Habari

Mke abanwa na nondo dirishani, afa

MKAZI wa kijiji cha Isoko wilayani Chunya mkoani hapa, Bibi Hilda Kiyombo (35) amefariki dunia baada ya kubanwa na nondo za dirisha, akiwa amelewa alipojaribu kupita dirishani kuingia ndani.

Na Esther Macha, Mbeya


MKAZI wa kijiji cha Isoko wilayani Chunya mkoani hapa, Bibi Hilda Kiyombo (35) amefariki dunia baada ya kubanwa na nondo za dirisha, akiwa amelewa alipojaribu kupita dirishani kuingia ndani.


Akielezea tukio hilo jana, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mbeya, Bw. Suleiman Kova, alisema tukio hilo lilitokea Septemba 25 mwaka huu saa 7 usiku kijijini Isoko.


Kamanda Kova alisema chanzo cha kifo hicho ni Hilda kulewa pombe za kienyeji huku akitamba kuwa anakunywa kwa pesa yake na mumewe kumsikia akisema hayo kutokana na kilabu kuwa karibu na nyumbani kwao na kuamua kumfuatilia.


Kamanda alisema Hilda alipoambiwa na mumewe arudi nyumbani akalale alikataa na kumtaka mumewe huyo asimbabaishe kwani ataondoka kwa muda wake zake.


Mume aliposikia hivyo, aliondoka kurudi nyumbani na kufunga mlango kwa nje na kwenda kwa mkewe mkubwa.


Kamanda Kova alisema Hilda alipofika nyumbani akakuta mlango umefungwa na hivyo kuamua kuingia kwa kupitia dirishani.


Lakini kwa kuwa nondo hizo zilikuwa na nafasi ndogoaliingiza kichwa na kukwama dirishani na kwa kuwa alikuwa amelewa mawe aliyokuwa amepanga chini ili kupandia dirishani yaliteleza na nondo zikambana baada ya kuning’inia na kufariki dunia.


Kamanda Kova alisema mwili wa marehemu umeshakabidhiwa kwa ndugu baada ya uchunguzi wa Polisi kukamilika.


Wakati huo huo, mkazi wa kijiji cha Nkunywa, Mbarali, Bw. Jackson Kiyahulo (30), amejinyonga kwa kamba baada ya kuona wake zake wawili, ambao alikuwa anaishi nao nyumba moja kutoelewana.


Kamanda Kova, alisema tukio hilo lilitokea Septemba 26 mwaka huu saa 12 asubuhi.


Alisema chanzo cha kujinyonga ni kuchoshwa na ugomvi wa wake zake hao, ambao walikuwa wakigombana kila siku na hivyo kumfanya marehemu kuchukua uamuzi wa kujinyonga.


Kamanda Kova alisema wake za marehemu huyo walikuwa wanagombana kila siku na sababu za kugombana kwao hazikuweza kujulikana, kwani ugomvi huo ulikuwa ni wa kila siku, ambapo ulimfanya marehemu kukosa amani ndani ya nyumba.


Akielezea zaidi tukio hilo, Kamanda Kova alisema marehemu alikaa na kufikiri na kuona kuwa ugomvi wa kila siku ni kero nyumbani kwake, hivyo kuamua kujimaliza.


Kamanda Kova alieleza kuwa marehemu alijaribu kuwasihi wake zake hao kutokuwa na ugomvi, lakini uliendelea kila siku nyumbani kwake, ambapo marehemu alichoshwa na ugomvi huo ndipo alipoamua kujinyonga.


Aidha Kamanda Kova alisema mwili wa marehemu ulikabidhiwa kwa ndugu zake mara baada ya uchunguzi wa polisi kukamilika.


Source: Majira

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents