Burudani

Mkoba wa rais wa zamani wa Zimbabwe, Mgabe uliojaa Dola za Marekani waibiwa

Watu watatu wamefikishwa mahakamani nchini Zimbabwe, wakishtakiwa kuiba mkoba uliokuwa na $150,000 (£117,600) pesa taslimu mali ya rais wa zamani wa taifa hilo Robert Mugabe.

Kwa mujibu wa BBC, Washukiwa hao wa wizi wanadaiwa kutumia pesa hizo kununua magari, nyumba na mifugo.

Jamaa wa rais huyo wa zamani, Constantia Mugabe, ni miongoni mwa walioshtakiwa, kwa mujibu wa taarifa katika vyombo vya habari vya serikali.

Mwanamke huyo anadaiwa kuwa na funguo za nyumba ya kijijini ya Bw Mugabe iliyo eneo la Zvimba karibu na mji mkuu wa Harare, na ndiye aliyewasaidia hao wengine kuingia humo na kufika ulikokuwa mkoba huo.

Washukiwa hao wengine walikuwa wameajiriwa kama wafanyakazi wa kufagia na kusafisha nyumbani humo wakati wa kutekelezwa kwa wizi huo siku moja kati ya tarehe 1 Desemba na mapema Januari.

“Johanne Mapurisa alinunua gari aina ya Toyota Camry… na nyumba ya $20,000 baada ya kisa hicho,” mwendesha mashtaka wa serikali Teveraishe Zinyemba aliambia mahakama ya hakimu eneo la Chinhoyi.

“Saymore Nhetekwa alinunua gari aina ya Honda… na mifugo wengine wakiwemo nguruwe na ng’ombe wa thamani ambayo haijulikani.”

Bw Mugabe, ambaye kwa sasa ana amiaka 94, aliondolewa madarakani na jeshi la Zimbabwe kwama 2017.

Kufikia wakati wa kufurushwa madarakani, alikuwa amekaa madarakani kwa miaka 37, mwanzoni kama waziri mkuu na baadaye kama rais wa taifa hilo.

Wakati mmoja anakumbukwa kwa kusema kwamba taifa lolote lile haliwezi kufilisika.
Lakini alituhumiwa kwa kuishi maisha ya anasa wakati uchumi wa Zimbabwe ulipokuwa unaendelea kuporomoka.

Dola za Marekani huthaminiwa sana nchini Zimbabwe.

Kimsingi, huwa kuna noti za thamana zinazotolewa na benki ambazo thamani yake hutakiwa kuwa sawa na sarafu hiyo ya Marekani, lakini katika uhalisia huwa thamani yake inachukuliwa kuwa chini kuliko dola zenyewe.

Tangu alipostaafu, Bw Mugabe amekuwa akikabiliwa na matatizo ya kutembea na alikaa miezi kadha Singapore akipokea matibabu.

Haijabainika iwapo alikuwa nyumbani wakati wa kutekelezwa kwa wizi huo.

Washukiwa hao watatu waliachiliwa huru kwa dhamana.

Shirika la habari la AFP linasema kuna mtuhumiwa wa nne ambaye bado anasakwa na polisi.

By Ally Juma.


Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents