taifa, John Komba, Naibu Katibu Mkuu wa CUF Taifa, Juma Duni Haji, Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa NCCR-Mageuzi, Sam Ruhuza na Kaimu Katibu Mkuu wa Chadema, Kimesera.


Viongozi hao walikutana na waandishi wa habari kuzungumzia majibu ya serikali kuhusu tuhuma kwa vigogo kumi na moja, wakiwamo mawaziri wa serikali ya awamu ya nne waliotuhumiwa na Mbunge wa Karatu ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa kuwa ni mafisadi waliohusika na ubadhirifu wa mabilioni ya fedha za umma.


Mkataba huo ulisainiwa na Waziri wa Nishati na Madini, Nazir Karamagi kwa niaba ya serikali na kampuni ya uchimbaji madini ya Barrick, jijini London, Uingereza.


“Tunachukua fursa hii kuanika wazi kwa umma, kupitia vyombo vya habari, mkataba wa uchimbaji wa madini Buzwagi ambao ni sehemu ya msingi wa tuhuma za ufisadi dhidi ya Karamagi. Katika hatua ya sasa tungependa kutoa nafasi kwa umma kujadili kuhusu yaliyomo pamoja na mchakato uliopelekea mkataba huo,” alisema Kimesera.


Akisoma tamko hilo, Kimesera alisema watasambaza orodha hiyo inayoitwa ya “mafisadi” kwa viongozi wa vyama hivyo wa mikoa, wilaya na kwa wananchi kwa ujumla.


Mbali na hilo, Kimesera alisema pia kuwa watafanya ziara nzima ili kuwaelimisha wananchi juu ya kile walichokiita “uporaji” au “utapanyaji” wa mali zao wanaodai kufanywa na baadhi ya vigogo wa serikali.


“Sisi kama viongozi wa vyama vilivyoko kwenye ushirikiano tutaisambaza orodha ya mafisadi nchi nzima kwa viongozi wa vyama vyetu mikoani, wilayani na kwa wananchi kwa ujumla pamoja na kufanya ziara ya kuwaelimisha wananchi wa Tanzania juu ya uporaji au utapanyaji wa mali zao,” alisema Kimesera.


Kimesera alisema wamefikia uamuzi huo baada ya baadhi ya viongozi wa ngazi ya juu serikalini kuzungumzia orodha ya vigogo hao bila kutoa majibu yanayoridhisha.


Viongozi hao walizungumzia orodha hiyo kwa nyakati tofauti siku chache baada ya Dk Slaa na mwanasheria wa Chadema, Tundu Lissu, kuitoa katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya Mwembeyanga, jijini Dar es Salaam, Septemba 15, mwaka huu.


Hadi kufikia jana, viongozi wa serikali waliokwishajitokeza na kuzungumzia tuhuma hizo ni watano ni pamoja na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utawala Bora), Philip Marmo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Siasa na Mahusiano ya Jamii), Kingunge Ngombale-Mwiru, Waziri wa Nishati na Madini, Nazir Karamagi, Waziri wa Miundombinu, Andrew Chenge na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Gray Mgonja. Mwingine ni Mbunge wa Musoma Vijijini ambaye pia ni wakili wa kujitegemea, Nimrod Mkono.


Tamko hilo limetolewa na vyama hivyo vilivyoko kwenye ushirikiano wa kisiasa, siku moja baada ya Waziri Karamagi kutangaza azma ya kufungua kesi mahakamani dhidi ya Dk Slaa, Gazeti la Mwana Halisi, kiwanda kilichochapisha gazeti hilo pamoja na wengine wote walioshiriki na wanaoendelea kushiriki katika kumdhalilisha.


“Hatutaogopa au kusita kutimiza wajibu wetu kwa wananchi wa Tanzania kwa sababu ya vitisho vya mashtaka dhidi ya viongozi wetu au dhidi ya vyama vyetu, tutaendelea na mchakato wa kuuanika wazi ufisadi na mafisadi,” alisema Kimesera.


Kimesera alisema pamoja na viongozi hao wa serikali kuzungumzia orodha hiyo, taarifa walizozitoa zinatofautiana.


“Kwa mfano Marmo amesema kwamba ushahidi wa ufisadi upelekwe kwenye vyombo vya dola, Kingunge amesema madai hayo ni uzushi mtupu na Chenge amekubali kuwa yeye ni mkurugenzi katika kampuni ya kigeni ya Tangold. Wakati huo huo Karamagi hajakanusha tuhuma juu yake, lakini amesema anakwenda mahakamani na amekwepa kuzungumzia mkataba wa Buzwagi ambao ni sehemu ya msingi ya tuhuma za rushwa dhidi yake,” alisema Kimesera.


Alisema mbali na hivyo, viongozi wengine wa serikali waliotajwa kwenye orodha hiyo, wamekaa kimya kwa wiki mbili tangu tuhuma hizo zitolewe dhidi yao. Kwa sababu za kisheria, kwa sasa hatuwezi kutaja majina ya viongozi hao.


Kimesera alisema kutokana na majibu yaliyotolewa na viongozi waliotajwa kutofautiana, imekuwa vigumu kwa wananchi kuelewa ni ipi kati ya taarifa zilizotolewa inawasilisha msimamo wa serikali na pia wanashindwa kuelewa iwapo misimamo hiyo tofauti ni mawazo binafsi ya hao mawaziri watano.


Pia kutokana na ukimya wa viongozi na watendaji wengine wa serikali waliotajwa, wananchi wanashindwa kuelewa iwapo kimya hicho maana yake ni kukubaliana na tuhuma za ufisadi zilizotolewa hadharani dhidi yao.


Alisema ukosefu wa msimamo wa serikali unaoeleweka, unatia wasiwasi mkubwa kwa wananchi kwa sababu tuhuma zilizotolewa ni nzito, zinahusu wizi au ubadhirifu mkubwa wa fedha za umma, matumizi mabaya ya madaraka ambayo yameliletea taifa hasara kubwa kiuchumi na pia yanawahusu viongozi wa ngazi za juu wa kiserikali.


Kimesera alisema pia tuhuma zilizotolewa zinahusu matukio mahsusi yaliyofanyika kwa vipindi vilivyotajwa na zinataja kiasi cha fedha zilizoibwa au vitendo vinavyoashiria matumizi mabaya ya madaraka na madhara yake kwa taifa.


“Hivyo tulitarajia serikali itoe majibu mahsusi hatua kwa hatua kuhusu tuhuma hizo badala ya kutoa majibu ya jumla,” alisema Kimesera.


Kutokana na kukosekana majibu ya mambo hayo, aliwaomba wananchi, vyombo vya habari na taasisi za kiraia kuendelea kuishinikiza serikali kutangaza msimamo wao kuhusiana na tuhuma hizo, pia vyombo vyenye mamlaka kisheria kuchukua hatua za kuchunguza matukio hayo ya ufisadi na kuwachukulia hatua wahusika.


“Hoja kwamba vyama vyetu vipeleke tuhuma hizo kwenye vyombo husika ni hoja potofu kwa sababu nyaraka zote zilizotajwa kuhusiana na ufisadi huu zimetoka serikalini,” alisema Kimesera.


Hata hivyo, Kimesera alisema mambo yaliyoelezwa na viongozi wa ngazi ya juu wa vyama hivyo katika mkutano wao na waandishi wa habari jana, ni madogo na kusema kuwa: “Mzinga wenyewe utapasuliwa kesho kutwa Ijumaa (kesho)”.


Akitetea uhalali wa kugawa nakala ya mkataba huo, kinyume cha Sheria ya Usalama wa Taifa ya mwaka 1976 inayozuia mtu wa kawaida kuwa na waraka wa serikali, Lissu alisema sheria hiyo ni miongoni mwa sheria zilizopendekezwa na ripoti ya Tume ya Jaji Nyalali kufutwa, lakini hadi sasa bado ipo.


Hata hivyo, alisema sheria hiyo imevunjwa na Katiba ya nchi Ibara ya 18 ambayo inatoa haki kwa kila raia kutoa na kupewa habari hivyo wana haki ya kugawa nakala ya mkataba huo kwa wananchi wa kawaida.


Akizungumzia kauli ya Kingunge iliyoziita tuhuma za Dk Slaa dhidi ya vigogo hao kuwa ni uchochezi, Lissu alisema sheria ya uchochezi, ilitungwa na wakoloni mwaka 1955 kwa lengo la kuwadhibiti wapigania uhuru wa Tanganyika mwaka mmoja baada ya harakati za kudai uhuru kuanzishwa na kwamba, mtu wa kwanza anayepaswa kutuhumiwa kwa suala hilo, ni hayati Mwalimu Julius Nyerere kutokana na hatua yake ya kuongoza harakati hizo.


Source: Mwananchi

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents